KITUO CHA POLISI CHACHOMWA MOTO

WATU tisa w a n a o d a i wa ni waendesha bodaboda (pikipiki), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kuchoma moto Kituo cha Polisi Mkuyuni na kusababisha majeruhi kwa watu wawili, akiwemo askari polisi na kumtorosha mtuhumiwa aliyekuwa anashikiliwa kituoni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema tukio hilo lilitokea Agosti 3, mwaka huu, saa11:45 alfajiri katika Tarafa ya Mkuyuni wilayani Morogoro.

Aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo ni askari mwenye namba G 7012, PC Edson ambaye alitibiwa na kuruhusiwa, Hamad Kimolo(26), mwendesha pikipiki na mkazi wa Kinole ambaye alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

Kamanda Paulo aliwataja waliokamatwa ni Valentino John (18), Jafari Hussein (20),Kulwa Kesi (32) na Rashidi Iddi(22), wote wakiwa ni wakazi wa eneo la Kinole, Mashaka Degeresa (20) na Juma Ally(19), wote wakiwa ni wakazi wa Kijiji cha Kalundwe.

Aliwataja wengine ni Hamisi Juma mkazi wa Dar es Salaam, Sheuna Hassan na Bilali Tamimu (19), wote wakiwa ni wakazi wa Kinole.

Kamanda alisema siku ya tukio askari wakiwa kazini walimkamata mwendesha pikipiki, Ally Musa (19), mkazi wa Kinole akiwa amepakia abiria watatu kwenye pikipiki namba T 162 CSC aina ya Fecon, ambapo mtuhumiwa alikataa kwenda polisi na kutelekeza pikipiki yake.

Paulo alisema baada ya kuondoka, polisi waliichukua pikipiki hiyo na kumfungulia kosa la kupakia watu watatu(mshkaki).

Alisema saa 12: 45 asubuhi waendesha bodaboda zaidi ya 30 walivamia kituo hicho, huku wakiwa na marungu, matofali na fimbo na kuanza kufanya vurugu wakitaka kumtoa mwenzao aliyekamatwa na kukiweka kituo hicho katika hali ya hatari, ambapo walifanikiwa kumtoa mwenzao na kuondoka na pikipiki yake.

Kamanda aliongeza kuwa, bodaboda hao waliamua kuchoma moto kituo hichona kumjeruhi askari namba G7012.

Aliwataka raia kutambua kuwa, polisi haihitaji uhuni katika maisha ya binadamu, bali inahitaji kuheshimu sheria ili waweze kuishi katika mazingira ya amani.