Tukio hilo lililothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Longinus Tibishubwamu, limetajwa kutokea jana saa moja na dakika 45 asubuhikatika eneo la Mhunze, Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa Kamanda Tibishubwamu, kitu hicho kinachodhaniwa kuwa bomu kililipuka ndani ya gari lenye namba za usajili T848 AKA aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Mohammed Hemed Zahoro, mkaziwa Ngara lililokuwa linaendeshwa na Khalifa Mussa (39), mkazi wa Ngara mkoani Kagera.
Alisema Rashid aliyekuwa utingo wa gari hilo, alikufa papo hapo baada ya mlipuko huo uliotokea ghafla na kujeruhi pia watu wengine watatu waliokuwa ndani ya gari hilo.
Aliwataja majeruhi kuwa ni Donald Nzugirwa alijeruhiwa mkono, Seni Edward aliyejeruhiwa bega na Maganga Pius aliyejeruhiwa paja, mkono na sehemu za mgongoni. Dereva wa gari hilo hakujeruhiwa popote.
Alisema majeruhi wametibiwa katika hospitali ya mkoa na kuruhusiwa ikiwa jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi juu ya chanzo cha tukio hilo.
Chanzo: Habari Leo