Mgomo huo ulianza asubuhi, ambapo wanafunzi walikusanyika katika uwanja wa mpira uliopo chuoni hapo huku Rais wa Wanafunzi, Damel Daniela akisisitiza wamegoma kutokana na mambo ya msingi.
Kaimu Mkuu wa Chuo, Profesa Casmir Rubagumya alisema atatoa taarifa kamili baada ya kumaliza kikao kati ya uongozi wa chuo na viongozi wa wanafunzi.
"Taarifa maalumu itatolewa mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo, kwa sasa sina cha kuongea mpaka tusikilize madai ya wanachuo," alisema.
Miongoni mwa mambo ambayo wanachuo wanadai yamechangia kugoma, ni chuo kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha ikiwemo maabara kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
Wanadai walimu wengi kutokuwa na sifa za kufundisha elimu ya juu, isipokuwa wanabebana kiundugu. Wanadai pia kukomolewa katika alama za ufaulu, kwani mwanafunzi anayetakiwa kurudia mtihani awe na alama zaidi ya 50 na hata akipata alama 49 atatakiwa kurudi nyumbani tofauti na vyuo vingine.
Inadaiwa walimu wanaofundisha kwa mkataba maalumu, wamekuwa wakikatwa asilimia 30 ya malipo yao, hivyo kuchangia wengi kukimbia na chuo kukabiliwana uhaba wa walimu.
Rais huyo wa wanafunzi alisema Chuo kimekuwa na sheria kandamizi, kwani ukipata alama za kurudia masomo matatu unarudi nyumbani, jambo ambalo limekuwa likiwaumiza wanafunzi wengi.
Pia, baadhi ya wanachuo wa shahada ya ualimu wa sayansi, walilalamika kuwa kozi yao haijasajiliwa na kwamba hawafahamu hatma yao licha ya kutoa ada.
Chanzo:Habari Leo