WATUPWA JELA KWA KUCHEZA WATUPU KWENYE VIGODORO

WAKAZI wanne wa eneo la Masasi Mbovu katika Halmashauri ya mji Masasi mkoani Mtwara wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kucheza wakiwa watupu kwa mtindo wa 'vigodoro' kwenye sherehe ya ndoa.

Akitoa hukumu hiyo juzi hakimu wa mahakama ya wilaya ya Masasi, Halfani Ulaya alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 30 mwaka huu kwa makusudi hukuwakijua ni kosa la jinai na ukiukwajiwa maadili ya kitanzania.

Waliohukumiwa kwenda jela ni Anna Yohana (25), Aziza Chukachuka (20) Jemima Jordan (22), huku mtuhumiwa mmoja ambaye ni mtoto mwenye umri wamiaka 17 (jina limehifadhiwa) akitakiwa kulipa faini ya Sh 50,000 kutokana na umri wake kuwa mdogo.

Kwa mujibu wa hakimu Ulaya, ameridhishwa na upande wa utetezi ulioletwa na mashahidi watatu mahakamani hapo na kwamba uamuzi huo ni wa haki na kisheria kwani walitenda kosa la jinai namba 167 ya mwaka 2014.

Washtakiwa hao walipotakiwa kujitetea hawa kusema chochote na kwamba wote wamekiri kuwa kwa makusudi walitenda kosa hilo huku mahakama ikitoa onyo kali kwa watakaobainika kuendelea na vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume na maadili ya Watanzania.

HELKOPTA YA KUPAMBANA NA MAJANGILI YAANGUKA YAUA WANNE

HELIKOPTA ya Wizara ya Maliasili naUtalii, iliyotolewa msaada kwa ajili ya kupambana na majangili Juni mwaka huu, imeanguka na kuua watu wanne, waliokuwa katika helkopta hiyo wakiwemo marubani wawili wa Jeshi la Polisi, askari mmoja na rubani mwingine ambayeni mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Helikopta hiyo aina ya Robertson R44 yenye thamani ya Dola za Marekani 500,000 (Sh milioni 800), ilitolewa msaada na Taasisi ya Howard Buffet kwa ajili ya kusaidia mapambano hayo.

Ajali ya helikopta hiyo iliyokuwa ikimilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), ilitokea jana saa 4:00 asubuhi maeneo ya Kipunguni B, Moshi Bar, wilayani Ilala, wakati ilipokuwa katika ukaguzi wa kawaida.

Akizungumza katika eneo la ajali, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana na upelelezi unaendelea kujua chanzo.

Kamanda Kova aliwataka wananchi na wakazi wa eneo hilo, kutosogea karibu na mabaki ya helikopta hiyo, ili kuepusha madhara makubwa zaidi yanayoweza kutokea kutokana na kuwepo kwa viashiria vya moto.

"Tunaomba msisogee karibu na eneo hili la ajali, panaweza kulipuka hapa na kusababisha madhara makubwa zaidi, tuchukue tahadhari na tukae mbali na eneo hili," alisema Kova.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidi (ACP), Hamis Suleiman, alitaja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Mrakibu waPolisi Kapteni Kidai Senzala, Mkaguzi wa Polisi Kapteni Simba Musa, Konstebo wa Polisi, Josso Selestine na Kapteni Joseph Khalfan.

Helikopta hiyo ilikuwa na namba 5H- TWA. Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alipongeza wananchi hao kwa kutoa taarifa mapema zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza madhara.

Hata hivyo Sadiki alitaka wananchi kutokimbilia maeneo ya tukio la ajali kama hizo zinapojitokeza kwani kuna uwezekano mkubwa wa wao kupata madhara yanayoweza kusababishwa kulipuka kwa chombo hicho.

Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema waliona helikopta hiyo ikiyumba na kutoa mngurumo usio wa kawaida na baadaye ikazima ambapo rubani alijaribu kuiwashwa bila mafanikio, lakini baadaye ilianguka.

"Tulisikia mlio wa helikopta usio wa kawaida na baadaye ilizima na kusikika tena ikiwashwa ikagoma ndio baada ya muda mfupi, tukasikia kishindo kikubwa cha helikopta hiyo kuanguka," alisema shuhuda huyo.

SHEKHE PONDA AACHIWA HURU

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Issa Ponda kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yake.

Shekhe Ponda aliwahi kutiwa hatianina Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 2, mwaka jana, kwa kosa la kula njama kuingia kwa nguvu katika eneo lililopo Chang'ombe wilaya ya Temeke na kupewa adhabu ya kifungo cha miezi 12 jela.

Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Augustine Shangwa alisema ushahidi uliotumika Mahakama ya Kisutu kumtia hatiani Shekhe Ponda ulikuwa na mapungufu hivyo uliachashaka.

Alisema upande wa mashitaka haukuthibitisha kwamba Shekhe Ponda aliwaamuru wafuasi wake kuvamia katika eneo hilo. Licha ya Ponda kuachiwa huru, bado anakabiliwa na mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro alikokuwa na kesi ya uchochezi.

Shekhe Ponda alishitakiwa katika Mahakama hiyo Agosti 19, mwaka jana, akikabiliwa na mashitaka matatu ya kutotii amri halali ya Mahakama.

Mwendesha mashitaka alidai kwamba Shekhe Ponda walifanya makosa hayo Agosti 10, mwaka jana katika Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro. Ponda alidaiwa kukiuka amri ya Mahakama kwa kutoa kauli za uchochezi na kuichochea jamii kufanya fujo.

Kulingana na mwendesha mashitaka, Shekhe Ponda alichochea waumini wa Kiislamu na kwamba Baraza Kuu la Waislamu waTanzania (BAKWATA), walikuwa ni vibaraka wa CCM na serikali na hivyo wanapaswa kuwapiga.

Taarifa hiyo alidaiwa kupinga agizo la Mahakama ya Kisutu.

Inadaiwa kwamba kwa misingi hiyo, kauli iliyotolewa na Ponda ni ya uchochezi kwa makusudi, akisema serikali iliingiza jeshi Mtwara ili kuleta machafuko ya wananchi ambao walikuwa wanapinga ujenzi wa bomba la gesi.

YAMETIMIA ESCROW

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imependekeza kutenguliwa kwa nyadhifa na kuwajibika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kutokana na sakata la fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.

Mbali ya mapendekezo hayo, Kamati hiyo imependekeza pia wote waliochukua fedha kutokana na kashfa hiyo iliyohusisha Sh bilioni 306, wafilisiwe mali zao na kushitakiwa mahakamani.

Wanaotajwa kutakiwa kutenguliwa kwa nyadhifa zao mbali ya kuwajibika kwa Pinda ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Naibu wake, Stephen Maselle, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliachim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Kamati hiyo ilitoa mapendekezo yake hayo kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akisoma maoni na mapendekezo yaKamati baada ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe kusoma sehemu ya uchambuzi wa sakata hilo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema kwa uzito na unyeti wa suala hilo, Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutotekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ilikurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.

Kwa mujibu wa Filikunjombe, baadaya kupitia vielelezo vilivyomo katikaripoti ya CAG, "Kamati imejiridhishapasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu alikuwa na taarifa zote kuhusu mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow."

"Ushahidi ulioletwa na Ofisi ya CAG kwenye Kamati unaonesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili. "Na Kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huu usifanyike," aliongeza Makamu Mwenyekiti huyo, na kubainisha kuwa Pinda pia aliwahi kunukuliwa akisema fedha za Escrow si za umma.

Kuhusu Profesa Muhongo, Kamati ilieleza kuwa alifanya udalali wa kuwakutanisha Harbinder Sethi na James Rugemalira (waliokuwa wamiliki wa Independent Power Tanzania Limited) na kuwa alilipotosha Bunge kuhusu fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwamba ndani ya fedha hizo, hakukuwa na fedha za umma."

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, aidha kwa makusudi, ama kwa sababu anazozijua vizuri zaidi mwenyewe, Waziri wa Nishati na Madini ananukuliwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge, kwa nguvu kubwa na kwa kujiamini, akitetea uchotwaji wa fedha hizo kinyume cha masharti ya mkataba wa Escrow," alisema Filikunjombe.

Alisema iwapo waziri huyo angetimiza wajibu wake kidogo tu na ipasavyo, fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama Kodi ya Ongezekola Thamani (VAT), Capital Gain Tax na ushuru wa stempu ambazo ni sawa na takribani Sh bilioni 30.

"Kamati inapendekeza kuwa mamlaka yake ya uteuzi, itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na sababu zilizoelezwa," alisema.

Akimzungumzia Maselle, Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha kuwa alisema uongo bungeni kwa kutamka kauli ambazo zilikuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow, ikiwemo kutoa kauli ambazo zingeweza kusababisha nchikuingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.

"Kamati inapendekeza kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini)achukuliwe hatua kali za kinidhamu,ikiwemo kutenguliwa uteuzi wake.
"Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu Waziri huyu afikishwe mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe kama mbunge kwa kusema uongo bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge wengine kuhusu kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu," aliongeza Filikunjombe

Kuhusu Mwanasheria Mkuu Jaji Werema, Kamati ilisema imethibitisha kuwa alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya Tanzania kuhusu hukumu ya Jaji John Utamwa kwa kutumia madaraka yake vibaya.

Alisema Jaji Werema aliagiza kodi ya Serikali yenye thamani ya Sh bilioni 21 isilipwe na hivyo kuikosesha Serikali mapato adhimu."

Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwakujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow ulikuwa ni mgogoro wa wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya Tanesco na IPTL.

"Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe na mara moja afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababisha Serikali kupoteza mabilioni ya fedha," alisema Filikunjombe.

Akimzungumzia Katibu Mkuu Maswi, Makamu Mwenyekiti huyo wa PAC alisema Kamati inapendekeza uteuzi wake utenguliwe na Takukuru wamfikishe mahakamani mara moja, kwa kuikosesha Serikali mapato na matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.

Kamati ilisema imethibitisha Maswi amefanya uzembe wa hali ya juu wakushindwa kujiridhisha kuhusu masharti ya sheria ya kodi, na pia imebaini kuwa hakujiridhisha uhalali wa Kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kulipwa kwa asiyestahili kinyume cha mkataba wa akaunti ya Escrow.

BARIDI YAGANDISHA BREKI ZA NDEGE

Abiria waliokuwa wanafanya safari na shirika ka ndege la Serbia walilazimika kushuka katika ndege hiyo na kuisukuma baada ya breki zake kuganda na kushindwa kuondoka.

Ndege hiyo ilikuwa inaanza kuruka kutoka katika mji wa Kirusi wa Igarka, lakini ilishindwa kusogea baada ya hali ya hewa kuwa -52C.

Abiria waliokuwa ndani ya ndege hiyo idadi yao kubwa walikuwa wafanyakazi wa ndege hiyo waliombwa kutoa msaada wa dharura wa kuisukuma ndege hiyo kwa hofu ya kutowachelewesha endapo watasubiri msaada Zaidi.

Ndege hiyo ya shirika la ndege la Katekavia baada ya muda ilimudu kuendelea na safari zake na baadaye kutua salama katika mji wa Krasnoyarsk.

kwa muujibu wa mashuhuda wa tukio hili kiwango cha baridikwa muujibu wa mashuhuda wa tukio hili, wanaeleza kuwa kiwango cha baridi kilishuka hadi kufikia nyuzijoto 52, na kugandisha mfumo wa breki za ndege hiyo.

Mkuu wa kitengo cha huduma za ndege hiyo Oxana Gorbunova, anaeleza kwama abiria hawakulazimishwa kuisukuma ndege hiyo bali kwa hiyari waliamua kusaidia kuisukuma, japokuwa kitendo hicho hakiruhusiwi kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kuathiri bodi ya nje ya ndege hiyo ,na wanasherianao wanachunguza endapo uwanja wa ndege, shirika la ndege, wafanyakazi wa ndege amaabiria endapo wamevunja sheria za usalama wa anga.

Uwanja huo wa ndege unatumiwana abiria takribani elfu moja kwa mwaka ,wengi wao hufanya kazi katika makampuni ya mafuta yanayomilikiwa na Urusi.

MTU MMOJA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI KIFUANI NA KICHWANI

Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la John Salehe (32) Mkazi wa Kijiji cha Itenka Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoani hapa ameuwawa kikatili kwa kupigwa risasi kichwani na kifuani na mtu asiye julikana wakati akiwa anakunywa pombe kwenye baa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la polisi wa Mkoa wa Katavi kamishina msaidizi mwandamizi Dhahiri Kidavashari tukio hilo la mauwaji ya kinyama lilitokea hapo juzi kijijini hapo majira ya saa mbili kamili usiku

Alisema kabla ya tukio hilo marehemu alikuwa amekaa akinywa katika baa moja iliyopo kijijini hapo inayomilikiwa na mkazi mmoja wa kijiji hicho cha Itenka aitwaye Mussa Juma(DEO).

Alieleza marehemu alifika kwenye baa hiyo toka majira ya saa kumi na moja jioni na toka muda huo aliendelea kunywa pombe kwenye baa hiyo huku akiwa na baadhi ya watu ambao nao pia walikuwa wakinywa pombe kwenye baa hiyo ya Mussa Juma ambayo ni maarufu kijijini hapo kwa kuuza pombe za aina ya bia mbalimbali Ndipo muuaji huyo asiye fahamika alifika hapo na kufyatua risasi mbili zilizompiga marehemu kifuani na kichwani na marehemu alifariki hapo hapo.

Kidavashari alieleza kuwa katika tukio hilo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la James Omar(30) Mkazi wa Kijij hicho cha Itenka ambae nae alikuwa kwenye eneo hilo alijeruhiwa kwa kupigwa na risasi moja na bunduki aina ya SMG kwenye maeneo ya kiunoni.

Alisema majirani wa eneo hilo baada ya muda walifika kwenye eneo hilo kwa lengo la kutowa msaada hata hivyo walikuta muhusika aliyafanya tukio hilo alikuwa ameisha tokomea mahari kusikojulikana Chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na wala hakuna mtu wala watu waliokamatwa kuhusiana na mauwaji hayo ya kikatili ya mtu huyo.

Kamanda Kidavashari alisema jeshi la Polisi Mkoani Katavi linaendelea kufanya msako mkali ilikuweza kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika mauwaji hayoili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

WAZIRI MUHONGO AHUSISHWA NA NYARAKA ZA ESCROW

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, ametajwa kuwa na uhusiano wakaribu na mmoja kati ya vijana wawili wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kuiba kutoka Ofisi ya Katibu wa Bunge ripoti ya ukaguzi wa hesabu za zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizochotwa kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Wakati Waziri Muhongo akitajwa kuwa na uhusiano wa karibu na mtuhumiwa huyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye jana ilikuwa ni siku yake ya kwanza kuongoza Bunge tangu lianze Novemba 4, mwaka huu, anadaiwa kutajwa kuwamo katika orodha ya vigogo waliovuna fedha hizo, huku yeye akipata mgawo wa Dola zaMarekani milioni moja.

Aliyemtaja Waziri Muhongo kuwa na uhusiano wa karibu nakijana huyo, ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.

Mnyika alimtaja Waziri Muhongo, wakati akichangia mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, bungeni jana.

Muswada huo uliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni, Ijumaa wiki iliyopita."Mheshimiwa Spika, ni muhimu ofisi yako ifuatilie. Kwa sababu mtuhumiwa yule ana uhusiano wa karibu sana naProf. Sospeter Muhongo, ambaye ni mmoja wa watuhumiwa kwenye kashfa tunazozijadili," alisema Mnyika.

Aliongeza: "Sasa nasema haya mapema ili isifikie hatua tukatumiwa kisingizio cha mambo kuwa mahakamani kushindwa kuwataja kwa majina wahusika. Polisi wafanye uchunguzi, wachukue hatua."

Mnyika alisema uharamia kwenye suala IPTL wa muda mrefu umezidi mipaka.

Alisema taarifa alizonazo ni kwamba, polisi wanamshauri Spika wa Bunge kwa sababu wanataka haraka haraka wamkimbize mtuhumiwa huyo mahakamani ili baada ya hapo alieleze Bunge kuwa kishapelekwa mahakamani, hivyo hakuna sababu ya kutaja jina wala suala lake kujadiliwa.

Mnyika alisema tangu siku waliyowapa polisi taarifa, mpaka leo wamekuwa wakisitasita wakishindwa kutaja jina la mtuhumiwa, huku wakisingizia uchunguzi.

Hata hivyo, alisema upande waserikali wanapokutana nao kwenye korido wamekuwa wakiwaambia kuwa mhusika anafahamika, ikiwa ni pamoja na watu wote ambao amekuwa akiwasiliana nao.

"Mheshimiwa Spika, ukiendelea kuyakinga mambo haya kwa kisingizio cha mambokuwa polisi, halafu baadaye polisi wakaenda mahakamani, ukaja kuyakinga hapa kwa kisingizio cha kwamba mambo yako mahakamani, maana yake Mheshimiwa Spika na wewe utahesabika kwamba, hizo mbinu za hao maharamia waliopora ripoti ndani ya ofisi yako pengine na ofisi yako inahusika," alisema Mnyika.

Alimshauri Spika Makinda kuwasiliana na vyombo vinavyohusika ili ofisi yake na kiti chake visitumiwe na watuhumiwa kuficha uharamia unaoendelea dhidi ya Bunge na uwajibikaji, ambao Bunge linapaswa kuusimamia kwa niaba ya wananchi.

Madai hayo ya Mnyika yalitolewa siku moja baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, kukaririwa akisema kuwa katika mahojiano na polisi, kijana huyo alikiri kwamba, alipewa ripoti hiyo na Mbunge mmoja, ambaye alikataa kutaja jina lake ili kuepusha kuharibu upelelezi.

Vijana hao walikamatwa na polisi Jumamosi wiki iliyopita, mjini hapa, baada ya kukutwa wakiwa na ripoti hiyo yenye mhuri wa Katibu wa Bunge, ambayo wanadaiwa 'kuichakachua' kabla ya kuidurufu na kuisambaza mitaani kama njugu.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, pia alithibitisha kutoa taarifa polisi kuhusu vijana hao kumiliki nyaraka zenye muhuri wa ofisi yake isivyo halali.

Kamanda Misime alisema hadi juzi vijana hao walikuwa wanashikiliwa na polisi.

Chanzo: Nipashe

ZITTO: MAISHA YETU YAPO HATARINI

Siku moja kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha bungeni, ripoti ya uchunguzi wa IPTL kuhusu ufisadi katika akaunti ya Escrow, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe amesema amekuwa akipata vitisho ili kuzuia ripoti hiyo.

Akizungumza jana, Zitto alisema pamoja na vitisho hivyo haogopi kwa kuwa maisha yake ameshayaweka nadhiri siku nyingi.

"Kuna kundi la wahuni kutoka Musoma limeletwa Dodoma likiongozwa na mtu (jina tunalihifadhi) mwenye rekodi ya ujambazi. Hivi sasa anashikiliwa na polisi kwa kukutwa na nyaraka zilizoibwa Ofisi ya Bunge. Usalama wa wajumbe wote wa PAC upo shakani," alisema Zitto.

Aliongeza kuwa kuna vipeperushi vimesambazwa mjini Dodoma kumkashifu lakini havitamsumbua kwa kuwa yeye anataka ukweli ujulikane.

Baadhi ya wabunge jana walionekana na kitabu kilichoandikwa 'mjue Zitto Kabwe kama mtetezi wa wanyonge,' lakini ndani yake kikiwa na mambo ya kumchafua mbunge huyo.

Vitabu hivyo vinaelezwa kusambazwa kwa wabunge katika nyumba zao vikilenga kuonyesha kwamba Zitto hafai kusimamia PAC ambayo hivi sasa inashughulikia escrow.

Wakati Zitto akisema hayo, suala hilo la vitisho jana pia liliibuka bungeni baada ya Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed kueleza kuwa hali ni tete kuhusu usalama wa wabunge kutokana na escrow.

Akiuliza swali la nyongeza, Mohamed alisema usalama wa wabunge uko shakani kuanzia maeneo wanayofanyia kazi na makazi yao na hasa kipindi hiki tangu kuanza kwa sakata la escrow.

"Je, nini tamko la Serikali juu ya ulinzi na usalama wa wabunge katika maeneo ya kazi, pia katika maeneo yao ambayo wanaishi?" alihoji.

Kabla ya majibu kutolewa na Serikali, Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye jana alianza kuongoza vikao baada ya safari yake nje ya nchi, aliingilia kati akisema ofisi yake inakusudia kujenga kijiji cha wabunge ambako watalindwa kwa pamoja.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alisema Serikali inafanya tathmini ya vitisho vyote vya viongozi nchini wakiwamo wabunge ili kuhakikisha wanakuwa salama.

Chanzo: Mwananchi

WAZIRI WA ULINZI AJIUZURU MAREKANI

Waziri wa ulinzi nchini Marekani, Chuck Hagel,amejiuzuru nafasi yake hiyo akiwa ametumia muda wa chini ya miaka miwili kazini.

Rais Barack Obama ameielezea hatua hiyo kuwa ni ya kawaida, nakumsifu Hagel kwa uamuzi aliouchukua lakini pia kwa ushauri alokuwa akimpatia na tabia yake ya ukweli na uwazi kwakipindi chote alichokuwa waziri wa ulinzi.

Lakini wachunguzi wa mambo mjini Washington wanaielezea sababu halisi ya kujiuzuru kwa waziri huyo wa ulinzi ni kushindwa kuingilia misimamo yaraisi Obama juu ya sera ya uhamiaji.

Mwandishi wa BBC mjini humo amemuelezea waziri Hagel ambaye ni M Republican kuwa alichaguliwa kuvirejesha nyumbani vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo vilivyoko Afghanistan na nje ya hapo lakini bajeti yake ikakatwa.

Lakini changamoto hiyo inayolikabili taifa hilo kutokana na kitisho cha kikundi cha dola ya kiislam Is, mgogoro wa Syria na Urusi na uchokozi wa Ukraine inadhaniwa kuwa ni toufauti za kitaaluma na bwana Hagel ametakiwa kusalia madarakani mpaka hapo mrithi wake atakapoteuliwa na baraza la Seneti.

SPIKA MAKINDA AWA MBOGO SAKATA LA ESCROW

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amerejea bungeni kwa kishindo, baada ya jana kukataa pendekezo la kusitisha kazi nyingine za Bunge kujadili taarifa ya kukamatwa kwa baadhi ya watu wanaodaiwa kusambaza ripoti kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow ya IPTL.

Aidha, amesema wabunge watamuonesha ni kwa jinsi gani amehongwa Sh bilioni 1.6 (Dola za Marekani milioni moja) katika sakata hilo.

Akiongoza Bunge kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 16 na 17 baada ya kuwa safarini kwa muda mrefu, Makinda pia ameahidi kuwa wabunge watapewa ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu sakata la fedha za IPTL.

Alitoa maelekezo hayo baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kuomba kupitia Kanuni za Bunge, shughuli za Bunge zilizopangwa zisiendelee badala yake wabunge wajadili kusambazwa kwa nyaraka za CAG zinazodaiwa kuibwa ofisini kwa Spika.

Mbatia alisema kumekuwapo na taarifa za mtu kudurufu ripoti hiyona kuisambaza kwa wabunge na watu mbalimbali, jambo ambalo nikinyume cha Kanuni.

Hivyo, kwa kutumia Kanuni za Bunge, alitaka Spika asitishe shughuli nyingine na jambo hilo lijadiliwe.

"Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali, sasa hili linashusha hadhi ya Bunge isifanye kazi yake vizuri, kwa hiyo napendekeza tulijadili hapa. Naomba mambo mengine yasitishwe, tulijadili," alisema Mbatia.

Lakini Makinda licha ya kumpongeza Mbatia kwa kulieleza hilo, alithibitisha kuwa Polisi wanamshikilia mtu mmoja kuhusu suala hilo, lakini akawahoji wabunge kwamba sasa wanataka kujadili nini."Sasa mnataka tujadili nini? Hatuendeshi Bunge bila taratibu. Mmeandika ninyi hizo nyaraka? Ofisi yangu imedhalilishwa. Lakini hili tayari liko Polisi, linashughulikiwa na wenzetu hawa.

"Watamhoji huyo mtu alipata wapi nyaraka hizo na kuna mahali walipochapia Dar es Salaam wataenda ku-confiscated (kutaifisha). Kwa hiyo, hapa hakunala kujadili, labda wangekuwa wamemaliza kazi yao ya uchunguzi," alisema Makinda huku baadhi ya wabunge wakiendelea kumbana.

Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF), alipopewa fursa ya kuzungumza , alidai kuwa suala hilo ni vyema likajadiliwa kwani kuna nyaraka zaidi zinawekwa katika makazi ya wabunge na usalama wao uko hatarini.

Mnyaa alikwenda mbali zaidi na kumweleza Spika kuwa "ipo minong'ono pia inakuhusisha nawe Spika kwamba umehongwa Dola za Marekani milioni moja. Sasa ni bora tukajadili suala hilo," alisema Mnyaa.

Ni kama alikuwa amemtonesha zaidi Spika Makinda, kwani alikuja juu na kusema: "Mtanionesha, mtanionesha, mtanionesha hizo hela. Hatuwezi kufanya mambo ya kitoto."

Akimjibu Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, Makinda alisema ni vyema wote wenye nyaraka hizo wakazirudishe Polisi.

Akijibu ombi la Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) la kutaka ripoti hiyoya CAG na vielelezo vyake kupewa wabunge mapema ili kujiandaa na mjadala, Spika alisema utaratibu unaandaliwa.

Akichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014,Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema mtu aliyekamatwa akisambaza nyaraka hizo ana uhusiano wa karibu na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Alisema kuwa polisi wanataka kumpeleka mtuhumiwa huyo mahakamani ili baadaye Bunge lizuiwe kujadili suala lake kwa kuwa litakuwa limefikishwa katika mhimili huo mwingine wa Dola, hivyo kikanuni watazuiwa kulizungumzia bungeni.

Ripoti ya CAG ilikabidhiwa bungenina Serikali, Novemba 14, mwaka huu na kisha Bunge iliikabidhi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) siku tatu baadaye, kwa ajili ya uchambuzi namaoni kabla ya kuwasilishwa ndani ya Bunge.

Kamati hiyo ya PAC inaendelea na vikao vyake na kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, mjadala wa ripoti hiyo utaanza kesho na unatarajiwa kuendelea kabla ya Bunge kuahirishwa Ijumaa wiki hii.

Akaunti hiyo ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kibiashara wa Tanesco na IPTL, kampuni inayofua umeme yenye mitambo yake Tegeta, Dar es Salaam.

Jumatano wiki iliyopita kuliibuka mabishano makali bungeni kwa wabunge kuonesha hisia kuwa ipo barua kutoka kwa mhimili mwingine wa Dola, Mahakama ikilizuia Bunge kujadili suala hilo lililozua gumzo nchini.

Sakata la Tegeta Escrow linahusu kuchukuliwa kwa Dola za Marekani milioni 200 katika akaunti hiyo, baada ya kutolewa kwa uamuzi katika Mahakama Kuu.

Zitto achafuliwa Aidha, joto la ripoti ya CAG iliyokabidhiwa kwa PAC, imemuibulia balaa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe baada ya vitabu kadhaa vya kumchafua kusambazwa ndani na nje ya viwanja vya Bunge.

Kitabu hicho chenye kichwa cha habari; "Mjue Mbunge Zitto Kabwe Mtetezi wa Wanyonge Tanzania", maudhui yake ni tofauti na kilichomo ndani, kwani Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini ameshambuliwa.

Maandishi yaliyomo ndani ya kitabu hicho yanahoji juu ya uadilifu wake kuanzia maisha binafsi hadi kazi za ubunge anazozifanya na jinsi anavyojinufaisha kupitia kamati anayoiongoza na umaarufu wake pia.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema amewataka wabunge kuacha kuchafuana juu ya sakata la Escrow,akisema Bunge na PAC wanafanya kazi kiuchunguzi.

Alisema, kuna watakaosema wamehukumiwa bila kusikilizwa, hivyo ni vyema kuacha kuchafuana kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamelisaidia Bunge na Taifa.

Akijizungumzia yeye mwenyewe, alisema: "Nitasimama mwenyewe kujitetea, lakini nawaomba, tafadhalini msichafuane. Acheni kutoa makaratasi na vitabu. Kesi hii inaendeshwa kiuchunguzi. Tuache kuchafuana."

Aidha, katika hilo, alisisitiza kuifuata Katiba ya nchi akisema ndio mwongozo unaokubalika.

Chanzo: Habari leo

MFANYAKAZI ALIYETESA MTOTO KUSHTAKIWA KWA JARIBIO LA MAUAJI

Polisi wamebadilisha mashtaka ya mfanyikazi wa nyumbani aliyenaswa kwa kamera akimpiga na kumtendea unyama mtoto wa mwaka mmoja na nusu, kutoka kwa kosa la kutesa na sasa anakabiliwa na kosa la jaribio la mauaji.

Video hiyo iliwaudhi watu wengi sana kwenye mitandao ya kijamii ila babake mtoto huyo alisema walisambaza video hiyo ili kuwatahadharisha wazazi wenegine.

Mfanyakazi huyo wa nyumbani Jolly Tumuhirwe, alikuwa amezuiliwa katika gereza la Luzira na mahakama ya Nakawa kwa kosa la kutesa chini ya kifungo cha 41 kwenye katiba kinachoongelea dhidi ya mateso.

Mwanamke huyo sasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani tarehe 8 Disemba.

Hata hivyo, msemaji wa polisi Bwana Fred Enanga, amesema"shtaka dhidi ya mwanamke huyo lilibadilishwa baada ya kupitiwa mwendesha mkuu wa mashitaka.

Tumuhirwe alikubali kosa la kumpiga mtoto huyo kwa kurunzi, tuki olililonaswa kwa kamara ya CCTV. Polisi walimfanyia Tumuhirwe uchunguzi wa kiakili na kubaini kuwa ana akili timamu.

Afisaa mkuu wa polisi Fred Enaga, amewaonya waajiri kuchunguza mbinu zinazotumika kuwachagua wasichana wa kazi, kwa sababu matendo kama haya yanaweza kutokana na matatizo ya kisaikologia.

Waziri wa Jinsia, Kazi na maendeleo ya jamii Bi Mary Karooro Okurut alipongeza juhudi za wazazi wa mtoto huyo Arnella "kutokana na kitendo hicho kwa mtoto. Ingekuwa mtu mwingine angemuua mischana huyo wa kazi lakini alifuata sheria. Pia tunapeleka marekebisho katika katiba kuhusu maslai ya watoto bungenikuimarisha sheria zinazowajali watoto," alisema waziri huyo.

Polisi wamesema kuwa nia ya shambulio hilo haijatambulika napia msichana huyo amefanyia kazi familia hiyo kwa siku 26 pekee. Wazazi wamesema kuwa mtoto huyo ametolewa hosipitalini na hali yake ya afya inaimarika.

Kulingana na msemaji wa polisi Fred Enaga, kesi hiyo iliripotiwa na Baba ya mtoto Erick Kamanzi mnamo tarehe 13 Novemba katika kituo cha polisi cha Kiwatule baada ya kuona video hio.

Kesi hiyo ilipelekwa kwa kitengo cha polisi cha Kiira. Baada ya uchunguzi, msichana huyo wa kazi alihukumiwa na shataka la mateso katika mahakama ya Nakawa na kuzuuliwa katika gereza la Luzira.

Bwana Enaga alisema Bi Tumuhirwe alishtakiwa chini ya kifungo cha tatu kwenye katika kinacholinda maslahi ya watoto. Kifungo hicho kinajumuisha mashataka kama ya kutesa inayopeana uwezekano wa kumfunga mtu hadi miaka 15 gerezani.

Hata hivyo, Bwana Enaga anashauriana na mkurugegenzi wa pande za mashtaka kurebisha hukumu hilo kuwa kifungu cha maisha.

UGAIDI WAINGIA MICHEZONI

Mtu mmoja aliyekuwa amejifungasha kwa mabomu amejitoa muhanga kwa kushambualia mechi ya Volleyball mashariki mwa Afghanstan,na kuua watu wapatao arobaini na watano.

Msemaji wa Gavana wa jimbo la Paktika amesema watu wengine hamsini walijeruhiwa vibaya baada ya mtu huyo kujiripua katikati ya mashabiki wa mchezo huo.

Inasadikiwa kuwa watu wapatao mia moja walijitokeza kushuhudia mechi hiyo ya fainali ya kuwania kuingia katika michuano ya maji nchini humo.

Mpaka sasa hakuna kundi lolote lililokubali kuhusika na shambulio hilo ingawa kuna shaka kwamba huenda kikundi cha kutoka nchini Taliban.

Naye raisi wa Afghanstan Ashraf Ghani ameelezea shambulio hilo kuwa si la kiutu wala si la kislam.

KENYA YAWACHAKAZA AL SHABAAB 100 WAUAWA

Makamo wa rais wa Kenya, William Ruto, anasema kuwa askari wa usalama wa Kenya wamewaandama wapiganaji wa al-Shabaab hadi kwenye kambi yao nchini Somalia, baada ya shambulio dhidi ya basi kaskazini-mashariki mwa Kenya hapo jana ambapo raia 28 waliuliwa.

Bwana Ruto alisema wapiganaji zaidi ya 100 waliuliwa katika operesheni mbili tofauti.

Alisema kambi ya al-Shabaab iliangamizwa.Habari hizo hazikuthibitishwa na upande wa pili.

Gavana wa Mandera - ambako shambulio la jana lilitokea - amelaumu vikosi vya usalama kwa kushindwa kuwalinda raia.

Alisema polisi kawaida wanashindwa kufanya uchunguzi kamili baada ya mashambulio.

KAULI NA MSIMAMO YA MWIGULU NCHEMBA NDANI YA KIKAO CHA KAMATI YA UONGOZI YA CCM KUHUSU WIZI WA ESCRO

KAULI NA MSIMAMO YA MWIGULU NCHEMBA NDANI YA KIKAO CHA KAMATI YA UONGOZI YA CCM KUHUSU WIZI WA ESCROW

"CAG ameshasema pesa zile zilikuwa mali ya umma, sasa zikamatwe zote na wahusika wote wakamatwe,"

"Nimemwagiza Kamishna wa Kodi amfukuze kazi yule mtumishi wa TRA iliyoko chini ya wizara yangu anayetajwa kuchota Bilion 1.6 na afilisiwe, pia mitambo na kodi vikamatwe na wahusika wakamatwe.

"Hatuwezi kuendeleza mazoea ya kufunga maskini na kuwapa likizo wezi wakatumie fedha. Walio serikalini na walioko kwenye siasa wakamatwe na tuwafilisi fedha irudi serikalini,"

"Tazama wanafunzi, watoto wa maskini zaidi ya elfu 40 wamekosa mikopo, madawa hospitalini hakuna, maskini wanakufa, watu wasio na hatia wanafungwa kwa kukosa michango ya maabara, walimu wanadai fedha zao, wazabuni wanauziwa nyumba zao na benki huku wakiidai Serikali kwa huduma walizotoa, leo wezi tuwape adhabu ya kujiuzulu? Tuwape likizo ya kwenda kutumia fedha walizo waibia maskini?"

THIERY HENRY KUPEWA KIBARUA ARSENAL

Arsenal ina mpango wa kumpatia aliyekuwa mshambulizi wa timu hiyo Thiery Henry fursa ya ukufunzi katika timu hiyo kulingana na gazeti la daily mail.

Kandarasi ya raia huyo wa Ufaransa katika kilabu ya New York Red Bulls inatarajiwa kuisha mwisho wa msimu wa ligi ya sokaya marekani MLS mwezi ujao na hajasema ni hatua gani anayotarajia kuchukua.

Wengi wanaamini kwamba kampeni hiyo itakamilisha harakati zake kama mchezaji na huenda Arsene Wenger akamchukua katika kilabu hiyo.Na alipoulizwa iwapo Henry anaweza kurudi katika kilabu hiyo kama kocha ,Wenger alijibu kwamba hakuna lisilowezekana.

''Mimi huwakaribisha watu ambao wameichezea timu hii''.

''Hata hivyo ni lazima ajifunze kazi hii mwanzo'',.

Nimewaona wengi ambao wana uwezo lakini wameshindwa katikafursa yao ya kwanza kwa kuwa hawakuwa tayari.

KIFO CHA MTOTO CHAZUA GABHABU KAMPALA

Shughuli za mazishi ya mtoto wa miaka miwili zimefanyika nchini Uganda, mtoto ambaye kifo chake kimezua ghadhabu baada ya mtoto huyo kugongwa na gari la halmashauri ya jiji la Kampala,baada ya mama yake kukamatwa akiuza matunda kinyume cha sheria.

Familia ya Ryan Ssemaganda na wanasiasa wa upinzani walitishia kutomzika mtoto huyo mpaka maofisa hao watakapo wajibika kwa kitendo hicho.

Mwili wake ulichukuliwa wakati wakiandamana kuelekea bungeni siku ya alhamisi.

Raia wa Uganda wanaona kuwa halmashauri hiyo inatumia nguvu nyingi kupambana na wachuuzi wa mitaani.

Mama wa mtoto Ryan alikamatwa siku ya jumatatu baada ya kukutwa akiuza matunda huku akiwa hana leseni.

Siku iliyofuata, Bibi wa mtoto huyo alimpeleka katika Ofisi za Mamlaka ya mji wa Kampala ambako mama mtoto alikuwa akishiliwa , nia ilikua kumpa mama mtoto ili amnyonyeshe.

Maafisa wa Ofisi hiyo walikataa na wakati wakijadiliana kuhusu hilo, mtoto alichoropoka kutoka kwa mama yake na kugongwa na gari linalomilikiwa na Mamlaka hiyo.

Siku ya Alhamisi polisi ilizuia kupelekwa kwa mwili katika Bunge, wakisisitiza mwili huo uzikwe ili marehemu apumzike kwa amani, na kuwataka waepukajambo hilo kushughulikiwa kisiasa.

SAKATA LA TEGETA ESCROW LATIKISA BUNGE

Wabunge Bila ya kujali itikadi za vyama vyao wamelitaka Bunge kuachana na Barua ya mahakama inayotaka kuzuia sakata la Kashfa ya fedha katika akaunti ya Tegeta ESCROW lisijadiliwe na kutolewa maamuzi Bungeni kwa kuwa liko Mahakamani.

Wakitoa ushauri kwa Bunge na kamati ya uongozi, Mbunge wa kigoma kusini Mhe.Davidi Kafulila amesema mahakama imekosa uhalali mamlaka ya kisheria na kikanuni ya kuzuia Bunge kuendelea na utaratibu wake katika kufuatilia sakata la ESCROW.

Baadhi ya wabunge kutoka chama tawala CCM wamelitaka Bunge kuchukua hatua kataka hilo kwa kuhakikisha taarifa ya kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali kuhusu wizi huo wa mabilioni ya fedha iwasilishwe bungeni.

Kwa upande wao wabunge wa chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA wametaka Barua hiyo kuwekwa mezani ili kuliwezesha Bunge kumjadili kiongozi wa mahakama kama hoja mahususi kwa mujibu wa kanuni ya 64 1e ambaye amediriki kuingilia mamlaka ya Bunge na kulifundisha kazi zake.

Akielezea kwa ufupi hatua ya kamati ya PAC inayochunguza sakata la ESCRO ilipofikia mwenyekiti wa kamati ya PAC amependekeza kuwepo kwa mjadala ili kuweza kuondoa Minong'ono pamoja na kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa sheria.

Aidha akizungumzia sakata hilo,waziri mkuu mheshimiwa mizengo pinda amependekeza katika kutatua sakata hilo ni lazima Bunge litumie Busara kubwa ili kuahikikisha maamuzi yatakayotolewa hayataleta hisisa za muingiliano wa majuku na mahakama.

KIKAO CHA BUNGE CHASAMBARATISHWA KWA MABOMU YA MACHOZI

Polisi katika mji mkuu wa Lagos, Nigeria, wamefyatua gesi ya kutoa machozi ndani ya jengo la bunge, na kulazimisha kuahirishwa kwa mjadala muhimu wa bunge hilo kuhusu kurefushwa kwa kipindi cha hali ya tahadhari kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwaandishi wa BBC amesema kuwa maafisa wa Polisi walikuwa wakijaribu kumzuia spika wa Bunge la waakilishi Aminu Tambuwal, ambaye alihamia chama cha upinzani mwezi uliopita kuendelea na mjadala huo.

Wabunge wa upinzani wanasema kuwa hali ya tahadhari imeshindwa kuhimili visa vya wapiganaji wa kiislam wa Boko Haram.

Mwaandishi wa BBC aidha anaongeza kuwa afisa mkuu wa polisi ametakiwa kufika mbele yabaraza la Senate kuelezea hatua hiyo ya maofisa wa polisi kurusha vitoa machozi ndani ya Bunge.

Bunge limefungwa hadi juma lijalo.

KOREA KASKAZINI KUFANYA JARIBIO LA NUKLIA

Korea Kaskazini imetishia kufanya majaribio ya zana zake za nuklia katika jibu lake kwa vitisho vya umoja wa Mataifa kuchunguza visa vya ukiukwaji wahaki za binadamu nchini humo.

Taarifa kutoka kwa wizara yake yamambo ya nje ilishutumu Marekani kwa kuchochea umoja wa Matifa kuchunguza visa vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo hivi majuzi.

Korea Kaskazini iliwahi kufanya majaribio ya zana zake za nuklia mwaka 2006,2009 na 2013.

Vitisho vya nchi hiyo vinakuja huku picha za satelite zikionyesha kuwepo shughuli nyingi tu katika kiwanda cha nuklia nchini humo.

Kamati ya umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, ilipitisha azimio lililokuwa linatoa wito kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kusihitaki Korea Kaskazini kwa mahakama ta kimatifa ya ICC kwa tuhuma za kukiuka haki za binadamu.

Pyongyang ilisema kuwa azimio hilo, lilitokana na ushahidi wa uongo na porojo dhidi ya serikali.

''Azimio hilo lililoshinikizwa na Marekani,lilikuwa hatua ya kuingilia uhuru wa taifa hili na inatuwacha bila budi la kufanya jaribio la nuklia kwa mara nyingine,'' ilisema taarifa ya serikali.

Taarifa hio iliongeza kusema jeshi litakuwa tayari kwa chochote dhidi yake na sanasana ikiwa kutakuwa na shambulizi dhidi ya nchi hiyo kutoka kwa Marekani.

MKENYA AFANYA MAUAJI BAR TARIME

MTUHUMIWA wa vitendo vya ujambazi kutoka Kijiji cha Masangura, Wilaya ya Kurya West nchi jirani ya Kenya, Chacha MarwaGibai maarufu kama Mapengo anashikiliwa na polisi katika Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya akituhumiwa kuua mtu kwa kumchoma kisu na kujeruhi mwingine kwa kisu katika vurugu aliyoianzisha baa mjini hapa.

Kukamatwa kwa Mapengo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa aliyesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumchoma kisu kifuani na tumboni mkazi wa mjini Tarime, Isack Mwita Matutu (20) nakumsababishia kifo kabla ya kumshambulia mfanyabiashara Deus Tenten pia wa hapa aliyejeruhiwa shingoni.

Kamanda Mambosasa, akielezea mkasa huo, alisema: "Tukio hilo la mauaji ya kijana Isack Mwita Matutu yalitokea saa 4 usiku wa kuamkia Jumatano (jana) katika Baaya Criss Pub ambapo kulitokea ugomvi kati ya mtuhumiwa na marehemu alikuwa akinywa na wenzake katika baa hiyo ambapo mtuhumiwa alichomoa kisu na kumchoma Isack kifuani na tumboni na kufariki muda mfupi kabla hajafikishwa katika Hospitali ya Wilaya kwa matibabu.

"Lakini pia akamjeruhi mfanyabiashara Deus Tenten shingoni ambapo majeruhi alikimbizwa hospitali haraka na kutibiwa na hali yake haijaimarika. Tunamshikilia Chacha Mapengo kwa mahojiano zaidi. Naye anatibiwa kwa sababu alishambuliwa na wananchi kabla ya kuokolewa na askari wetu waliowahi eneo la tukio."

Alisema mtuhumiwa huyo anahusishwa kutishia watu maisha, na kwamba tayari ana kesi katika Mahakama ya Wilaya Tarime ya kumtishia maisha Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mkoa wa Mara Ben Usaje.

Pia ana kesi ya kumchoma kisu tumboni mkazi wa Sirari, wilayani hapa aitwaye Soko Waisaki na kumsababishia ulemavu.

ASKARI POLISI AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA JIJINI MBEYA

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa polisi wa upelelezi, Maduhu, F5842, aliyekuwa akikabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Daniel Mwakyusa.

Aidha, mahakama hiyo imewaachia huru washitakiwa wengine wawili wa kesi hiyo, polisi wa upelelezi, Shaaban, F 7769, na polisi wa kike mpelelezi, Neema, F 6545, baada ya kuwakuta hawana hatia.

Hukumu hiyo ya kesi namba 16 ya mwaka 2013, ilitolewa jana mjini hapa na Jaji Rose Temba, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewana pande zote mbili.

Awali, ilielezwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali, Archiles Mulisa akisaidiwa na Catherine Paul kuwa washitakiwa walifanya mauaji ya kukusudia Februari 14 mwaka 2012 kinyume cha Kifungu Namba 196 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa Marejeo mwaka 2002.

Mulisa alidai washitakiwa hao kwa pamoja walihusika na mauaji ya Daniel Mwakyusa baada ya kumpiga kwa kutumia silaha inayodhaniwa kuwa ni bunduki, njeya ukumbi wa starehe wa Universal uliopo Uyole jijini Mbeya.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Temba alisema anawaachia huru mshitakiwa namba mbili, Shaaban ambaye alikuwa dereva wa gari ya polisi kwa kuwa ushahidi uliotolewa, unadhihirisha kuwa alibaki ndani ya gari akimsubiri mshitakiwa namba moja aliyeshuka na kuingia kwenye ukumbi wa Universal.

Kwa upande wa mshitakiwa namba tatu, Neema, Jaji Temba alisema aliridhishwa na mshitakiwa huyo kutohusika na mauaji kwa kuwa siku ya tukio alikuwa akijisikia vibaya, hivyo alilazimika kubaki na dereva kwenye gari.

Jaji Temba alisema mshitakiwa namba moja, Maduhu, anahusika moja kwa moja na mauaji hayo, kutokana na ushahidi wa kimazingira, kwani yeye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuondoka na Daniel Mwakyusa eneo la tukio na kumpeleka kwenye gari.

Alisema sababu ya pili, ushahidi ulionesha kuwa silaha yake pekee ndiyo iliyotumika, tofauti na za askari wengine kwa kuwa risasi tatu zilionekana kupungua kati ya zile alizokabidhiwa sambamba na ushahidi wa maganda matatu ya risasi, yaliyookotwa eneo la tukio.

Jaji Temba alisema sababu ya tatu ni kuwa ushahidi uliotolewa, unaonesha kuwa mshitakiwa huyo alikuwa wa mwisho kurejesha silaha, hivyo kuhusishwa moja kwa moja na mauaji hayo.

Alisema kutokana na sababu hizo, mahakama inamtia hatiani kwa kuua kwa kukusudia, hivyo mshitakiwa Maduhu, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Awali, ilidaiwa kuwa siku ya tukio ilikuwa Siku ya Wapendanao (Valentine's Day), ambapo mtuhumiwa akiwa doria na askari wenzie, alimkuta Daniel Mwakyusa akiwa kwenye eneo la starehe na mwanamke anayesadikiwa kuwa alikuwa pia na mahusiano na askari huyo.

Chanzo: Habari leo

WANAFUNZI ST. JOHN'S WAGOMA

WANACHUO wa Chuo Kikuu cha St. John's mjini hapa jana wamegoma kuingia madarasani, kushinikiza uongozi wa chuo hicho kutatua matatizo yao, ikiwemo madai ya chuo kuwa na sheria kandamizi.

Mgomo huo ulianza asubuhi, ambapo wanafunzi walikusanyika katika uwanja wa mpira uliopo chuoni hapo huku Rais wa Wanafunzi, Damel Daniela akisisitiza wamegoma kutokana na mambo ya msingi.

Kaimu Mkuu wa Chuo, Profesa Casmir Rubagumya alisema atatoa taarifa kamili baada ya kumaliza kikao kati ya uongozi wa chuo na viongozi wa wanafunzi.

"Taarifa maalumu itatolewa mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo, kwa sasa sina cha kuongea mpaka tusikilize madai ya wanachuo," alisema.

Miongoni mwa mambo ambayo wanachuo wanadai yamechangia kugoma, ni chuo kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha ikiwemo maabara kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Wanadai walimu wengi kutokuwa na sifa za kufundisha elimu ya juu, isipokuwa wanabebana kiundugu. Wanadai pia kukomolewa katika alama za ufaulu, kwani mwanafunzi anayetakiwa kurudia mtihani awe na alama zaidi ya 50 na hata akipata alama 49 atatakiwa kurudi nyumbani tofauti na vyuo vingine.

Inadaiwa walimu wanaofundisha kwa mkataba maalumu, wamekuwa wakikatwa asilimia 30 ya malipo yao, hivyo kuchangia wengi kukimbia na chuo kukabiliwana uhaba wa walimu.

Rais huyo wa wanafunzi alisema Chuo kimekuwa na sheria kandamizi, kwani ukipata alama za kurudia masomo matatu unarudi nyumbani, jambo ambalo limekuwa likiwaumiza wanafunzi wengi.

Pia, baadhi ya wanachuo wa shahada ya ualimu wa sayansi, walilalamika kuwa kozi yao haijasajiliwa na kwamba hawafahamu hatma yao licha ya kutoa ada.

Chanzo:Habari Leo

MABEHEWA 50 KATI 274 YA MIZIGO YAWASILI

Mabehewa Hamsini kati ya 274 ya kusafirishia mizigo katika Reli ya Kati yamewasili nchini kutoka India na mabehewa 22 ya abiria yana tarajiwa kuwasili Desemba mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dakta SHABANI MWINJAKA amesema kuwasili kwa mabehewa hayo kutaokoa kwa kiasi kikubwa miundombinu ya barabara ambayo huharibika muda mfupi baada ya kutengenezwa kutokana na malori ya mizigo kwani kwa sasa mizigo yote itasafirishwa kwa njia ya reli.

Amesema Kampuni ya Reli Tanzania imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 45 kwa ajili ya kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kununua vichwa na mabehewa mapya.

Amesema hadi mwaka 2015 injini 45 zitakuwa z imekamilika amba zo z itawezesha kusafirisha tani milioni 1.5 na kuongeza kuwa u jenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es salaam kwenda Kigoma, Tabora hadi Mwanza na Uvinza Msongati hadi B urundi utafanyika.

Mkurugenzi M tendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania Mhandisi KIPALLO KISAMFU amesema injini nne zilizokuwa zikitengenezwa mkoani Morogoro zimekamilika na nyingine 15 zinatengenezwa Afrika ya Kusini ambazo zitagharimu shilingi bilioni 70.

MBOGO AJERUHI WANNE

Watu wanne kutoka kijiji cha Namabengo Wilaya ya Namtumbo Wamejeruhiwa na Nyati na kusababishiwa kulazwa katika kituo cha Afya Namabengo Mkoani Ruvuma.

Kamanda wa Police Mkoa wa Ruvuma Mihayo Msekhela amesema watu walio jeruhiwa walikuwa katika shuguli za kawaida za kila wakipalilia makaburi,wengine kuloweka mihogo bila kujua ndipo walipovyamiwa na Nyati.

Kamanda wa Police Mihayo Msekhela amesema Jeshi la Police lilipo pata Tarifa Hiyo lilichukua Hatua Mara Moja na kushirikiana na Askari wa wanyama Pori kumsaka Nyati huyo hatimaye kuweza kumuua.

FAMILIA YA BOB MARLEY KUANZA KUUZA BIDHAA ZA BANGI

Familia ya aliyekuwa mwanamuziki wa Jamaica, Bob Marley imezindua kampuni ambayo wanaitaja kama ya kwanza duniani kuuza bidhaa za Canbbisa au marujuana au Bangi kama wanavyoijua wengi.

Bidhaa hizo zitajulikama kama 'Marley Natural' na na zitajumuisha mafuta ya urembo pamoja na manukato mengine yawanawake na bidhaa nyinginezo.

Bidhaa hizo zitatengezwa na kampuni kubwa ijulikanano Privateer Holdings iliyo mjini Washington Marekani, ikisisitiza kutaka kudumisha kumbukumbu ya mwanamuziki huyo aliyesifika kote duniani.

Bidhaa hizo zitauzwa nchini Marekani na kwingineko duniani kuanzia mwaka ujao.

Mwanawe Bob Marley, Cedella Marley, alisema hayati babake angekuwa hai angefurahishwa sana na wazo hilo.

''Babangu angekuwa na fahari kubwa kuona watu wakitambua uwezo wa kuponya wa Bangi,'' alisema Cedella.

Mkuu wa kampuni hiyo, Brendan Kennedy alisema Marley alikuwa mtu ambaye kwa njia nyingi alisaidia kuanzisha harakati za kupinga juhudi za kuharamisha Bangi miaka 50 iliyopita.

"Marley alipenda sana kutumia Bangi na hakuna aliyemshinda kwa hilo duniani kote.'' Bob Marley alifariki mwezi Mei mwaka 1981, kutokana na Saratani.

Alipenda sana kutumia Bangi kama sehemu ya imani yake ya Rastafarian na kuunga mkono kuhalalishwa kwake.

Matumizi ya Bangi kwa ajili ya kujiburudisha yamehalalishwa katika majimbo ya Colorado na Washington nchini Marekani.

Majimbo mengine huenda yakaidhinisha matumizi ya Bangi nchini Marekani na mengine tayari yanaruhusu utumiaji wa bidhaa hiyo kwa sababu za matibabu.

KESI YA SITTI MTEMVU YANUKIA

Kesi ya sakata la kudanganya umri ambalo linamkabili aliyekuwa miss Tanzania mwaka 2014 Sitti Mtemvu linakaribia kufunguliwa baada ya uchunguzi unaofanywa na RITA kuelekea ukingoni.

Habari toka RITA zimeeleza kuwa taasisi hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taarifa za uchunguzi kwa kuangalia wote waliohusika kudanganya umri na kumpatia Sitti cheti kipya kilichotolewa septemba 9, mwaka huu ambacho kinaonesha amezaliwa mei 31,1991.

MWANAMKE AFANYIWA UKATILI ARUMERU

Mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Olkokola Wilayani Arumeru Mkoani Arusha amefanyiwa ukatili wa kutisha kwa kukatwakatwa na Panga kichwani na kuondolewa kiganja cha Mkono, sikio na sehemu nyingine za mwili wakeMwanamke huyo anayefahamika kwa jina la Paulina Joseph amefanyiwa ukatili huo na mtu anayedaiwa kuwa ni shemeji yake kwa madai ya kuingilia ndoa yake.

Tukio hilo lilimkuta bi Paulina akiwashambani kwake akikata nyasi kwa ajili ya kulisha mifugo.

Mume wa Paulina ameeleza masikitiko yake kwa uongozi wa kijiji,Kitongoji na kata kwa kushindwa kumkamata mtuhumiwa na kutoroka kwani kitendo hicho kinaweza kusababisha kuendelea kwa vitendo vya ukatii dhidi ta wanawake nchini.

Viongozi wa kijiji hicho wamekanusha kuwa hakuna uzembe uliofanyika kumkamata mtuhumiwa huyo kwani bado inaendelea kumtafuta na kumtia hatiani.

Bi Paulina anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospital Teule ya Seriani wilayani Arumeru alipolazwa na hali yake bado sio nzuri.

BIKIRA, KIPIMO CHA ASKARI

Serikali ya Indonesia inaelezwa kuruhusu kuwafanyia wanawake wanaotaka kujiunga na Jeshi la Polisi kipimo cha bikira ,shirika la Human rights Watch limeeleza.

Shirika hilo uangalizi wa haki za binaadam liliwahoji Polisi wanawake na wanaotaka kujiungana Jeshi la polisi ambao tayari wamepimwa katika miji sita ya nchini Indonesia,wawili kati yao wamefanyiwa kipimo hicho mwaka huu.

Kipimo cha bikira kimeorodheshwa kuwa moja ya matakwa ya kuingia kwenye Jeshi,tovuti ya polisi imeeleza.

Wanawake waliofanyiwa kipimo hicho wamesema walipata maumivu na kujisikia kudhalilishwa.

Askari wa kike walishapeleka malalamiko kwa ngazi za juu za jeshi la Polisi bila mafanikio.

Afisa wa juu wa Human Rights Watch,Nisha Varia amesema kipimo hicho ni unyanyasaji na kinawadhalilisha wanawake, amewataka polisi mjini Jakarta kufuta kipimo hicho na kukipiga marufuku nchi nzima.

Polisi nao wanasema kuwa hawafanyi kipimo hicho kwa sasa kwa kuwa wamepiga marufuku.

Hata hivyo hakuna ushahidi wa kutosha kuwa Jeshi la Polisi limesitisha kitendo hicho kwa kuwa katika tovuti yake eneo la kazi tangazo la tarehe 5 mwezi Novemba mwaka 2014 imeeleza kuwa wanawake wanaotaka kuwa polisi wanapaswa kujaribiwa kama wana bikira,hivyo basi wanawake wanaotaka kuwa askari wanapaswa kutunza bikira zao.

Wanawake walioolewa hawapewi nafasi hiyo.

Mashuhuda wanasema kuwa jaribio la bikira hufanywa katika hospitali zinazoendeshwa na jeshila Polisi, vidole hutumika katika kubaini kama mwanamke ni bikira au la.

Shirika la Human Rights Watch limesema kipimo hiki hufanywa na Polisi pia nchini Misri, India na Afghanistan.

Mwaka 2010 Brigedia Jenerali, Sigit Sudarmanto alieleza namna alivyotofautiana na wenzake kuhusu kipimo cha bikira kwa wanawake yeye haungi mkono.Kisa cha kufanywa kwa kipimo hiki dhidi ya wanawake ni madai kuwa hawahitaji wanawake wasio bikira wakiwafananisha na makahaba.

Lakini swali linabaki kuwa je kunaushahidi wa kisayansi kuwa aliye bikira hufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko asiye bikira, je asiye na bikira hana adabu kuliko aliye nayo?Sudarmanto amesema baada ya kulumbana kwa muda mrefu iliridhiwa kusitishwa kwa zoezi hilo, hata hivyo inashangaza kuona bado hali ni ileile japo ahadi ya kusitishwa ilitolewa.

SHAHIDI MKUU KESI YA MAUAJI YA KIMBARI RWANDA ATOWEKA

Shahidi mmoja muhimu wa uchunguzi unaofanyika kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda ambaye alikuwa akitarajiwa kuhojiwa na majaji Nchini Ufaransa kuhusu kudunguliwa kwa ndege ya aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana, anasemekana kutekwa nyara na kutoweka jijini Nairobi.

Idara ya Polisi Nchini Kenya imekanusha kumtia mbaroni Emile Gafirita.

Majirani wa Emile Gafirita wanasema kuwa walisikia milio ya breki za gari na kamsa pale alipokuwa akirejea nyumbani muda mfupi kabla ya usiku wa manane Jumatatu usiku na kuwaona watu wawili wakimtia pingu na kumrusha kwenye gari.

Idara ya Polisi Nchini Kenya inasema kuwa hawajamtia mbaroni.

Jina la bwana Gafirita liliibuka katika kesi ya hivi majuzi Nchini Rwada, pale alipotajwa kama askari wa zamani katika kikosi chaulinzi cha Rais Paul Kagame.

Majaji wawili wa Ufaransa, Marc Trevidic na Nathalie Poux, walikuwa wakipanga kumhoji ili atoe ushahidi mjini Paris kuhusiana na mzinga ulioshambulia na hatimaye kuiangusha ndege iliyombeba Rais wa zamani wa Rwanda hayati Juvenal Habyarimana mnamo mwezi Aprili ya mwaka 1994.

Mauaji ya Habyarimana yaliibua mapigano makali ya kikabila yaliyosababisha mauwaji ya zaidi ya watu laki nane, wengi wao waTusti na wahutu wenye siasa zakadri.

WANAJESHI WAANDAMANA IVORY COAST

Wanajeshi nchini Ivory Coast wameingia ndani ya majengo ya radio ya taifa hilo katika mji wa Bouaké kutokana na maandamano yao ya kudai maslahi zaidi ya kazi.

Hata hivyo wanajeshi hao wamerekodi ujumbe wa madai yao, unaosisitiza wafanyakazi kuondoka katika vituo vyao vya kazi.

Waziri wa Ulinzi Ivory Cost Paul Koffi amewataka waandamanaji hao waliopo katika mji wa Bouaké na Abidjan kurejea kazini mara moja.

Ripoti zinasema kuwa lingekuwa jambo la msingi kama angelitoa ahadi ya kulipa madai ya wanajeshi hao na kuboresha mazingira ya huduma za afya na mafao mengine.

Jeshi la Ivory Cost linajumuisha askari wa zamani na wengine wakiwa ni waasi waliojiunga na jeshi la serikali kuunda jeshi jipya baada ya mgogoro wa Ivory Cost kumalizika mwaka 2011 uliokuwepo kati ya Alassane Ouattara na mtangulizi wake Laurent Gbagbo.

'OPERATION LIKOFI' VIJANA WALIKUFA KIHOLELA

Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch inasema polisi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa jumla wamewaua vijana wapatao 51 katika operesheni ya kupambana na uhalifu Kinshasa.

Watu wengine 33 hawajulikani waliko tangu operesheni hiyo ilopewa jina "Operation Likofi", ilioidhinishwa Kinshasa mwaka uliopita kufanyika.

Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya maafisa 100 wa polisi, watu walioshuhudia nauaji hayo pamoja na jamaa wa waathiriwa.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, liliwahoji zaidi ya maafisa 100 wa polisi , walioshuhudia matukio pamoja na jamaa wa waathiriwa waliotoa taarifa ya kile kilichosemekana kuwa mauaji ya kiholela.

Msemaji wa shirika la hilo,(Anneke Van Woudenberg), alituhumu serikali kwa kuficha taarifa kuhusu mauaji hayo na kusema familia za waathiriwa zilikuwa zimetishwa na kuonywa dhidi ya kufichua taarifa za mauaji hayo.

Ripoti iliyotolewa na umoja wa Mataifa mwaka jana pia ilielezea kuhusu mauaji hayo.

KOREA KASKAZINI KUPELEKWA ICC?

Baraza la umoja wa mataifa la haki za binadamu limesema Korea Kaskazini inastahili kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu kutokana na kukiuka haki za binadamu.

Katika baraza hilo zimetolewa tuhuma dhidi ya Korea Kaskazini kwamba serikali yake imekuwa ikifanya vitendo vya ukiukaji haki za binadamu.

Mapendekezo hayo yaliyopitishwa na baraza la haki za binadamu la kimataifa yanapaswa kupigiwa kura ili kupitishwa na bunge yaweze kuhalalishwa.

Ripoti ya mwezi Februari mwaka huu iliyotolewa na umoja wa mataifa ilibainisha kuwa watu wa Kawaida Korea Kaskazini wanakabiliwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu napia mauaji.

Umoja wa mataifa unafanya uchunguzi dhidi ya Korea Kaskazini ili kupata ushahidi wa majina ambayo yapo kwamba taifa hilo limeua, likitesa watu,ukatili wa kisiasa na uhalifu mwingine.

Hata hivyo China na Urusi wanaoshikilia kura ya Veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamepingana na mapendekezo hayo ya Baraza la Usalama, huku nayo Korea Kaskazini ikiipinga ripoti hiyo.

Wanadiplomasia wana wasiwasi kuwa huenda China inataka kutumia kura yake ya Veto kupinga Baraza la Usalama kupeleka kesi zake katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.

PODOLSKI KUTIMKA ARSENAL

Mchezaji wa Arsenal Lucas Podolski ataka kuihama kilabu hiyo ili kupata fursa za kuchezeshwa mara kwa mara.

Mchezaji huyo wa Ujerumani alilichezea taifa lake kwa dakika 90 dhidi ya Gibraltar siku ya ijumaa lakini anashangazwa kuona ni kwa nini hajaanzishwa kuichezea kilabu yake ya Arsenal.

Kulingana na mtandao wa Goal.com Lucas Podolski anasema kuwa mkufunzi wa kilabu hiyo Arsene Wenger anampuuza.

Mshambuliaji huyo amechezeshwa mechi nne pekee katika ligi ya Uingereza msimu huu, huku akianzishwa katika mechi ya kombe la Carling ambapo Arsenal ilipoteza kwa Southampton mnamo mwezi Septemba.

Lucas Podolski alicheza dakika 90 wakati Ujerumani ilipoicharaza Gibraltar mabao 4-0 katika mechiza kuwania kufuzu katika dimba la Ulaya, lakini mkufunzi Joachim Low anataka mchezaji huyo kuanza kuchezeshwa mara kwa mara katika kilabu yake.

Mchezaji huyo aliyetoka kilabu yaKoln nchini Ujerumani alisema kwamba anapanga kufanya mazungumzo na Arsenal kuhusu hatma yake mwezi january na akasisitiza tena siku ya ijumaa wakati taifa lake liliposhinda.

''Nimekuwa nikiichezea Arsenal kwa dakika chache ,niko tayari kuionyesha Arsenal kile naweza kuifanyia ,lakini fursa hiyo haipatikani'',alisema Podolski.

WAFUGAJI WAVAMIA SHAMBA LA MUWEKEZAJI NA KUCHOMA MOTO

Wafugaji wa jamii ya kimasai kutoka wilaya ya Longido Mkoani Arusha wamevamia shamba la mwekezaji la Ndarakwai katika wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na kuchoma moto baadhi ya maeneo na kuharibu mali mbalimbali kwa madai ya kugombania mipaka kwa ajili ya maeneo ya malisho.

Baadhi ya wananchi wamesema kundi la Wamasai kutoka vijiji vinavyozunguka shamba hilo ambalo liko Jirani na wilaya ya longido lilivamia eneo hilo wakiwa na mifugo yao na kuanza kuchoma baadhi ya mali za mwekezaji huyo, magari na nyumba za watalii kwa madai kuwa mwekezaji huyo ameoongeza maeneo ya mipaka.

Wamesema ni vema serikali ikachukua hatua ya kukutana na wananchi hao na kuwasikiliza ili kutatua mgogoro huo ambao umeaanza kuhatarisha amani.

Kutokana na mgogoro huo Mkuu waMkoa wa Kilimanjaro Bw.Leonidas Gama akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro amelazimika kutembelea maeneo hayo na kusema kuwa kitendo kilichofanyanywa na wafugaji hao hakikubaliki na kwamba wote waliohusika lazima wachukuliwe hatua za kisheria kutokana na shamba hilo kuwa na makundi ya wanyamapori 65 wakiwemo Tembo,Twiga na Pofu.

MWANAMKE ATUPWA JELA KWA KUSAIDIA ISIS

Mwanamke mmoja nchini Uingereza aliyeshitakiwa kwa kumfadhili mumewe aliyejiunga na vita nchini Syria, amefungwa jela kwa zaidi ya miaka miwili.

Amal El-Wahabi, mwenye umri wa miaka 28, alijaribu kumhadaa rafiki yake kumbebea pauni 15,800 hadi nchini Uturuki ambako mumewe angeweza kuzichukulia.

Jaji aliyetoa uamuzi katika kesi hiyo, Nicholas Hilliard, alimwambia El Wahabai kuwa alifahamu vyema kwamba mumewe Aine Davis alikuwa anapigana nchini Syria na kwa hivyo alikuwa anamsaidia katika harakati zake.

Davis, ambaye alikuwa mlanguzi wa dawa za kulevya pamoja na kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha, aliondoka Uingereza mwaka 2013 kwenda Syria kupigana na kundi la Isis.

Jaji alisema kuwa El-Wahabi anapaswa kutumikia sehemu ya kifungo chake jela na kabla ya kuachiliwa kumalizikia kifungo hicho nje.

Jaji aliongeza kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa huruma kwani mwanamke huyo ni mama wa watoto wawili wachanga.

Mapema mwaka huu Davisa ambaye anajulikana kama Hamza alimtaka mkewe kumtumia pesa hizo kupitia nchini Uturuki.

El-Wahabi, kutoka London alimuomba rafiki yake wa zamani, Nawal Msaad,kumbebea pesa hizo akimuahidi kumlipa Euro 1,000 kwa kumshukuru.

Hata hivyo, mpango huo ulitibuka baada ya Msaad kusimamishwa katika uwanja wa Heathrow na kukiri ni kweli alikuwa amebeba pesa hizo. Pesa hizo alikuwa amzificha kwa nguo zake za ndani.

Bi Msaad alisema hakujua pesa hizo zilikokuwa zinakwenda na kwa hilo mahakama ikamwachilia.

Katika hukumu yake jaji alisema ni wazi kuwa mumewe El-Wahabi alikwenda Syria kupigana chini ya kundi la kiisilamu la Isis.

"HATURUHUSU VITENDO VYA NGONO MAGEREZANI"

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeendeleza msimamo wake kuwaTanzania bado haina sheria ya kuwaruhusu wafungwa kukutana kifaragha na waume au wake zao.Hii ni mara ya tatu kwa serikali kutoa majibu hayo kutoakana na maswaliya wabunge, ambako mara kadhaa swali hilo limekuwa likiulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Msabaha (CHADEMA).

Jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima, alikiri kuwa Tanzania haina sheria hiyo na akajibu kuwa, ujauzito ambao huwapata wafungwa wanawake, unatokanana kuupata nje ya magereza.

Alitoa majibu hayo kutokana na swali la Mbunge wa Viti maalum, Rukia Kassim Ahmed (Cuf), ambaye alitaka kujua ni kwa namna gani wafungwa wanawake wanapata ujauzito wanapokuwa ndani yamagereza yao.

Mbunge huyo, pia alihoji kama magerezani kuna usiri, ni kwa namna gani mahabusi ambao ni mashehe kutoka Zanzibar wanafanyiwa vitendo vya ulawiti gerezani.

Naibu Waziri huyo, alisema kuwa Jeshi la Magereza lina utaratibu wa kutenganisha wafungwa wa kiume na wa kike, kwani kilawatu hutunzwa kwa sehemu zao na hulindwa na watu wa jinsia zao.

Kuhusu tuhuma za kulawitiwa kwa Mashehe wa Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe, alisema kuwa sakata la Sheikh Salum Ali Salumu, linafanyiwa kazi na kwamba kiongozi huyo ameshafanyiwa uchunguzi wa awali katika hospitali ya Amana.

"Jambo hilo lipo mikononi mwetu, tumempeleka hospitali ya Amana nakesho (leo) tutampeleka hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, lakinitunachunguza pia tabia ya kiongozi huyo na mwenendo wake kabla ya kuingiagerezani," alisema Chikawe.

Hata hivyo, Chikawe alisema kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa watuhumiwa hao, kwani tangu mwanzo hakuwa ameripoti vitendo hivyo lakini alipofika mara ya nnegerezani ndipo akaripoti kufanyiwa vitendo hivyo na mmoja wa askari polisi.

HABARI NJEMA KWA WASTAAFU

SERIKALI imeongeza kima cha chini cha malipo ya pensheni kwa wastaafu kuanzia mwaka wa fedha ujao.

Kwa sasa wastaafu wanalipwa pensheni ya sh 50,000 kwa mwezi, ambazo hulipwa kila baada ya miezi mitatu, lakini kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/16 watalipwa katika kiwango kipya cha juu.

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema hayo juzi wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia mjadala kuhusu mapendekezo ya serikali ya Mpangowa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka 2015/2016.

Waziri Saada, alisema kiwango hicho kipya cha pensheni kitakachoongezwa kwa wastaafu hao kitatangazwa katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2015/2016, mwakani.

"Mheshimiwa Spika, uamuzi huo umefikiwa baada ya kuona kiwango cha pensheni cha sasa chash 50,000, hakistahili kuendelea kulipwa kwa wastaafu kwa sababu hakiendani nahali ya maisha," alisema.

Pia, alisema deni sahihi, ambalo Bohariya Dawa (MSD), inaidai serikali ni sh bilioni 81 na kwamba,kati ya fedha hizo, sh bilioni 37 zimehakikiwa na kuanzia juzi sh bilioni 20 zimelipwa.

Waziri Saada, alisema mwezi ujao wataendelea kulipa sehemu nyingine ya deni hilo ambalo limetokana na uzembe uliofanywa na baadhi ya watendaji kutofuata taratibu.

Alisema kuanzia sasa,wizara yake itahakikisha taratibu zinafuatwa ili tatizo lililojitokeza lisijirudie.

NUSU YA WABUNGE WACHOKWA MAJIMBONI

KARIBU nusu ya wabunge wa majimbo yote ya uchaguzi nchini, wapo hatarini kuangushwa na wapigakura wao katika katika uchaguzi mkuu wa mwakani, kutokana na kutotekeleza ahadi walizotoa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Asilimia 47 ya Watanzania wote, wameweka wazi kutowapigia kura wabunge wao, kutokana na kushindwa kuzitekeleza au kuzitekeleza kwa kiwango kidogo ahadi, walizotoa wa kampeni za uchaguzi.Ahadi hizo zilihusisha kuboresha barabara, miradi ya maji, kujenga hospitali na zahanati, kuboresha elimu, umeme, mikopo kwa vikundi, kuongeza ajira kwa vijana, kujenga madaraja, kuboresha kilimo na kadhalika.

Hayo yamebainishwa katika ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza, iliyotolewa jana katika mdahalo ulioandaliwa na taasisi hiyo, ambao uliwakutanisha wachambuzi mbalimbali, uliokuwa na mada ya 'Tanzania Kuelekea 2015'.

Kwa mujibu wa utafiti huo, ambao hufanyika kwa njia ya simu, wapiga kura wanane kati ya 10 ambayo ni sawa na asilimia 79, bado wanakumbuka ahadi walizotoa wabunge wao wakati wa kampeni, ambapo wabunge wengi walitoa ahadi za miradi ya ujenzi, miradi ya maji, hospitali, uboreshaji wa elimuna kuongeza madarasa kama vipaumbele vyao.

Akifafanua ripoti hiyo, Mtafiti wa taasisi hiyo, Elvis Mushi alisema kitukibaya ni kuwa ni mwananchi mmoja kati ya wanane ambao ni sawa na asilimia 12, ndiye aliripoti kuwa mbunge wake ametekeleza ahadi zote.

Hata hivyo, Mushi alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kina nafasi ya kushinda uchaguzi japo kwa asilimia ndogo. Alisema takwimu zinaonesha kama uchaguzi ungefanyika Septemba mwaka huu CCM ingeibuka kidedea.

"Sauti za Wananchi iliuliza kama uchaguzi ungefanyika leo, mgombea wa chama gani ungempigia kura, kwa mwaka 2014 asilimia 51 walisema CCM, asilimia 23 Chadema na asilimia 16 walisema wanampigia mgombea na siyo chama," alisema Mushi.

Aidha takwimu za utafiti huo, zinaonesha hata kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukisimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya Urais, bado haitaweza kuiangusha CCM, kutokana na nusu ya wahojiwa ambao ni asilimi 47 walijibu kuwa wangeipigia kura CCM huku asilimia28 walijibu wangeipa kura Ukawa.

Baada ya kutolewa ripoti ya utafiti huo, ambayo pia iligusa maeneo ya utendaji wa viongozi, changamoto zinazolikabili taifa, ushindani wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM, Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema kumekuwa natabia ambayo imefanywa kuwa ni yakawaida na kubeza maoni ya tafiti kama hizo, jambo ambalo si sawa.Alisema kuwa maoni hayo, yana ukweli ndani yake na pia yanaakisi mawazo ya jamii juu ya mambo mbalimbali, ikiwemo utendaji wa viongozi wao na pia changamoto wanazotaka zitatuliwe.

"Takwimu hizi ziwe ni jicho la kuangalia matatizo yetu na kuondokana na mambo ambayo yamekuwa ni kero kwetu. Ni masuala ya msingi yanayowakera wananchi kwa sababu ni matatizo yale yale ambayo tulianza nayo tangu kipindi cha uhuru, maradhi, umasikini na ujinga," alisema.

Aidha, alitaka vyama vya siasa vikaena kutafakari kwa kuangalia hizo takwimu, kwani zimeonesha kuna mmomonyoko wa kukosa imani na vyama hivyo, jambo ambalo alisema si zuri.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, kuongezeka kwa imani ya wananchi kwenye taasisi za siasa kuliko kwa mtu binafsi ni jambo zuri kwa kuwa inaonesha ustawi mzuri wa demokrasia.

Wakati Nape akiwakilisha chama chake akiyasema hayo, vyama vya Chadema na CUF vilivyoalikwa, havikuwa na wawakilishi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani, walituma pia mwaliko kwa vyama hivyo, ingawa walishindwa kuhudhuria mdahalo huo, kutokana na sababu mbalimbali walizozitoa.

Alisema waliwasiliana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa ajili ya kumpa mwaliko huo, ambapo hata hivyo, katibu huyo inaelezwa alijibu kwa sasa viongozi wa chama hicho wamebanwa na shughuli za mikutano inayofanyika mikoani, huku kwa upande wa CUF ukikubali na kutuma mwakilishi, ambaye pia baadaye alitoa udhuru.

"Chadema walisema hawawezi hata kutuma mwakilishi, lakini CUF, Profesa Lipumba alisema atawakilishwa na Naibu Katibu MkuuBara, Magdalena Sakaya ambaye hata hivyo jana (juzi) alituma taarifakuwa asingefika angetuma mwakilishi. "Lakini mwakilishi wa CUF ambaye tuliambiwa angekuja leo (jana) asubuhi, alitoa taarifa amepata dharura hivyo hataweza kufika katika mdahalo huu, hiyo ndiyo sababu mnaona wawakilishi wa vyama vingine hawapo hapa," alisema.

Gazeti hili liliwatafuta viongozi wanaounda Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR na NLD ili kuzungumzia utafiti huo, lakini mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni hawakuweza kupatikana kupitia simu zao za mkononi.


Chanzo: Habari Leo

ROBOTI LA ULAYA LATUA KATIKA KIMONDO

Baada ya safari ya miaka kumi katika anga za juu, chombo cha anga za mbali cha Ulaya kimevuka kilomita chache za mwisho kutoka ardhini kutekeleza kile kitakachokuwa kifaa cha kwanza kuwahi kutengenezwa na binadamu kutua kwenye kimondo.

Roboti hiyo iliyotengezwa Ulaya kwa jina Philae, imefanikiwa kutua katika kimondo likiwa ni jambo la kihistoria kuwahi kushuhudiwa.

Aidha roboti hiyo ilitua katika Kimondo kinachojulikana kama 67P/Churyumov-Gerasimenko saa kumi jioni saa za Ulaya.

Kulikuwa na vifijo na nderemo pamoja na wanasayansi kupigana pambaja katika chumba ambako shughuli hiyo ilikuwa inadhibitiwa mjini Darmtadt, Ujerumani baada ya ishara kuonyesha kuwa roboti hiyo ilikuwa imetua kwenye kimondo.

Ishara ya kuonyesha kuwa roboti hiyo ilifanikiwa kutua ulikuwa mwanga kutoka kwenye roboti hiyo.

"Hii ni hatua kubwa sana katika historia ya binadamu kulingana na wanasayansi hao".

BROOKLYN BECKHAM AMWAGA WINO ARSENAL

Ni ajabu, kwamba safari hii maji hayajafuata mkondo! Mtoto wa nyota wa zamani wa Manchester United na England, David Beckham, Brooklyn amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Arsenal.

Brookyln aliyewahi kufanya mazoezi na klabu hiyo ya London amekataa kufuata nyayo za mzazi wake na kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu hiyo.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 15 alikuwa akifuatiliwa kwa karibu na klabu kama Chelsea pamoja na hata Manchester United.

Jana, gazeti ya The Daily Star lilifichua kuwa Brooklyn ambaye ni mtoto wa kwanza waDavid na mwanamitindo Victoria Beckham amesaini mkataba wa awali wa mwaka mmoja baada ya kuwafurahisha makocha wa klabu hiyo wakati wa mazoezi aliyofanya klabuni hapo hivi karibuni.

Inadaiwa kwamba Arsenal wamekuwa wakimfuatilia chipukizi hiyo kwa muda mrefu na wapo tayari kumpa mkataba wa muda mrefu, endapo ataendelea kung'ara msimu huu.

Chanzo cha habari kilichonukuliwa na The Daily Star kimefichua kuwa Brooklyn ni kijana mwenye kipaji kikubwa , ameonyesha ukomavu na utulivu kwenye mazoezi, hata mechi za timu ya watoto ambazo amekuwa akichezeshwa.

Beckham aliyeichezea kwa mafanikio klabu ya Manchester United ana watoto wanne, ambao ni Brooklyn, Harper Seven, Romeo na Cruz.

Nguli huyo wa zamani alizichezea timu mbalimbali ambazo ni Manchester United, Preston North End, Real Madrid, Milan, Los Angeles Galaxy, Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya England, ambayo imemfanya kuwa na rekodi ya kucheza michezo mingi zaidi.

Beckham ameichezea England michezo 115.

MBUNGE KEISSY ANUSUSIKA KICHAPO TENA

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy almanusura azue kizaazaa kwa mara nyingine na wabunge wa Zanzibar alipohoji sababu ya wabunge hao kuzungumzia suala la Rais Jakaya Kikwete kwenda kutibiwa Marekani akisema wenyewe wamekuwa wakienda kutibiwa India.

Mbunge huyo amekuwa akiingiakatika mgogoro na wabunge wa Zanzibar kuhusu masuala mbalimbali. Kwanza ilikuwa katika Bunge la Bajeti lililopita, alipochangia Bajeti ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akihoji mchango wa Zanzibar katika wizara hiyo na mwisho ilikuwa katika Bunge la Katiba alipokuwa akichangia suala la Muungano.

Jana, Kessy alisema hayo wakatiNaibu Spika, Job Ndugai alipokuwa akijibu miongozo mbalimbali ya wabunge walioiomba baada ya kipindi cha maswali na majibu kitendo ambacho kiliwafanya wabunge karibu wote wa upinzani kusimama wengine wakitaka atolewe nje.

Wakati Ndugai akiendelea kusikiliza miongozo hiyo, Kessy alisimama na kupewa nafasi kisha kusema: "Hao wanapiga kelele kwa nini Rais amekwenda kutibiwa Marekani mbona wao wamekwenda kutibiwa India? Tena nawafahamu wabunge kama sita hasa wa CUF, sasa Rais kaenda kutibiwa Marekani mnahoji, je, mlitaka akatibiwe Zanzibar? Kauli hiyo iliamsha hasira za wabunge wa upande wa upinzani ambao walisimama wakitaka Keissy achukuliwe hatua za kinidhamu.

Rais Kikwete yuko Marekani baada ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume kwenye Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Maryland ambako taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana,ilisema hali yake inaendelea kuimarika na alianza kufanya mazoezi ya kutembea tangu juzi.

Baada ya wabunge wa upinzani kusimama akiwamo David Kafulila (Kigoma Kusini - NCCR Mageuzi), David Silinde (Mbozi Magharibi - Chadema) na wengine wakitaka Kessy atimuliwe, Ndugai aliwaomba kuwa watulivu huku Kessy akiamua kutoka kwenye Ukumbi wa Bunge.

Wakati Kessy akitoka, Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji alinyanyuka na kuonekana kumfuata lakini alizuiwa na walinzi pamoja na Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail AdenRage na kumrudisha huku Keissy akisindikizwa na Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumbana mmoja wa walinzi wa Bunge.


Miongozo mingine

Katika miongozo ya awali, baadhi ya wabunge walitaka Serikali kutoa tamko kuhusu ununuzi wa mahindi ya wananchi hasa baada ya kuzalishwa mengi na kukosekana kwa soko, pia wengine wakitaka tamko la Serikali kuhusu tatizo la dawa tiba nchini kiasi cha kufanya wananchi kukosa matibabu.

Silinde alitaka kauli ya Serikali kuhusu ununuzi wa mahindi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Marc Mwandosya alisema wizara husika itatoa tamko hilo wiki hii... "Napenda niwaambie waheshimiwa wabunge kuwa Serikali imesikia na itatoa tamko la suala la mahindi wiki hii."

Wabunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) na Rukia Kassim (CUF) walitaka tamko la Serikali kuhusu tatizo la dawa nchini na hasa deni la Bohari yaKuu ya Dawa (MSD) pamoja na kukosekana kwa mashine ya mionzi katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.

Akijibu swali hilo, Profesa Mwandosya alisema Serikali piaitatoa tamko kuhusu hali ya tibaya saratani nchini, madaktari namipango iliyopo katika kupambana na tatizo la kukosekana kwa mashine ya mionzi Ocean Road... "Tutatoa tamko kuhusu hayo katika bunge hili."

Akizungumzia mwongozo huo, Ndugai alisema: "Kwa vile Serikali itatoa tamko, tuiombe ilete mapema suala hilo kwa kuwa limekuwa likitusumbua hapa bungeni."

MAHAKAMA YACHOMWA MOTO TARIME

MAHAKAMA ya Mwanzo ya Riagoro wilayani Rorya mkoani Mara, imechomwa moto na watu wasiojulikana na mali na nyaraka mbalimbali zilizokuwao, zimeteketea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa alisema tukio hilo ni lausiku wa kuamkia Novemba 8.

Uchunguzi wa awali unaonesha mahakama hiyo, haina umeme na inasadikiwa huenda imechomwa nawahalifu wanaotuhumiwa katika mahakama hiyo.

Moto huo uliteketeza samani na vielelezo katika ofisi ya makarani. Hata hivyo, kwa upande wa ofisi yahakimu, mafaili yalinusurika kuteketea baada ya wananchi kufika na kuzima moto huo wakisaidiana na polisi wa Kituo cha Utegi.

"Tumepeleka askari wetu wa uchunguzi katika maeneo hayo ili kuweza kupata wahusika ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria," alisema Mambosasa.

TETESI SHERIA MPYA DHIDI YA USHOGA UG

Suala la wapenzi wa jinsia moja na sheria nchini Uganda baado linazua mijadala nchini humo.

Miezi mitatu tangu mahakama nchini humo kuibatilisha sheria dhidi ya ushoga kwa sababu za kiufundi sasa habari zingine zimeanza kujitokeza kuhusu uwezekano wa serikali kuleta tena muswada huo bungeni.

Kujitokeza tena kwa suala hilo wakati huu ni baada ya hati maluum kuvujishwa. Hati hiyo yakurasa tano ni ya muswada jaribio kuhusu suala la mapenzi ya watu wa jinsia moja.

Hati hiyo inaitwa : 'Mswada wa mwaka 2014 kuzuia kueneza visa vya kujamiiana ambavyo si asili wa mwaka wa 2014.

Katika hati hiyo kuna pendekezo la kifungo cha miaka saba ikiwa mtu atapatikana na hatia ya kile kinachoweza kuitwa kufagilia ushoga.

Neno lilotumiwa ni kutangaza na hivyo kutiliwa mkazo badala ya sheria ya zamani iliokuwa inatilia mkazo ushoga wenyewe.

Wachambuzi wanasema kuwa hati hii ikipasishwa kama sheria itakuwa mbaya zaidi ya ile iliobatilishwa kwani itawahukumu watu wengi mkiwemo vyombo vya habari pamoja na watu wote wanaotumia mitandao yote ya kijamii.

*'Sheria mbadala kali zaidi?'

Hati hii inasema kuwa mtu yeyote akipatikana na hatia atahukumiwa kifungo cha miaka saba.

Sheria iliobatilishwa na mahama mapema Agosti mwaka huu miongoni mwa mengine ilikuwa inasema yeyote akipatikana na hatia atafungwa jela maisha.

Waziri wa taifa wa sheria na naibu mwanasheria mkuu Fred Ruhindi akizungumza na BBC kwasimu amekataa kutoa kauli kwa kile alichoita hati iliovujishwa na kusema kuwa mchakato kuhusu sheria mpya ya kudhidbiti ushoga unaendelea.

Yeye waziri anaehusika na maadili Padri Lokodo amesema hajui lolote kuhusu hati hiyo.

*Hatua zilizofuata

Punde baada mahakama kubatilisha sheria hiyo mapema mwezi Agosti mwaka huu, chama tawala cha NRM kiliunda kamati maalum ya watu 10, ikiongozwa na makamu wa rais Edward Sekandi, kutahmini muswada hatua hiyo.

Hadi sasa haijatoa taarifa yoyote kuhusu kazi yao mpaka muda huuambapo hati ya mwaswada kuvujishwa.

Mchakato wa kuunda sheria dhidiya ushoga ilianza mwaka wa 2009 na imepitia awamu kadhaa kutokana na utata wa suala hilo.

Huku wanaounga mkono kuweka sheria kali dhidi ya mapenzi hayo, baadhi ya makundi ya kutetea haki za binadamu pamojana mataifa ya magharibi yanapinga hilo yakisem ani kugandamiza haki za bindamu.

Na serikali pamoja na mashirika ya misaada ya kimaghari yamekata miaaada kwa serikali ya Kampala kuhusiana na suala la mapenzi ya watu wa jinsia moja.Na hivyo suala la mapenzi hayo baado linavuma Uganda.

KURA ZA MAONI CATALONIA KUTAKA KUJITENGA ZAHESABIWA

Matokeo ya kura ya maoni isiyokuwa na makubaliano iliyopigwa jana kutaka ama kutotaka jimbo la Catalonia lililoko kaskazini mashariki mwa Hispania kutaka kujitenga yanaonesha zaidi ya asilimia themanini ya wapiga kura wamepigia kura kujitenga kwa eneo hilo, huku kukiwa tayari asilimia tisini ya kura zimehesabiwa.

Kura hiyo ya maoni imelenga kutathmini idadi ya watu wanaotaka Catalonia kuwa nchi huru.

Mapema kiongozi wa Catalonia Artur Mas ameelezea zoezi hilo la upigaji kura kama ni mafanikio.

Hata hivyo serikali ya Hispania imesema kura hiyo ni ya bure na haiathiri chochote.

Waziri wa Sheria wa nchi Rafael Catala hiyo amesema zoezi hilo halikuwa la kidempokrasia na kulielezea kama lisilo na mafanikio yoyote na lisilofaa.

Zoezi hilo la upigaji kura limefanyika baada ya mahakama ya katiba nchini Hispania kuamuru kufanyika kwa kura hiyoya maoni.

RAIS KIKWETE AFANYIWA UPASUAJI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Kikwete afanyiwa upasuaji wa tezi dume

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alfajiri ya jana, Jumamosi, Novemba 8, 2014, alifanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostrate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.

Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa Rais alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.

Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa. Hali ya Mheshimiwa Rais Kikwete inaendelea vizuri, bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba.

Wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais Kikwete kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
 
Mwisho.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
09 Novemba,2014

GARI LA TRENI VYAGONGANA 12 WAFARIKI PAPO HAPO

MATUKIO ya ajali za barabarani nchini yameendelea kuteketeza maisha ya Watanzania, baada ya watu 12 kufa papo hapo katika ajali iliyohusisha basi na treni katika makutano ya reli eneo la Kiberege, wilaya Kilombero mkoani Morogoro.

Watu 40 walijeruhiwa katika ajali hiyo.

Ajali hiyo, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paul, ilitokea jana majira ya saa 9:15 alasiri ikihusisha basi aina ya Scania lenye namba za usajili T 725 ATD, mali ya kampuni ya Aljabry na treni mali ya Mamlakaya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Wakati basi hilo lilikuwa likitoka Morogoro kwenda Ifaraka, treni ilikuwa inatoka Mbeya kwenda Dar es Salaam. Kamanda Paul alisema dereva wa basi hilo ambaye hakufahamika jina mara moja hakuwa makini wakati akivuka katika eneo hilo, hali iliyosababisha gari alilokuwa analiendesha kugongwa kwa nyuma na treni.

Alisema wote waliokufa papo hapo ni abiria wa basi, kati yao sita wakiwa ni wanaume, wanawake wanne na watoto wawili wenye umri wa kati ya miaka 5 hadi 6.

Baadhi ya majeruhi waliondolewa eneo la tukio na wasamaria na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis ya mjini Ifakara.

Hata hivyo, kwa upande wa waliokufa, watatu wametambuliwa kuwa ni Flugencia Lusangila (60) na Albeta Lusangila (62), wakazi wa Ichonde, Mang'ula wilayani Kilombero na Joseph Kuzwila (34) mkazi wa Dar es Salaam.

Mara baada ya kusababisha ajali, dereva alikimbia na kwamba Polisi inaendelea kumtafuta sambamba na kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.

UFAULU DARASA LA SABA JUU, MPANDA YAONGOZA WILAYA 10 BORA

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2014 yanayoonesha kuwa, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 6.38 huku Kanda ya Ziwa iking'ara kwa kuwa na shule nane kati ya kumi bora kitaifa.

Shule nyingine mbili zinazokamilisha kumi bora ni za mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Aidha, mwanafunzi bora kitaifa ametajwa kuwa ni Rolly Gedi Mabura wa Shule ya Twibhoki ya Mara aliyepata alama 243 kati ya alama 250.

Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde alisema wanafunzi451,392 kati ya 792,118 waliofanya mtihani wamepata jumla ya alama 100 na zaidi kati yaalama 250, ambayo ni sawa na asilimia 56.99 ambapo mwaka janaufaulu ulikuwa asilimia 50.61.

Hata hivyo, alisema wanafunzi 340,726 wamefeli mtihani huo kwa kupata madaraja ya D na E. Alisema wasichana wamefanya vizuri kuliko wavulana ambapo wanafunzi 224,909 sawa na asilimia 60.87 ni wasichana na 226,483 ambayo ni asilimia 53.59 ni wavulana.

Msonde alisema miongoni mwa wanafunzi waliofaulu wenye ulemavu ni 795 (wasichana 355 ambayo ni asilimia 44.65 na wavulana 440 sawa na asilimia 55.35.)

Akizungumzia ufaulu katika madaraja mbalimbali ni kuwa wanafunzi 10,331 (asilimia 1.30) wamepata Daraja A, Daraja B ni wanafunzi 98,789 (asilimia 12.47) na Daraja C ni wanafunzi 342,272 (asilimia 43.21) wakati waliopata Daraja D ni 321,939 asilimia 40.64na Daraja E ni wanafunzi 18,787.

Watahiniwa 792,122 kati ya 808,085 wa Shule za Msingi walisajiliwa kufanya mtihani, walifanya mtihani huo uliofanyika Septemba 10 hadi 11, 2014.

Aidha, alisema takwimu za matokeo zinaonesha ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 0.64 hadi 8.94 ikilinganishwa na mwaka jana, huku watahiniwa wakifaulu zaidi somo la Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 69.70 na kiwango cha chini zaidi ni Hisabati ambayo ufaulu wake ni asilimia 37.56.

Kiingereza ni asilimia 38.84, Maarifa ya Jamii asilimia 57.33 na Sayansi asilimia 54.89.

Shule Bora Msonde alitaja shule kumi bora kitaifa kuwa ni Twibhoki (Mara), Mugini, Peaceland na Alliance (Mwanza), Kwema (Shinyanga), St. Severine (Kagera), Rocken Hill (Shinyanga), Tusiime (Dar es Salaam), Imani (Kilimanjaro) na Palikas (Shinyanga).

Alisema mikoa kumi iliyofanya vizuri kitaifa ni Dar es Salaam ambayo imeongoza, Kilimanjaro, Mwanza, Iringa, Arusha, Tanga, Njombe, Kagera, Geita na Mtwara wakati wilaya zilizofanya vizuri kitaifa zimeongozwa na Mpanda Mjini (Katavi) na kufuatiwa na Biharamulo (Kagera), Halmashauri ya Moshi (Kilimanjaro), Kibaha (Pwani), Halmashauri ya Arusha (Arusha), Kinondoni (Dar es Salaam), Korogwe Vijijini (Tanga), Ilala (Dar es Salaam), Iringa (Manispaa) na Mji wa Makambako (Njombe).

Aidha, alisema Baraza limefuta matokeo ya mtahiniwa mmoja aliyebainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo ukilinganisha nawatahiniwa 13 wa matokeo ya mwaka jana.

"Baraza linachukua fursa hii kuzipongeza Kamati za Uendeshaji Mitihani za mikoa, wilaya na walimu waliosimamia mtihani hii kwa kuzingatia ipasavyo kanuni za usimamizi wa mitihani ya taifa,"

Waliopata alama za juuMsonde alisema watahiniwa 7,600 wamepata alama 50/50 katika somo la Kiingereza, wanafunzi 32 somo la Kiswahili na hisabati ni wanafunzi 34 ambapo wasichana ni wanane na wavulana 26.

BERAHINO AITWA THE THREE LIONS, ARSENAL YATOA NYOTA WATANO

Mshambuliaji wa West Bromwich Albion Saido Berahino mwenye asili ya Burundi ametajwa kwenye timu ya Taifa ya England.

Mshambuliaji huyo mwenye umriwa miaka 21 anatarajiwa kuonekana kwenye orodha ya majina ya timu ya England katika mechi ya kimataifa ya kuwania kufuzu fainali za Euro mwaka 2016 kati England Slovenia mechi itakayopigwa Novemba 15 mwaka huu.Berahino ambaye alizaliwa nchini Burundi tayari ameshatia wavuni magoli saba katika mechi 10 za ligi kuu ya England ambayo timu yake West Bromwich imecheza kwa msimu huu.

Timu kamili iliyotajwa na kocha England Roy Hodgson hii hapa chini


Walinda Mlango:

Fraser Forster, Ben Foster na JoeHart


Safu ya Ulinzi:

Leighton Baines, Gary Cahill, Calum Chambers, Nathaniel Clyne, Kieran Gibbs, Phil Jagielka,Luke Shaw na Chris Smalling.


Viungo:

Ross Barkley, Michael Carrick, Stewart Downing, Jordan Henderson, Adam Lallana, James Milner, Alex Oxlade-Chamberlain, Raheem Sterling, Andros Townsend, Jack Wilshere na Theo Walcott.


Washambuliaji:

Rickie Lambert, Wayne Rooney, Daniel Welbeck na Saido Berahino.

NDEGE YA RAIS YATUMIKA KUSAFIRISHA PEMBE ZA NDOVU

Inadaiwa kuwa wanunuzi, raia wa Uchina walinunua maelfu ya kilo za pembe za ndovu nchini Tanzania na kuzitorosha kutoka nchini humo katika ndege ya kibinafsi ya raia wa Uchina Xi Jinping,wakati alipozuru bara Afrika.

Kulingana na shirika la ujasusi la mazingira lililo na makao yake mjini London.

Pembe hizo zilinunuliwa wiki moja tu kabla ya ziara ya rais huyo wa Uchina nchini tanzania mwaka ulioipita ambapo zilifichwa katika mifuko ya wanadiplomasia ili kutokamatwa.

Shirika hilo pia linadai kwamba wajumbe waliokuwa wakiandamana na Rais Xi walinunua viwango vikubwa vya pembe hizo.

Uuzaji wa Pembe za ndovu ulipigwa marufuku mwaka 1989 ili kuwazuia wawindaji haramu kuwaua ndovu.


*TANZANIA YASHTUSHWA

Tanzania imeshtushwa na ripoti inayoelezea biashara haramu ya meno ya tembo kati ya baadhi yaviongozi wa nchi hiyo na China Serikali ya nchi hiyo imesema imesikitishwa na ripoti iliyotolewa na taasisi ya uchunguzi ya mazingira inayodai kwamba majangili wa kichina wakishirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali ya Tanzania ndio wanaoangamiza idadi ya tembo kutokana na biashara haramu ya meno ya tembo.

Inadaiwa kwamba raia wa China walitumia ziara ya rais wao nchinihumo kusafirisha kimagendo maelfu ya kilo za pembe za ndovu.

Kulingana na shirika la utafiti wa mazingira, EIA, Pembe hizo zilinunuliwa wiki moja tu kabla yaziara ya rais huyo nchini tanzania mwaka jana na zilifichwa katika mifuko ya wanadiplomasia ili zisitambuliwe.

Msemaji wa serikali Assah Mwambene amemwambia mwandishi wa BBC Aboubakar famau kwamba ripoti kama hiyo zinatatiza jitihada za serikali kukabiliana na uuzaji haramu wa pembe za ndovu.

WATU WAWILI WAUAWA, MMOJA ACHINJWA

Watu wawili wamefariki dunia mkoani Iringa katika matukio mawili tofauti, likiwamo la Maurisia Malangalila aliyeuawa kwa kuchinjwa shingo kama kuku na kitu chenye ncha kali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Maurisia (65), mkazi wa kijiji cha Bumulianga, Tarafa ya Malangali, inadaiwa aliuawa na Patrick Ngelenge.

Alisema mauaji hayo yalitokea Novemba mosi, saa tatu usiku kijijini hapo wakati marehemu alipokuwa nyumbani kwake.

WALIOKUWA WAMEHUKUMIWA KESI YA EPA WAACHIWA HURU

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru wafanyabiashara watatu, wakiwemo mume na mke, waliokuwa wamehukumiwa kifungocha miaka 13 na miezi sita jela kwasababu ya wizi wa Sh bilioni 1.1 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya(EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Walioachiwa huru ni mume Manase Makale na mkewe Edda Makale, na mfanyabiashara mwingine Bahati Mahenge.

Washitakiwa hao waliachiwa mwisho wa wiki iliyopita baada ya Jaji Augustine Shangwa kukubali rufaa iliyowasilishwa na wafanyabiashara hao kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka jana.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Shangwa alisema anawaachia huru wafanyabiashara hao kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kabisa kuthibitisha mashitaka dhidiyao.

Aliamuru wafanyabiashara hao waachiwe huru mara moja na kutengua amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyowataka warejeshe fedha hizo mara baada ya kutumikia kifungo.

Katika rufaa, wafanyabiashara walikuwa wakipinga hukumu iliyotolewa na jopo la mahakimu Sekela Mushi, Sam Rumanyika na Lameck Mlacha, wakidai kuwa kulikuwepo na upungufu mkubwa wa kisheria na kihoja katika kuwatia hatiani.

Katika hukumu iliyotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahenge alitakiwa kutumikia kifungo cha miaka saba jela, Makale kifungo cha miaka mitano jela na mkewe Edda kifungo cha mwaka mmoja na nusu.

Aidha, mahakama iliamuru baada ya kutumikia adhabu hiyo, Mahenge na Makale warejeshe kiasi cha Sh bilioni 1.18 walichodaiwa kukiiba katika akauntiya EPA.

Washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kutenda kosa, kughushi nyaraka mbalimbali na kuziwasilisha sehemu husika na kuiba fedha hizo.

Katika kesi hiyo, wafanyabiashara hao walikuwa wameshitakiwa na wenzao Davis Kamungu na GodfreyMushi ambao waliachiwa huru katika Mahakama ya Kisutu kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao bila kuacha shaka.

BOMU LAUA NA KUJERUHI BAADA YA KULIPUKA NDANI YA GARI SHINYANGA

KIJANA Juma Rashid anayesadikiwa kuwa na umri kati ya 21 na 23 amekufa baada ya kujeruhiwa vibaya na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu kilicholipuka ndani ya gari na kumkata kiganja cha mkono, mguu na tumbo, huku watu wengine watatu waliokuwa ndani ya gari hilo nao wakijeruhiwa.

Tukio hilo lililothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Longinus Tibishubwamu, limetajwa kutokea jana saa moja na dakika 45 asubuhikatika eneo la Mhunze, Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kamanda Tibishubwamu, kitu hicho kinachodhaniwa kuwa bomu kililipuka ndani ya gari lenye namba za usajili T848 AKA aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Mohammed Hemed Zahoro, mkaziwa Ngara lililokuwa linaendeshwa na Khalifa Mussa (39), mkazi wa Ngara mkoani Kagera.

Alisema Rashid aliyekuwa utingo wa gari hilo, alikufa papo hapo baada ya mlipuko huo uliotokea ghafla na kujeruhi pia watu wengine watatu waliokuwa ndani ya gari hilo.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Donald Nzugirwa alijeruhiwa mkono, Seni Edward aliyejeruhiwa bega na Maganga Pius aliyejeruhiwa paja, mkono na sehemu za mgongoni. Dereva wa gari hilo hakujeruhiwa popote.

Alisema majeruhi wametibiwa katika hospitali ya mkoa na kuruhusiwa ikiwa jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi juu ya chanzo cha tukio hilo.


Chanzo: Habari Leo

MDAHALO WA KATIBA WAKATISHWA NA VURUGU

Mdahalo uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini DSM umeshindwa kuendelea kutokana na vurugu zilizojitokeza ukumbini hapo.

Mdahalo huo uliokuwa unahusu Elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa ulikuwa umeandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kushirikisha waliokuwa makamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji mstaafu Joseph warioba.

Jaji warioba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuichambua Katiba inayopendekezwa, na kuelezea mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na masuala ambayo Bunge La Katiba limeyaacha kutoka katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume hiyo.

Katika maelezo yake, Jaji Warioba ameeleza kusikitishwa kwake na kuachwa kwa mambo ya muhimu ikiwa ni pamoja na miiko ya uongozi pamoja na Tunu za Taifa, lakini amepongeza baadhi ya mambo kuboreshwa ikiwa ni pamoja na Haki za Binadamu.

Kuhusu muundo wa muungano, Jaji Warioba amesema kuwa muundo uliopendekezwa katika Katiba Inayopendekezwa haufai na kuwa unasababisha mgogoro mkubwa zaidi wa muungano, hasa katika suala la kiuchumi.

Amesema Katiba hii inasababisha kile kinachoitwa koti la muungano kimekuwa kikubwa zaidi zaidi, na kuna uwezekana mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar yakashindikana hali inayoweza kuzalisha kuwepo kwa nchi mbili zenye Katiba tofauti ndani ya nchi moja.

Wakati akielezea umuhimu wa kuweka miiko ya uongozi kwenye Katiba, ndipo baadhi ya vijana wakatoa mabango yenye ujumbe wakupinga hotuba ya Warioba na kuunga mkono katiba inayopendekezwa.

Bango mojawapo lilisomeka "TUMEIPOKEA, TUNAIKUBALI NA TUNAIUNGA MKONO KATIBA PENDEKEZWA"

Baada ya hapo kilichofuata ni vurugu zilizoambatana na mapigano miongoni mwao kati ya wanaounga mkono katiba na wanaopinga.

KAMBI YA JESHI YAVAMIWA

Wanajeshi katika kambi ya jeshi ya Nyali iliopo mjini Mombasa pwani ya Kenya wamewaua kwa kuwapiga risasi watu 6 baada ya genge la wahalifu kuvamia kituo hicho cha jeshi mapema leo.

Inadaiwa kuwa kundi la watu 15 lilijaribu kuvamia kambi hiyo mwendo wa saa kumi na moja alfajiri ya jumapili.

Wanajeshi waliokuwa katika zamu waliweza kulidhibiti kundi hilo ambapo watu watano waliuawa huku askari mmoja akiweza kujeruhiwa kwa kukatwa na mapanga na wavamizi hao.

Kufikia sasa maafisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha shambulizi jilo.

Hata hivyo wengi wanashuku watuhao huenda ni wanachama wa kundi la Mombasa Republican Council MRC.

Lakini msemaji wa kundi hilo Randu Nzai amekanusha habari hizo akisema kuwa kundi hilo halikuhusika kamwe.