WATUHUMIWA ULIPUAJI MABOMU ARUSHA WATAJWA

WATUHUMIWA 19 wa ulipuaji mabomu mkoani Arusha, majina yao yamewekwa hadharani jana na leo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Watuhumiwa hao ni pamoja wanaodaiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika viwanja vya Soweto, wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa Chama cha Demokrasiana Maendeleo (Chadema) uliofanyika Juni 15, 2013.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema askari Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa watuhumiwa wengine akiwemo mtuhumiwa Yahaya Hella, ambaye anatafutwa sana na polisi akihusishwa na matukio mbalimbali ya ulipuaji mabomu.

Alifafanua kwamba mahojiano kati ya polisi na watuhumiwa hao, ndiyo yaliyotoa mwanga wa kukamatwa kwa watuhumiwa wengine na kuunganishwa katika kesi mbalimbali ambazo tayari zilishapelekwa mahakamani.

Mbali na mashitaka ya kulipua mabomu, Kamanda Sabas alisema watuhumiwa hao leo watakabiliwa pia na mashitaka ya kumwagia watu tindikali na kuhamasisha vitendo vya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, baadhi ya watuhumiwa walishiriki katika tukio zaidi ya moja hali inayoonesha ulikuwa mtandao.

Hata hivyo tofauti na ilivyotarajiwa, Chadema iliposhirikishwa katika kuwapata watuhumiwa, kutokana na madai kwamba ina ushahidi wa aliyetupa bomu katika viwanja vya Soweto, viongozi wa chama hicho walishindwa kutoa ushahidi.

Akizungumza jana katika utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na Taifa kila mwisho wa mwezi, Rais Jakaya Kikwete, alisema watuhumiwa waliokamatwa safari hii, wanaelekea kutoa sura nzuri zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili jijini Arusha na kwingineko nchini. Alipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri ya kukamata watuhumiwa wa mashambulio ya mabomu.

"Kila lilipotokea shambulizi uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa kukamatwa. Lakini, watuhumiwa waliokamatwa safari hii wanaelekea kutoa sura nzuri zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili pale Arusha na kwingineko nchini," alisema Rais Kikwete.

Alisema watu 38 wameishafikishwa Mahakamani, wengine watafikishwa mahakamani kesho na uchunguzi na msako unaendelea kote nchini kuwapata watuhumiwa wengine.

Ameomba vyombo hivyo viongeze bidii, maarifa na ushirikiano mpaka wote waliohusika wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Aidha Rais Kikwete alishukuru wananchi waliotoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa.

"Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wananchi wenye taarifa kuhusu wanaotafutwa au yeyote anayejihusisha na vitendo hivi viovu watoe taarifa kwenye vyombo vya usalama ili hatua zipasazo zichukuliwe," alisema Rais Kikwete.

Tukio la kwanza ni la mlipuko wa bomu uliotokea nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo, Oktoba 25 mwaka 2012, ambapo watuhumiwa wanne walikamatwa.

Watuhumiwa hao ni Yusuph Huta (30), mkazi wa Ngusero, Kassim Ramadhan (34), mkazi wa Kaloleni na Shekhe wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa na Abdul-Aziz Mohamed (49), ambaye ni mkazi wa Faya ambaye pia alikuwa ni Imamu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa.

Tukio la pili ni la mlipuko wa bomuuliotokea katika Kanisa Katoliki la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti Mei 5 mwaka jana ambapo watuhumiwa 12 wanadaiwa kuhusika.

Watuhumiwa hao ni Huta (30), ambaye anadaiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo na Ramadhan Waziri (28) ambaye ni mkazi wa Kwa mrombo.

Wengine ni Abdul Humud (30) ambaye ni wakala wa mabasi ya Mohamed Trans ambaye pia aliwahi kufikishwa mahakamani akishitakiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama.

Pia yupo Jafar Lema (38) aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Quba, ambaye pia alifikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na tukio la bomu katika mgahawa wa Vama, Said Ramadhan (34) ambayeni mwendesha bodaboda Standi Kuu Arusha na Kassim Ramadhan (34) ambaye ni dereva wa bodaboda eneo la Friends Corner, Arusha.

Watuhumiwa wengine ni Abashar Omar (24) ambaye ni dereva wa bodaboda Stendi Kuu Arusha, Abdulrahaman Hassan (41), mfanyakazi wa Benki ya Stanbic Arusha na Morris Muzi (44) mkazi wa Kilinzi mkoani Kigoma.

Pia yupo Niganya Niganya (28) mkazi wa Businde Ujiji mkoani Kigoma, Baraka Bilango (40), ambaye ni mkazi wa Kalinzi mkoani Kigoma na Hassan Omar (40) mkazi wa Ilongero mkoani Singida.

Tukio la tatu ni la mlipuko wa bomu Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema Juni 15 mwaka jana, ambalo viongozi wa kitaifa wa chama hicho walidai kuwa na ushahidi wa mhusika wa bomu hilo.

Watuhumiwa waliokamatwa na Polisi, baada ya Chadema kukataa kutoa ushirikiano ni Huta (30) mkazi wa Ngusero, ambaye pia anadaiwa kushiriki katika ulipuaji wa bomu nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo na katika Kanisa la St Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Mwingine ni Humud (30) ambaye ni wakala wa mabasi ya Mohamed Trans, ambaye pia aliwahi kufikishwa mahakamani akishitakiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama, na pia anadaiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Wengine ni Jafar Lema (38) mkazi wa Ngulelo, Arusha, Said Temba (42), ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Kilombero, Morogoro ambaye pia alifikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama.

Pia yupo Kassim (34) mbaye ni dereva wa bodaboda eneo la Friends Corner na anatuhumiwa pia kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti na Ramadhan Omar (24), mkazi wa Arusha.

Wengine ni Hassan (41) ambaye ni mfanyakazi wa Benki ya Stanbic na Muzi (44), Niganya (28) na Bilango (40) wanaotokea Mkoa wa Kigoma na Omar (40) anayetokea Singida, ambao pia wanadaiwa kushiriki ulipuaji bomu katika Kanisa Katoliki la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Tukio la nne ni la kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Said Makamba, lililotokea katika Msikiti wa Kwamrombo Julai 11/2013. Watuhumiwa wapo wanne ambao ni Huta (30) anayedaiwa kushiriki katika mlipuko wa bomu uliotokea nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo, mlipuko wa bomu uliotokea katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti na mlipuko wa bomu katika viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema.

Mwingine ni Waziri (28) anayedaiwa pia kushiriki katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Mtuhumiwa mwingine ni Kassim (34) mbaye ni dereva wa bodabodaeneo la Friends Corner na anatuhumiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti na mlipuko wa bomu katika viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema na Jafar Lema (38)Tukio la tano ni la kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Mustapha Kiago wa Msikiti Mkuu Februari 28 mwaka huu, ambapo watuhiwa wanne wametajwa ambao ni Huta (30), Kassim Ramadhan (34), Jafar Lema (38) na Hassan Mfinanga (57).

Tukio la sita ni la bomu Arusha Night Park lililotokea Aprili 13 mwaka huu, ambapo watuhumiwa wawili ambao ni Jafar Lema (38) naIbrahim Lenard maarufu kwa jina la Shekhe Abuu Ismail (37) mkazi wa mabatini Mwanza watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.

Katika tukio la sita ni bomu nyumbani kwa Shekhe Sudi Ally Sudi, lililotokea Julai 3 mwaka huu,ambapo watuhumiwa nane watafikishwa mahakamani akiwepo Yahaya Twahir (37) ambaye ni mfanyabiashara mtaa wa Bondeni na Idd Yusuph (23), mkazi wa mtaa wa Jaluo.

Wengine ni Said Temba (42), ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Kilombero, Morogoro ambaye pia alifikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama na pia ametajwa katika tukio la bomu Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema.

Mwingine ni Anwar Hayael (29) ambaye ni mfanyabiashara, Jafar Lema (38), Hassan Mfinanga (57) ambaye pia ametajwa katika tukio la kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Mustapha Kiago wa Msikiti Mkuu.

Wengine ni Yusuph Ramadhan (23) mkazi wa Ngusero na Omar (24) ambaye ametajwa pia katika tukio la mlipuko wa bomu Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema.

Kukutwa na mabomu Tukio la nne ni la kupatikana kwa mabomu Julai 21 mwaka huu, ambapo watuhumiwa 10 watafikishwa mahakamani wakiwemo mume na mke.

Watuhumiwa hao ni Huta (30) ambaye anatajwa katika matukio mengi na mkewe Sumaiya Ally (19)wakazi wa Ngusero na Waziri (28) anayedaiwa pia kushiriki katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti na kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Said Makamba.

Pia yupo Mfinanga (57) na Omar (24), Muzi (44) na Niganya (28) ambao wametajwa katika matukio kadhaa, Kimoro Mchana (25) mkaziwa Itolwa Kondoa, Hassan Omar (40) mkazi wa Mkoa wa Singida na Baraka Ntembo (40) mkazi wa Arusha.

Kosa la tisa ni la kuhamasisha vitendo vya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii, ambalo watakaotakiwa kujibu mashitaka yake ni Lenard (37), anayetajwa katika tukio la bomu la Arusha Night Park, Hayel (29) anayetajwa katika tukio la bomu nyumbani kwa Shekhe Sudi na Yasin Shaban (20), mkazi wa Arusha.

Kamanda Sabas alisema operesheni ya kukamata watuhumiwa wengine bado inaendelea nchi nzima, na tayari wanayo majina ya watuhumiwa kadha ambao wametoweka Arusha kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.