MDAHALO WA KATIBA WAKATISHWA NA VURUGU

Mdahalo uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini DSM umeshindwa kuendelea kutokana na vurugu zilizojitokeza ukumbini hapo.

Mdahalo huo uliokuwa unahusu Elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa ulikuwa umeandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kushirikisha waliokuwa makamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji mstaafu Joseph warioba.

Jaji warioba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuichambua Katiba inayopendekezwa, na kuelezea mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na masuala ambayo Bunge La Katiba limeyaacha kutoka katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume hiyo.

Katika maelezo yake, Jaji Warioba ameeleza kusikitishwa kwake na kuachwa kwa mambo ya muhimu ikiwa ni pamoja na miiko ya uongozi pamoja na Tunu za Taifa, lakini amepongeza baadhi ya mambo kuboreshwa ikiwa ni pamoja na Haki za Binadamu.

Kuhusu muundo wa muungano, Jaji Warioba amesema kuwa muundo uliopendekezwa katika Katiba Inayopendekezwa haufai na kuwa unasababisha mgogoro mkubwa zaidi wa muungano, hasa katika suala la kiuchumi.

Amesema Katiba hii inasababisha kile kinachoitwa koti la muungano kimekuwa kikubwa zaidi zaidi, na kuna uwezekana mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yakashindikana hali inayoweza kuzalisha kuwepo kwa nchi mbili zenye Katiba tofauti ndani ya nchi moja.

Wakati akielezea umuhimu wa kuweka miiko ya uongozi kwenye Katiba, ndipo baadhi ya vijana wakatoa mabango yenye ujumbe wakupinga hotuba ya Warioba na kuunga mkono katiba inayopendekezwa.

Bango mojawapo lilisomeka "TUMEIPOKEA, TUNAIKUBALI NA TUNAIUNGA MKONO KATIBA PENDEKEZWA"

Baada ya hapo kilichofuata ni vurugu zilizoambatana na mapigano miongoni mwao kati ya wanaounga mkono katiba na wanaopinga.