Imeelezwa kuwa katika majimbo ya Bavaria na Baden Wurttemberg sadaka (zaka) ni asilimia nane ya mapato halisi.
Maeneo mengine ya Ujerumani sadaka ni asilimia 9. Kwa mujibu wa taarifa zinazopatikana mtandaoni zinasema kwamba mwaka huu kumekuwepo na kundi kubwa linalojiondoa katika Ukristo (Ukatoliki na Uprotestanti) nchini humo.
Waumini elfu kumi wa Kiprotestanti wamejiondoa kutoka Kanisa la Berlin, idadi inayoelezwa kuwa kubwa kuliko waliojitoa mwaka 2011 na 2012 wakichanganywa pamoja.
Aidha ukanda wenye Ukatoliki mkubwa wa Bavaria,Wakatoliki 14,800 walijiondoa kati ya Januari na Juni mwaka huu ukilinganisha idadi ya waliojiondoa 2013 kwa mwaka mzima. Zaka ya kanisa nchini humo hukatwa moja kwa moja na Hazina ya Ujerumani.
Mpaka mwaka huu walipa kodi walitakiwa kujieleza kuhusiana na zaka lakini kuanzia mwaka ujao zaka hizo zitakatwa moja kwa moja na benki zao. Kutokana na mabadiliko hayo ya sheria, benki zitalazimika kujua madhehebu ya wateja wao.
Pamoja na masuala ya sadaka, masuala mengine yanayosababishawatu kujitoa ni ndoa ambapo imeelezwa wengi wa wanandoa walioachana wameenda kuoa au kuolewa kwingine, na wanajitoa wakihofia adhabu ya kufungiwa kiimani.
Pamoja na waumini kupungua makanisa hayo yamekuwa yakiingiza fedha nyingi za kanisa. Mwaka jana Kanisa Katoliki lilikusanya euro bilioni 5.5 (Sh trilioni 11.5) wakati makanisa ya Kiprotestanti yalikusanya euro bilioni 4.8 (Sh trilioni 10).