Mkutano huo wa siku mbili unafanyika kuanzia leo ukianza na mkutano wa biashara kati ya Afrikana Marekani. Unafuatiwa na mkutano wenyewe wa Marekani naAfrika utakaofanyika kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles mjini Washington, Rais Kikwete alipokewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Kwenye ziara hiyo, Rais Kikwete ameongozana na mkewe, Mama Salma Kikwete ambaye naye atakuwa na programu tofauti wakati wa ziara hiyo, kama watakavyokuwa wake wa viongozi wengine wa Afrika wanaohudhuria mkutano huo.
Mkutano huo wa kwanza wa aina yake kati ya kiongozi wa Marekani na viongozi wa Afrika umepangwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi 47 ambazo zote zimealikwa naRais Obama kushiriki mkutano huo.
Mbali na shughuli zake nyingi za mjini Washington, Rais Kikwete atasafiri kwenda Dallas, Jimbo la Texas, ambako atakutana na Rais wa 43 wa Marekani, George W. Bush, kabla ya kuendelea na safari katika mji mwingine mkubwa wa jimbo hilo wa Houston.
Mjini Houston, Rais Kikwete atafanya mkutano wa kimkakati wakibiashara na wafanyabiashara maarufu mbalimbali hasa wa sektaya gesi na mafuta kabla ya kumaliza ziara yake.
Miongoni mwa shughuli zake, Mama Salma Kikwete atahudhuria mkutano wa wake wa marais wa Afrika na mke wa Rais wa Marekani, Michelle Obama utakaofanyika kwenye Kituo cha John F Kennedy.
Mkutano huo utahudhuriwa pia na mke wa Rais George W. Bush, Mama Laura Bush.