Gazeti hili limethibitisha kwamba Pinda tayari ameamua kujitosa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ambayo tayari inawaniwa na makada wa chama hicho wasiopungua 15 na baadhi yao wameishatangaza nia zao kwa nyakati tofauti.
Habari kutoka ndani ya CCM zinasema uamuzi wa Pinda kuwania urais mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani, umesababisha kiwewe miongoni mwa wagombea na kunakifanya kinyang'anyiro hicho kuchukua sura mpya.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia gazeti hili siku chache zilizopita mjini Dodoma kuwa: "Na sisi tumesikia kwamba PM (Waziri Mkuu) amejitosa na kama ni kweli atawasumbua wagombea wengi kutokana na rekodi yake hasa katika uadilifu."
"Yeye (Pinda) ana faida tatu kubwa; kwanza hana kundi katika chama, anaelewana na watu wote, pili nafasi yake ya uwaziri mkuu inampa nafasi ya kufahamika kwa watu wengi na tatu rekodi yake ya uadilifu, hana kashfa za ovyoovyo, labda kama ataharibu dakika hizi zamwisho," alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania uraia kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wakekatika nafasi hiyo, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wegine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.
Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba, Asha-Rose Migiro.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na aliyewahikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Balozi Ali Karume.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema wingi wa wanaojitokeza kutaka kuwania urais ni njia ya kuunda mtandao utakaomwezesha mtu fulani au mmoja kunyakua tiketi hiyo.
"Watu wanapiga kampeni katika harambee kwa njia ya kutengeneza mitandao, kwani ukifika wakati wa chama kumpitisha mgombea, asiposhinda ataibuka na kuwaeleza kuwa mnaoniunga mkono mimi muungeni fulani," alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kujitokeza kwa idadi kubwaya wanaowania nafasi ya urais, kutatoa fursa ya wananchi kutambua udhaifu wa kila mmoja jambo litakalowezesha kupatikana kwa mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya chama hicho.
"Wakiwa wengi, kila mmoja atataka kuonyesha umahiri wake na sisi ambao ni wananchi watawaliwa tutaweza kutambua upungufu wa kila mmoja, jambo litakalosaidia kupatikana kwa mtu sahihi," alisema Mbunda
Kambi ya Pinda
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa mjini Dodoma ambako vikao vya Bunge Maalumu vinaendelea umebaini kuwa kambi ya Pinda inaongozwa na Mwenyekitiwa Mamlaka za Mitaa Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
Inadhaniwa kuwa Dk Masaburi atatumia ushawishi wake kwa viongozi wa mamlaka za miji na wilaya zinazoongozwa na wenyeviti wa halmashauri na mameya wa miji, manispaa na majiji kumuunga mkono mgombea huyo ambaye piahivi sasa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziko chini ya ofisi yake.Wiki hii kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini Dodoma likijaribu kutafuta kuungwa mkono na makada viongozi wa CCM ambao walikuwa wakishiriki kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho pamojana wale walioko katika Bunge Maalumu. Habari zinasema mbali na Dodoma, tayari kambi hiyo imeshafanya vikao kadhaa jijini Dares Salaam na Visiwani Zanzibar lengo likiwa ni kutafuta kuungwa mkono na makada wa CCM katika sehemu hizo. Hivi sasa nguvu za Pinda zinaelekezwa katika mikoa mingine nchini kwa lengo hilohilo. Kutokana na kasi ya kambi yake, wafuasi wa baadhi ya wagombea wameanza kufuatilia mwenendo wao kwa lengo la kukusanya ushahidi wa kile wanachokiita 'rafu' zinazochezwa ili kupata ushahidi unaoweza kutumika dhidi ya mgombea huyo wakati mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM utakapoanza mapema mwakani.
Itakumbukwa kwamba makada watano wa chama hicho ambao ni Lowassa, Membe, Makamba, Wassira na Ngeleja wanatumikia adhabu na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema hivi sasa ni mapema mno kusema ni lini mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama hicho utaanza na kwamba wakati mwafaka ukiwadia wananchi watafahamishwa.
Uwezo, udhaifu wake
Hata hivyo wakosoaji wake wanasema Pinda akiwa Waziri Mkuuhana cha kujivunia na kwamba amekuwa mzito kufanya uamuzi mara kadhaa kiasi cha kusababisha baadhi ya mambo muhimu ya nchi kukwama na kwamba kwa maana hiyo hastahili kuwa rais.
"Ni kitu gani ambacho nchi inakikumbuka kuhusu huyu bwana ambacho alikifanya katika miaka yake ya uwaziri mkuu, kama alikuwa kwenye nafasi kubwa kiasi hicho na hakuna alichofanya, atawezaje kumudu madaraka ya mkuu wa nchi?" alihoji mmoja wa makada wakongwe wa CCM.
Waziri mmoja wa sasa (jina tumelihifadhi), alisema Pinda hana uwezo wa kuongoza nchi, kwani wao wakiwa mawaziri ameshindwa kuwasaidia katika kero mbalimbali walizokuwa wakimfikishia kama kiongozi wao.
"Muulize waziri yeyote kuhusu uwezo wa jamaa, kila kukicha tunampelekea mambo tunayokutana nayo, lakini hakuna kinachowezekana kwake, atakwambia subiri leo, subiri keshona hatimaye jambo linaishia hivyohivyo," alisema.
Kwa upande mwingine, watetezi wake wanasema Pinda wanayemnadi ni yule aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi) kiasi cha kuonekana anafaa kuwa Waziri Mkuu.
Wanasema kushindwa kwake kufanya kazi ipasavyo ni matokeo ya sababu zilizomfanya mtangulizi wake, Lowassa kung'oka katika nafasi yake.
Chanzo: Mwananchi