MAJAJI WATATU KUAMUA HATMA YA BUNGE LA KATIBA

JOPO la Majaji watatu linatarajia kusikiliza ombi kwa Mahakama itoe amri ya kusimamisha Bunge Maalumu la Katiba lililofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Said Kubenea katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Jopo litakalosikiliza ombi hilo linaongozwa na Jaji Augustine Mwarija. Wengine ni Jaji Dk Fauz Twaib na Jaji Aloysius Mujulizi lakini bado halijapangiwa tarehe yakusikilizwa.

Kubenea aliwasilisha ombi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala, akiomba Bunge hilo lisimamishwe hadi Mahakama itakapotoa tafsiri sahihi ya Bunge hilo kuhusu mamlaka iliyonayo na kama ni sahihi kwenda kinyume na Rasimu.

Katika ombi hilo, Kubenea anaiomba Mahakama itoe amri hiyo wakati wakisubiri uamuzi wa Mahakama kuhusu tafsiri sahihi kama Bunge hilo linaweza kwenda kinyume na Rasimu pia tafsiri kuhusu mamlaka ya Bunge hilo.

Aidha anaomba Mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 25(1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi ambacho kinaeleza mamlaka ya Bunge hilo.

Ombi hilo lililowasilishwa chini ya hati ya dharura limeungwa mkono na hati ya kiapo ya Kubenea ambapo anaeleza, Desemba Mosi, mwaka 2011, Bunge la Tanzania lilipitisha mabadiliko ya Katiba na kuanza maandalizi ya kupata Katiba mpya.

Hati hiyo inadai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa ajili ya kusimamia mchakato huo, ambapo Rais alitoa maelekezo kwaTume hiyo kukusanya maoni kwa wananchi kwa ajili ya kuandaa Rasimu ya Katiba mpya.

Kwa mujibu wa hati hiyo, Tume ilianza kutekeleza kazi hiyo kwa kukusanya maoni kwa wananchi kupitia mikutano na njia nyingine ikiwemo Mabaraza ya Katiba katikawilaya zote ambapo wananchi 33,537 walitoa maoni.

Tume iliandaa Rasimu ya pili ya Katiba na Desemba 8, 2013, iliikabidhi kwa Rais ambapo Rais kwa mamlaka yake alielekeza Bunge Maalumu kujadili Rasimu hiyo.

Anadai baada ya kuanza kwa Bungehilo wajumbe walitofautiana kutokana na kuingizwa kwa hoja ambazo hazipo kwenye Rasimu ndipo wajumbe wengine ambao ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakatoka bungeni kwa madai Rasimu hiyo haiwezi kufanyiwa marekebisho kama wajumbe walivyokuwa wanadai.

Chanzo: Habari leo