BOMU LATUPWA NDANI YA HIACE LAUA WATATU

Watu watatu wamekufa, akiwemo mtoto mchanga ambaye mashuhuda wanasema "alitupwa nje," baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace kurushiwa bomu na watu wasiojulikana huko Kasesema, Kigoma alfajiri ya leo.

Shambulizi hilo limefanyika jirani na Kambi ya Jeshi ya Migongo wilayani Buhigwe majira ya saa 11 alfajiri, wakati basi hilo likivusha abiria toka Kilelema kwenda Kasulu Mjini.

Watu wengine 6 wamejeruhiwa vibaya katika tukio hilo la kutisha, ameeleza kamanda wa polisi (OCD) wa wilaya ya Buhigwe, Samuel Utonga.

Mashuhuda wameiambia Mwananchi kwamba, wakati Hiace hiyo ilipokuwa ikipita eneo la Migongo, alijitokeza mtu mwenye bunduki, akasimama katikati ya barabara akiishinikiza isimame.

Alipoona dereva hapunguzi mwendo, haramia huyo alilipisha hilo basi, ambalo lilosonga mbele umbali mfupi tu kabla ya mtu mwingine kujitokeza toka kusikojulikana na kulirushia bomu.

Taarifa toka wilayani humo leo mchana zinasema hali ya wahanga hao wa bomu "imezidi kuwa mbaya," hivyo imebidi wahamishwe toka hospitali ya Muyama na kupelekwa Kasulu Mjini kwa tiba zaidi.

Chanzo: Mwananchi