MWANAMKE ATUPWA JELA KWA KUSAIDIA ISIS

Mwanamke mmoja nchini Uingereza aliyeshitakiwa kwa kumfadhili mumewe aliyejiunga na vita nchini Syria, amefungwa jela kwa zaidi ya miaka miwili.

Amal El-Wahabi, mwenye umri wa miaka 28, alijaribu kumhadaa rafiki yake kumbebea pauni 15,800 hadi nchini Uturuki ambako mumewe angeweza kuzichukulia.

Jaji aliyetoa uamuzi katika kesi hiyo, Nicholas Hilliard, alimwambia El Wahabai kuwa alifahamu vyema kwamba mumewe Aine Davis alikuwa anapigana nchini Syria na kwa hivyo alikuwa anamsaidia katika harakati zake.

Davis, ambaye alikuwa mlanguzi wa dawa za kulevya pamoja na kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha, aliondoka Uingereza mwaka 2013 kwenda Syria kupigana na kundi la Isis.

Jaji alisema kuwa El-Wahabi anapaswa kutumikia sehemu ya kifungo chake jela na kabla ya kuachiliwa kumalizikia kifungo hicho nje.

Jaji aliongeza kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa huruma kwani mwanamke huyo ni mama wa watoto wawili wachanga.

Mapema mwaka huu Davisa ambaye anajulikana kama Hamza alimtaka mkewe kumtumia pesa hizo kupitia nchini Uturuki.

El-Wahabi, kutoka London alimuomba rafiki yake wa zamani, Nawal Msaad,kumbebea pesa hizo akimuahidi kumlipa Euro 1,000 kwa kumshukuru.

Hata hivyo, mpango huo ulitibuka baada ya Msaad kusimamishwa katika uwanja wa Heathrow na kukiri ni kweli alikuwa amebeba pesa hizo. Pesa hizo alikuwa amzificha kwa nguo zake za ndani.

Bi Msaad alisema hakujua pesa hizo zilikokuwa zinakwenda na kwa hilo mahakama ikamwachilia.

Katika hukumu yake jaji alisema ni wazi kuwa mumewe El-Wahabi alikwenda Syria kupigana chini ya kundi la kiisilamu la Isis.