Amesisitiza kuwa yeye si msaliti, bali anachojali ni maslahi ya wananchi kwanza na maslahi ya vyama vya siasa, yanafuata baadaye. Pia, Arfi ameonya kwamba baadhi ya vyama vya siasa, hivi sasa vinataka kupora mamlaka ya wananchi, kuhusu mchakato wa katiba, kitu ambacho si sahihi na kinapaswa kuepukwa.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge jana, muda mfupi baada ya kukamilisha taratibu za usajili kwa ajili ya kushiriki vikao vya Bunge hilo, Arfi alisema yeye anafuata maslahi ya wananchi wake waliomtuma na wala si vinginevyo.
"Bunge Maalumu la Katiba limeundwa kwa mujibu wa sheria, ambayo sote tulishiriki kuiandaa, ambayo inasema kutakuwa na makundi matatu, ambayo ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wateule 201 wa Rais kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
"Hivyo mimi ni Mbunge wa Mpanda Kati, naingia kwa mujibu wa Katiba, nina haki kisheria kuwakilisha wananchi wangu, vyama visitake kupora mamlaka ya wananchi waliotutuma," alisema Arfi.
Alisisitiza kuwa kushiriki kwake vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hakumaanishi yeye ni msaliti kama baadhi ya watu wanavyodai, bali wale wanaoshindwa kuhudhuria vikao, ndiyo wasaliti wa wananchi.
Alisema kwamba msimamo wake katika muundo wa serikali, unabakikuwa serikali tatu, na bado yeye ni mwanachama wa Chadema.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba halina wajumbe wa chama tawala wala wa upinzani, kama ilivyo katika Bunge la kawaida la Tanzania.
"Bunge Maalumu la Katiba lina makundi ambayo naweza pia kusema mawili, wajumbe kutoka Tanzania Bara na wajumbe kutoka Zanzibar, hakuna Kambi Rasmi ya Upinzani kama ilivyo katika lile bunge letu, hivyo mimi nimekuja kama Mjumbe wa Tanzania Bara," alisisitiza.
Alieleza kuwa jana alitarajia kuhudhuria vikao vya kamati yake Namba 10, kujadili rasimu hiyo. Alisema kwamba kinachotakiwa bungeni ni hoja na suala la wingi au uchache halina nafasi, kwani kuna wakati wakiwa wachache wanaweza kusikilizwa kama wakiwana hoja. Pia, alieleza kuwa suala la muundo wa serikali haliwezi kumfanya akae nje, kwani yapo mambo mengi ya kimsingi ya kwenda kujadili, ambapo yeye atatoa mawazo yake akiwa ndani bungeni na wala si vinginevyo.
Arfi, ambaye amepata kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema kabla ya kujivua nyadhifa zote alizokuwa nazo kwenye chama hicho mapema mwaka huu, anakuwa Mbunge wa tatu wa Chadema kujisajili kwa ajili ya kushiriki vikao vya Bunge hilo. Wengine ni Leticia Nyerere na John Shibuda.
Mjumbe mwingine ni Clara Mwatuka ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (CUF).
Wakati huo huo, Sitta alisema idadiya wajumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) itazidi kuongezeka katika kuhudhuria vikao kadri siku zinavyoenda, kwa vile Rasimu ya Katiba ina mambo mengi ya msingi yanayojadiliwa.
Alitoa kauli hiyo jana mjini hapa, kutokana na swali aliloulizwa na waandishi wa habari, waliotaka maoni yake kuhusu wajumbe wa Ukawa, ambao wameanza kujisajili.
"Wataongezeka kadri siku zinavyoenda…unajua katika rasimukuna mambo mengi sana ya kujadili na utaonekana mtu wa ajabu kama haupo, mfano wewe mjumbe unatoka katika jimbo la wafugaji na suala hilo linajadiliwa halafu haupo, kuna mambo ya ardhi na mengine mengi.
"Kamati zetu mbalimbali tangu jana (juzi) zinaendelea kujadili Suraya Pili na ya Tatu, mijadala imekuwa mizuri sana na wajumbe wanatoa michango kwa nia ya kuboresha rasimu," alisema Sitta.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Ukawa wamekataa kuzungumza na yeye, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo maalum, Samia Suluhu Hassan na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, hivyo kama kuna wanaotafuta namna ya kuzungumza nao, basi ni nje ya ofisi yake.
"Kama kuna vyama huko vinazungumza sijui," alisema. Alisema anaamini mjadala wa kamati mbalimbali, zitakapokuwa zinawasilisha bungeni ripoti zao kuanzia Septemba 2, mwaka huu idadi ya wajumbe waliokuwa wamesusia, itakuwa imeongezeka kurejea bungeni, kutokana na kuwepo maslahi ya wananchi yanayojadiliwa.
Akizungumzia hali hiyo jana, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alisema mjumbe wa Ukawa atakayeshiriki vikao vya Kamati na Bunge, atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama." Msimamo wa Ukawa ni kuwa wajumbe wanaotoka Ukawa kutoshiriki vikao vya Bunge au kamati mpaka hapo tutakaporidhiana, na mpaka sasa hilo halijafanyika.
"Kutoa maelekezo ni jambo moja na kutekeleza ni jambo jingine, hivyo mjumbe atakayeshiriki vikaovya Bunge au Kamati, atakuwa ameshindwa kutekeleza agizo la chama, hivyo litakuwa ni suala la chama na atashughulikiwa kwa taratibu za chama," alisema.
Alisema jamii inatakiwa kuelewa kuwa wabunge ambao vyama vyao vimekataa kushiriki vikao vya Bunge Maalumu, hawana kosa kuonekana Dodoma, viwanja vya Bunge na kuwasiliana na wajumbe wa 201 na wale wa Chama Cha Mapinduzi."
Mbunge kuonekana viwanja vya Bunge au Dodoma si kosa, kwani Bunge Maalumu la Katiba linatumia majengo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ambayo pia shughuli zingine za Bunge zinaendelea.
"Hata mimi (Mbowe) ukiniona viwanja vya Bunge si kosa, ofisi zangu ziko katika majengo ya Bunge, pia kuna masuala mbalimbali ya maslahi ya wabunge, mishahara, majalada na masuala ya utumishi wa wabunge yanafanyika hapo," alisema.
Akizungumzia tamko la Mbowe kwamba watakaohudhuria Bunge hilo, watachukuliwa hatua kulingana na taratibu za chama, Arfi alisema ifike mahali unapofanyika uamuzi, uzingatie hoja.
Alisisizita kuwa ni haki yake, kufanya hivyo na ikiwa vipo vyama visivyozingatia demokrasia, ni jambo la kushangaza katika uendeshaji wa nchi.
Alisema mgogoro uliopo ni juu ya tafsiri ya Kifungu Namba 25 cha Sheria, ambayo waliitunga wabunge wenyewe.
Arfi alisema kwa kuwa wabunge ndiyo waliotunga sheria husika, hakuna mahali pengine ambako tafsiri ya sheria hiyo, inaweza kupatikana isipokuwa mahakamani.
"Njia pekee ni mahakamani na si kujadili nje ya Bunge au kususa," alisema Arfi.