Amesema kwa hali inavyokwenda sasa, mapendekezo ya upande mmoja wa chama tawala ndiyo yanayopita na kuongeza: "Tungekuwepo wote ndani ya Bunge hili, lisingewezekana kwa sababu tungepinga kwa nguvu zaidina hata kuhakikisha Bunge haliendelei."
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Arfi alisema kuondoka kwa Ukawa ndani ya Bunge, ni sawa na nyani aliyekabidhiwa shamba la mahindi lisilo na mlinzi.
Alipoulizwa kama wajumbe wa kuteuliwa wa Kundi 201, wangeweza kusaidia kutetea baadhi ya hoja za Ukawa, alisema wajumbe wa kundi hilo wanaangalia maslahi ya makundi yao zaidi na ya wananchi kwa ujumla.
Pamoja na kutokuwepo nguvu ya ajenda za Ukawa, Arfi alikiri kuwepo kwa mabadiliko mazuri yaliyofanyika katika Rasimu ya Pili ya Katiba mpya, yatakayo nufaisha wananchi hasa wakulima, wafugaji na wavuni.
Arfi, ambaye amejitapa hajutii uamuzi wake wa kushiriki Bunge hilo, akipingana na wajumbe wenzake wa Ukawa, alitaja mazuri hayo kuwa ni pamoja na haki za wakulima, wafugaji na wavuvi kumiliki ardhi, haki ya hifadhi ya jamii, haki ya makazi na haki ya afya, chakula, maji safi na salama.
Hata hivyo, Arfi alidai amepanga kwenda mahakamani ili kupata ufafanuzi juu ya alichoita Bunge hilo kuachana na rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba.
Amedai kuwa kinachofanyika sasa ni kuandika rasimu nyingine ili iendane na muundo wa serikali mbili ambao ndio CCM wanaoutaka, kazi ambayo imekuwa rahisi kwa sababu hakuna upinzani wa kutosha kuzuia.
Hata hivyo, tayari Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alishatoa ufafanuzi kuwa msingi wamajadiliano yote tangu Bunge hilo limeanza, ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na hakuna rasimu nyingine inayojadiliwa isipokuwa hiyo ya Tume."Maana ya rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza … anayekabidhiwa rasimu, anayo hakina mamlaka ya kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu.
"Itakuwa ni jambo la ajabu na lisilona mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili rasimu, ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa," alisema Sitta.
Hata hivyo, Arfi alisema kutokana na mwandishi wa habari Said Kubenea kupitia mwanasheria wake, Peter Kibatala kufungua kesi Mahakama Kuu kutaka mahakama kuzuia kuendelea kwa Bunge la Maalumu la Katiba, anasubiri ushauri wa wanasheria wake kuhusu azma yake ya kufungua kesi hiyo.
Kuhusu Muungano, Arfi alisema kwa sasa wajumbe wanajadili namna ya kuboresha Muungano kwa kupunguza kero zake, ikiwemo kuanzishwa kwa Makamu wa Rais watatu; wa kwanza ambaye atatokana na Mgombea Mwenza, wa pili Rais wa Zanzibar na wa tatu Waziri Mkuu.
Alitaja jambo jingine la kuboresha Muungano kwa kuondoa kero kuwani kuanzishwa kwa mabunge matatu ya Jamhuri, Zanzibar na Tanganyika.
Kwa sasa Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na vikao vya kamati yakupitia rasimu ya Katiba na kesho kutwa kamati hizo zinatarajiwa kukamilisha kazi zao kupisha kamati ya uandishi chini ya Mwenyekiti Andrew Chenge kuandaa maoni ya kamati zote na Septemba 2, mwaka huu majadiliano yataendelea ndani ya Bunge maalumu kwa ajili ya utungaji wa Katiba mpya.
Chanzo: Habari Leo