MTU MMOJA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI KIFUANI NA KICHWANI

Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la John Salehe (32) Mkazi wa Kijiji cha Itenka Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoani hapa ameuwawa kikatili kwa kupigwa risasi kichwani na kifuani na mtu asiye julikana wakati akiwa anakunywa pombe kwenye baa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la polisi wa Mkoa wa Katavi kamishina msaidizi mwandamizi Dhahiri Kidavashari tukio hilo la mauwaji ya kinyama lilitokea hapo juzi kijijini hapo majira ya saa mbili kamili usiku

Alisema kabla ya tukio hilo marehemu alikuwa amekaa akinywa katika baa moja iliyopo kijijini hapo inayomilikiwa na mkazi mmoja wa kijiji hicho cha Itenka aitwaye Mussa Juma(DEO).

Alieleza marehemu alifika kwenye baa hiyo toka majira ya saa kumi na moja jioni na toka muda huo aliendelea kunywa pombe kwenye baa hiyo huku akiwa na baadhi ya watu ambao nao pia walikuwa wakinywa pombe kwenye baa hiyo ya Mussa Juma ambayo ni maarufu kijijini hapo kwa kuuza pombe za aina ya bia mbalimbali Ndipo muuaji huyo asiye fahamika alifika hapo na kufyatua risasi mbili zilizompiga marehemu kifuani na kichwani na marehemu alifariki hapo hapo.

Kidavashari alieleza kuwa katika tukio hilo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la James Omar(30) Mkazi wa Kijij hicho cha Itenka ambae nae alikuwa kwenye eneo hilo alijeruhiwa kwa kupigwa na risasi moja na bunduki aina ya SMG kwenye maeneo ya kiunoni.

Alisema majirani wa eneo hilo baada ya muda walifika kwenye eneo hilo kwa lengo la kutowa msaada hata hivyo walikuta muhusika aliyafanya tukio hilo alikuwa ameisha tokomea mahari kusikojulikana Chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na wala hakuna mtu wala watu waliokamatwa kuhusiana na mauwaji hayo ya kikatili ya mtu huyo.

Kamanda Kidavashari alisema jeshi la Polisi Mkoani Katavi linaendelea kufanya msako mkali ilikuweza kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika mauwaji hayoili sheria iweze kuchukua mkondo wake.