Pia mahakama hiyo imeamuru vyombo vya dola kuacha kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani kusikiliza kesi zake, na kushauri kama wana wasiwasi nao, waweke mashine za ukaguzi katika mlango wa kuingilia mahakamani hapo.
Mwenendo huo wa Sheikh Ponda ulihojiwa mahakamani hapo na Jaji Augustine Shangwa juzi kabla ya kuanza kusikiliza rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia hatiani katika kesi ya jinai, mwaka 2012.
"Sheikh Ponda, sijui ni kwa nini unakesi nyingi kiasi hiki. Kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi (Kisutu) una kesi, Mahakama Kuu una kesi. Nani yuko nyuma ya kesi zako? Je! Serikali inakuchukia?" alihoji Jaji Shangwa.Licha kumhoji Sheikh Ponda maswali hayo, alimweleza kuwa kama atakuwa na jambo la kuzungumza, atampa nafasi siku nyingine rufaa yake itakapotajwa. Pia Jaji Shangwa alimshauri apunguze mapambano.
"Ikiwezekana uyapunguze (mapambano) maana dunia hii si yakupambana nayo," alisema Jaji Shangwa na kusisitiza kuwa lazima ajiulize kwa nini ana kesi nyingi.
Jaji Shangwa aliendelea kusema: "Jambo likitokea Zanzibar, wewe umo; likitokea Morogoro umo; likitokea Dar es Salaam umo. Bahati mbaya kuna kikundi cha Uamsho kinadaiwa kulipua mabomu na kuua watu, nasikia na wewe unatajwa kuhusishwa."Hata hivyo baadaye Jaji Shangwa alimuuliza Ponda kama ana la kueleza kuhusu wingi wa kesi zinazomkabili.
Sheikh Ponda alidai kuwa kesi hizo ni mzigo anaotwisha kutokana na kutetea kile alichokiita masilahi, huku akijitetea kuhusu hukumu ya kesi iliyomtia hatiani ambayo amekata rufaa kuipinga, akieleza kuwa eneo analodai kuvamia ni mali ya Waislamu.
Hata hivyo, Jaji Shangwa alimkata kauli akisema anayoyaeleza yanapaswa kusemwa na mawakili wake katika rufaa hiyo kama alikuwa na hatia au la. Alimtaka aeleze ni kwanini anakabiliwa na kesi nyingi.
Hata hivyo, wakili wake Juma Nassoro alisimama na kuieleza Mahakama kuwa si kwamba mteja wake ana kesi nyingi, bali anakabiliwa na kesi mbili tu moja iliyokuwa Mahakama ya Kisutu ambayo ndiyo wameikatia rufaa na ile iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Awali, wakati akivipiga 'stop' vyombo vya dola kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani, Jaji Shangwa alisema: "Huyu Sheikh Ponda ana wafuasi wengi, wanahitaji kuja kusikiliza kesi yake. Vyombo husika visiwazuie, waacheni waje wasikilize kesi ya Sheikh wao." Pia aliwaonya wafuasi hao kuacha mapambano na vyombo vya dola.