BROOKLYN BECKHAM AMWAGA WINO ARSENAL

Ni ajabu, kwamba safari hii maji hayajafuata mkondo! Mtoto wa nyota wa zamani wa Manchester United na England, David Beckham, Brooklyn amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Arsenal.

Brookyln aliyewahi kufanya mazoezi na klabu hiyo ya London amekataa kufuata nyayo za mzazi wake na kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 15 alikuwa akifuatiliwa kwa karibu na klabu kama Chelsea pamoja na hata Manchester United.

Jana, gazeti ya The Daily Star lilifichua kuwa Brooklyn ambaye ni mtoto wa kwanza waDavid na mwanamitindo Victoria Beckham amesaini mkataba wa awali wa mwaka mmoja baada ya kuwafurahisha makocha wa klabu hiyo wakati wa mazoezi aliyofanya klabuni hapo hivi karibuni.

Inadaiwa kwamba Arsenal wamekuwa wakimfuatilia chipukizi hiyo kwa muda mrefu na wapo tayari kumpa mkataba wa muda mrefu, endapo ataendelea kung'ara msimu huu.

Chanzo cha habari kilichonukuliwa na The Daily Star kimefichua kuwa Brooklyn ni kijana mwenye kipaji kikubwa , ameonyesha ukomavu na utulivu kwenye mazoezi, hata mechi za timu ya watoto ambazo amekuwa akichezeshwa.

Beckham aliyeichezea kwa mafanikio klabu ya Manchester United ana watoto wanne, ambao ni Brooklyn, Harper Seven, Romeo na Cruz.

Nguli huyo wa zamani alizichezea timu mbalimbali ambazo ni Manchester United, Preston North End, Real Madrid, Milan, Los Angeles Galaxy, Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya England, ambayo imemfanya kuwa na rekodi ya kucheza michezo mingi zaidi.

Beckham ameichezea England michezo 115.