Klabu ya Arsenal iliyopo kaskazini mwa jiji la London imeanza mkakati wa kujikita katika kutafuta ubia na kampuni Tanzania kwa lengo la kujitangaza na kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii.
Katika ziara ya Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Mheshimiwa Peter Kallaghe aliyoifanya jana katika Uwanja wa Emirates, na kufuatiwa na mazungumzo rasmi na maofisa wa Klabu ya Arsenal, maofisa hao walieleza kutambua umuhimu wa Tanzania katika kukua kwa Arsenal.
Ofisa Miradi ya Jamii, Samir Singh alimweleza balozi baadhi ya takwimu juu ya wapenzi wa Arsenal walioko Tanzania, akisema kuwa mtandao wa www.arsenal.com unasomwa na watu zaidi ya milioni mbili kutoka Tanzania, huku wakirudia kuutembelea zaidi ya mara laki saba; kwenye face book wanafuatwa na watu zaidi ya 120,000.
Arsenal wamekuwa wakitoa msaada na makocha kwa mradi wa Tanzania Street Children ulioko Mwanza kwa karibu miaka minne sasa, ambapo kupitia mradi huu watoto zaidi 1,280 wamenufaika. Arsenal wamesema wangependa kuwa na ushirikiano na kampuni mbalimbali huko nyumbani ili kusaidiana katika kuinua michezo na kutambua vipaji vya wanamichezo.
Naye Ofisa Masoko wa Arsenal, Daniel Willey, alisisitiza umuhimu wa wanachama na wapenzi wa Arsenal kujisajili na kuwa na uongozi imara utakaotambuliwa na klabu na hivyo kutoa fursa mbalimbali kwa umoja huo wa wapenzi wa Arsenal Tanzania.
“Umoja wa wanachama unaotambuliwa kwa hivi sasa ni ule wa Kasulu, Kigoma, ambapo kumbukumbu zetu zinaonesha kuna wapenzi 150,000, lakini tuna imani wapo wengi zaidi, tunataka tufanye nao kazi, nitaenda Tanzania hivi karibuni, nitapenda kuonana nao Dar, sitakuwa na nafasi ya kwenda nje ya Dar kwa sasa,” alisema Willey.
Kwa upande wake Balozi Kallaghe, ambaye si mpenzi wa Arsenal, alisema hiyo ni fursa muhimu sana kwa wapenzi na mashabiki wa Arsenal kuchangamkia, na kuwataka kujisajili na kuwa na viongozi wanaotambulika.
“Unajua kubishana bishana masuala ya mpira bila kuwa na kadi ua uanachama kumepitwa na wakati, inapendeza upotumia pesa kidogo, kwa kuvaa fulana original ya timu yako,” alisema Balozi na kuwawataka wanachama hao kuisaidia klabu yao, kuwaunganisha na kampuni kama benki, viwanda vya bia na kampuni za simu.
Balozi Kallaghe alisema hiyo italeta changamoto itakayopelekea timu ya Arsenal kwenda Tanzania siku moja, ambapo Willey alionesha hamu kubwa sana ya kufanya mazungumzo na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kuona jinsi gani wanaweza kushirikiana.
“Mna vivutio vikubwa sana vya utalii; Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Manyara - haya ni maeneo ambayo tungependa kuyafanyia mazungumzo.
“Tunafahamu kuwa Rais Kikwete ni mpenzi sana wa michezo, na hasa soka, tunamkaribisha sana, japo hatujui yeye ni shabiki wa timu gani hapa England,” alisema Willey.
Balozi Kallaghe aliwashukuru Arsenal na kuahidi kutoa msaada pale itakapobidi, na kuwataka wasisite kumwona wakati wowote, na aliwashukuru kwa mwaliko kwa Rais Jakaya Kikwete kutembelea Emirates wakati wowote atakapo kuwa London.
Kazi kwenu sasa, mashabiki wa Arsenal, kutaneni, chaguaneni, mchangamkie fursa.
Source: Tanzania Sports