MVIETNAM ADAKWA NA KUCHA NA MENO YA SIMBA

RAIA wa Vietnam, Dong Van (47) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa na meno 65 na kucha 447 za simba zote zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 189.

Kamanda wa Polisi Makao Makuu ya Viwanja vya Ndege, Hamisi Seleman alisema Van alikamatwa juzi saa 10 jioni akijiandaa kusafiri kwa ndege ya Shirika la Qatar kwenda Vietnam.

Alisema Polisi ilimkamata raia huyo wa nje mwenye hati ya kusafiria No.B 9306216 iliyotolewaVietnam, akiwa katika eneo la kuondokea abiria.

Baada ya kupekuliwa, inadaiwa alikutwa akiwa amehifadhi nyara hizo kwenye pakiti saba za kahawa na moja ya mchele aina ya 'Pure Basmati'.

Inadaiwa alichanganya na pakiti zingine 15 za vyakula mbalimbali.

"Baada ya kupekuliwa raia huyo alipatikana na meno 65 na kucha 447 za simba akiwa amevihifadhi katika hali ya umaridadi katika begilake la nguo ambapo ndani yake pia kulikutwa suruali mbili," alisema Selemani.

Aidha alisema uchunguzi wa suala hilo unaendelea ukihusisha vyombo mbalimbali vya usalama pamoja na watu kutoka Idara ya Maliasili kubaini mahali alipotoa nyara hizo.

Kulingana na tathmini iliyofanywa, inaonesha simba 21 wameuawa. Kwa mujibu wa Kamanda, mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuandaa mashitaka kabla ya kuwasilisha jalada la kesi yake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DPP).

"Tunawaomba Watanzania kuwa makini katika suala zima la ulinzi wa maliasili kwa kuwa sasa inaonekana ujangili haufanyiki kwa tembo peke yake bali hata kwa wanyama wakali kama simba ambao hapo awali hatukuwahi kuusikia," alisisitiza Selemani.

Pi alitaka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa pamoja waweze kuzuia uhalifu unaofanywa kupitia maeneo mbalimbali ya mipaka.