WANANDUGU WATANO WA FAMILIA MOJA WATEMBELEA MIKONO NA MIGUU

FAMILIA moja ya Uturuki inawapasua kichwa wanasayansi, kutokana na wanandugu watano kutokuwa na uwezo wa kutembea kama binadamu, na badala yake wanatembea mithili ya wanyama, wakitumia miguu na mikono.

Hata hivyo, katika uchunguzi wao waawali, wanasayansi hao wameeleza kuwa, hali iliyowakumba wanandugu hao haina uhusiano na mabadiliko ya binadamu, kwamba wanaanza kurudi katika zama za mwanzo ambako inaelezwa walitembea kwa miguu minne, wengine wakisema walianza kuwa nyani.

Ndugu hao watano ambao ni kaka na madada, wakiwa na umri wa miaka 16 hadi 34 kutoka kijiji cha Jimbo la Hatay, kusini mwa Uturuki,walianza kufuatiliwa na wanasayansi mwaka 2005 baada ya kugundulika na watu kutoka nje ya kijiji chao.

Wanatembea kwa mtindo wa kutambaa kama dubu kwa mikono na wanaweza kusimama tu kwa muda mfupi, kwa magoti yao.

Utafiti wa hivi karibuni ulifanywa na wanasayansi, Shapiro, Whitney Cole,Scott Robinson na Karen Adolph, wote wa Chuo Kikuu cha New York, Jessica Young wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Northeast Ohio na David Raichlen, wa Chuo Kikuu cha Arizona.

"Lakini hawa hawana uhusiano na mgeuko wa binadamu kwamba baada ya kupitia hatua kadhaa za mabadiliko, sasa wanarudi katika hatua za awali, hilo halipo," mmoja wa wanasayansi hao amenukuliwa akisema.

Nadharia za awali zilidai familia ya Ulas ilikuwa ikitembea kama nyani, na kupendekeza kuwa huenda ni hatua ya kurudi nyuma kwa mabadiliko ya binadamu.

Lakini sasa, wanasayansi wa Kimarekani wamethibitisha kwa kusema wanandugu hao wanakabiliwa na kasoro isiyoonekana na hutokea mara chache.

Katika ripoti iliyochapishwa na PLOSOne, watafiti walisema familia hiyo wanatembea kwa namna tofauti kama nyani, ambao wakitembea huweka mikono upande mmoja na miguu upande mwingine wakijirudia rudia.

Walidai kutembea kwa wanandugu hao ni matokeo ya hali ya kurithi ambayo husababisha uwiano wa akili kutatizika.

"Nilikuwa na hamu ya kuweka rekodi sawa, kwa kuwa haya madai ya asili na sababu ya kutembea kama mnyama wa miguu minne imechapishwa mara kwa mara, bila kuwepo uchambuzi wa kwa nini wanatembea hivyo, na watafiti ambao si wataalamu wa namna mamalia wa hali ya juu wanavyotembea," Mtafiti Kiongozi Liza Shapiro wa Chuo Kikuu cha Texas alilieleza gazeti la The Washington Post.

"Tumeonesha wanyama wa miguu minne wanavyofanana na mtu mzima mwenye afya njema ambaye ameambiwa atembee kwa miguu minne wakati wa kufanya majaribio.

Mwaka 2005, watafiti wa Uingereza walikubali katika utafiti tofauti kuwautembeaji wa ndugu hao unatofautiana na baadhi ya mamalia wengine, ikizingatiwa wenyewe hubeba uzito wao wote kwenye viganja vya mkono na kifundo cha mkono na sio kiungio.

Hata hivyo, Mtaalamu wa Bayolojia wa Uturuki, Uner Tan awali alidai wanandugu hao, ambao pia wanaonekana kuwa wameathirika kwenye ubongo wanakabiliwa na hali inayoitwa Uner Tan Syndrome.

Alisema watu wanaokabiliwa na halihiyo hutembea kwa miguu minne na mara nyingine huzungumza kama wanyama na huwa na mtindio wa ubongo.

"Ghafla nimegundua wanatembea kwa mtindo kama nyani kama walivyokuwa wahenga wetu… nilikuwa wa kwanza kupendekeza kuwa kuna uwezekano wa hali ya binadamu kugeuka na kurudi enzi za zamani za ubinadamu," alisema.

Wandugu hao ambao wazazi wao wanatembea kawaida, mara ya kwanza walirushwa mwaka 2006 kwenye dokumentari ya BBC2, dokumentari hiyo ikiitwa The Family That Walks On All Fours.

Wakati mabinti wawili na mtoto mmoja wa kiume wamekuwa wakitembelea mikono miwili na miguu miwili, mtoto mwingine wa kiume na kike mara nyingine huweza kutembea wakiwa wamenyooka sawa, ingawa si kwa muda mrefu.

Profesa Nicholas Humphrey, ambaye aliitembelea familia hiyo mara mbili wakati wa dokumentari hiyo, alisema,
"inashangaza kama mfano wa kitu cha ajabu cha maendeleo ya binadamu. Lakini kinachovutia ni jinsia wanavyoweza kuishi katika ulimwengu wa kisasa."

Alisema alifikiri familia hiyo imerudi katika silika ya mfumo wa tabia iliyojikita ndani sana kwenye ubongo, lakini aliachwa wakati wa mageuko.

"Sidhani kama walitakiwa kuwa wanyama wanaotembelea miguu minne kutokana na jeni zao, lakini mfumo wa utengenezaji jeni zao zinawaruhusu kuwa hivyo," alisema.

Wanandugu hao watano ambao wana kaka na dada zao wengine 14 ambao hawajaathirika na hali hiyo, hutumia muda mwingi kukaa nje ya nyumba yao ya familia iliyoko kijijini. Hata hivyo, mmoja wao hutembea kijijini, kuchanganyika na kuzungumza na watu.