BARAZA LA KIISLAMU WAMUUNGA MWIGULU MKONO

Baraza la Maadili la Kiislamu nchini (BAMAKITA), limeunga mkono kauli iliyotolewa na Mbunge wa Iramba Magharibi, mkoani Singida, Bw. Mwingulu Nchemba kutaka vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, viahirishwe ili kuokoa fedha za walipakodi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa baraza hilo, Shekhe Athuman Mkambaku, alisema kauli ya Bw. Nchemba inaonesha ni mzalendo halisi anayelipenda Taifa lake.

Alisema hivi karibuni, Bw. Nchemba alishauri Bunge hilo liahirishwe kwani wajumbe waliopo hawawezi kuwapatia Watanzania Katiba Mpya kutokana na theluthi mbili inayotakiwa kwa mujibu wa sheria, haiwezi kupatikana kwa sababu baadhi ya wajumbe kutoka upinzani hawashiriki vikao vya Bunge hilo.

“Kuendelea kuwalipa posho wajumbe wa bunge hili ni matumizi mabaya ya fedha za umma…Nchemba ameonesha ukomavu wa kisiasa na manenoyake hayapaswi kupingwa wala kupuuzwa bali aungwe mkono na kupongezwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, baraza hilo linapinga vikali kitendo cha baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuendelea kususia vikao wakiamini pengine wanatumiwa na kundi la watu wasiotaka Katiba Mpya ipatikane.

“Hoja za UKAWA zilizowafanya wagomee vikao hivyo hazina mashiko kwani wao wanataka rasimu ipite kama ilivyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba…kama madai yao ni sahihi, kwa nini waende bungeni kuchukua posho tu?” alihoji.

Alisema lazima wajumbe wa Bunge hilo wabadili baadhi ya vifungu, waongeze na kuviboresha ndio maana ya vikao.

Shekhe Mkambaku wajumbe kutoka umoja huo hawapaswi kugoma kwa hofu kwamba, Katiba Mpya itatengenezwa kulingana na matakwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na wingi wao bali watambue kuwa, chama hicho si waamuzi wa mwisho kwani mwisho wa siku rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi ambao ndio waamuzi wa mwisho.

“Kama rasimu hii itatoka kinyume na tulivyopendekeza, wananchi wataikataa, hivyo UKAWA wasijipe kazi ambayo siyao…kazi hiyo waiache kwa wananchi waitolee majibu kwa kupiga kura ya kuikataa au kuikubali,” alisema.

Baraza hilo pia limewapinga watu wanaomshambulia Rais wa Jakaya Kikwete wakidai amevuruga mchakato huo kutokana na hotuba yake alipolihutubia Bunge la Katiba kwani alichokisema ni ushauri tu.

“Kama Kiongozi Mkuu wa nchi, bado ana fursa ya kushauri si lazima wajumbe kufuata maoniyake ndio maana baada ya hotuba yake, vikao viliendelea,” alisema Shekhe Mkambaku