Kukamatwa kwa Mapengo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa aliyesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumchoma kisu kifuani na tumboni mkazi wa mjini Tarime, Isack Mwita Matutu (20) nakumsababishia kifo kabla ya kumshambulia mfanyabiashara Deus Tenten pia wa hapa aliyejeruhiwa shingoni.
Kamanda Mambosasa, akielezea mkasa huo, alisema: "Tukio hilo la mauaji ya kijana Isack Mwita Matutu yalitokea saa 4 usiku wa kuamkia Jumatano (jana) katika Baaya Criss Pub ambapo kulitokea ugomvi kati ya mtuhumiwa na marehemu alikuwa akinywa na wenzake katika baa hiyo ambapo mtuhumiwa alichomoa kisu na kumchoma Isack kifuani na tumboni na kufariki muda mfupi kabla hajafikishwa katika Hospitali ya Wilaya kwa matibabu.
"Lakini pia akamjeruhi mfanyabiashara Deus Tenten shingoni ambapo majeruhi alikimbizwa hospitali haraka na kutibiwa na hali yake haijaimarika. Tunamshikilia Chacha Mapengo kwa mahojiano zaidi. Naye anatibiwa kwa sababu alishambuliwa na wananchi kabla ya kuokolewa na askari wetu waliowahi eneo la tukio."
Alisema mtuhumiwa huyo anahusishwa kutishia watu maisha, na kwamba tayari ana kesi katika Mahakama ya Wilaya Tarime ya kumtishia maisha Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mkoa wa Mara Ben Usaje.
Pia ana kesi ya kumchoma kisu tumboni mkazi wa Sirari, wilayani hapa aitwaye Soko Waisaki na kumsababishia ulemavu.