KAMATI ZASHAURI RAIS KUPUNGUZIWA MADARAKA

PAMOJA na Rasimu ya Katiba mpya ya Jaji Joseph Warioba kupunguza madaraka ya Rais, kamati zilizotoa taarifa ya mwenendo wake jana zimependekeza madaraka zaidi kupunguzwa.

Katika majadiliano kwenye kamati namba 10, 11 na 12, aidha imependekezwa watakaobaki kuwa wateule wa Rais ni lazima wapelekwe kuthibitishwa na Bunge au mamlaka nyingine.

Mwenyekiti wa kamati namba 12, Paul Kimiti, alisema wajumbe wengi wamejikita katika upunguzajizaidi wa madaraka ya Rais hasa katika mamlaka ya uteuzi.

Kwa kuangalia mwenendo wa majadiliano katika kamati hadi jana, inaonekana kwamba kasi ya kuchambua Rasimu ya Katiba ipo kiwango cha juu na kila Mwenyekiti aliyezungumza kuhusu akidi alisifia kutimia kwake.

Kimiti alisema wapo katika sura ya saba na wanaendelea na majadiliano na japokuwa vipengelevingi vimeshazungumzwa, wajumbe wengi wamejikita katika upunguzaji zaidi wa madaraka ya Rais.

Katika kikao hicho mjumbe wa kamati hiyo ambaye alikuwa mgonjwa kutokana na kipigo, Thomas Mgoli alisema aliomba kupiga kura kwa sababu alishiriki katika kujadili sura hizo na ilikuwa haki yake.

Alisema uamuzi huo ni tofauti na ilivyotafsiriwa kwamba ulitokana na kukosekana kwa akidi. Wakati huo huo, kamati nyingi zinaendelea kuzungumzia uraia pacha huku wakiwemo wanaopinga suala hilo.

Makamu Mwenyekiti wa kamati namba 10, Salmin Awadh Salmin alisema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba wameshaanza kupiga kura kwa kamati 2,3 na 4 huku wakiendelea na majadiliano katika sura namba 5.

Hata hivyo alisema jana waliacha majadiliano ya sura hiyo na kuingia sura namba saba ambapo wao watawasilisha maoni ya walio wengi na wachache kutokana na jinsi mambo yalivyojiri katika majadiliano.

Alisema katika kamati yake kulikuwa na mijadala mirefu hasa kwenye mazingira yanayosababisha haki, kiasi cha kuamini kwamba kuna hitajika sura nyingine.

Alisema sura hiyo itajikita zaidi katika haki za wakulima, wavuvi na wafugaji; pia haki za kimakundi kama wanawake.
"Tutapendekeza sura nyingine ili kila mtu apate haki zake..." alisema Salmin.

Aidha alisema katika kamati yake Sura ya 7 imekuwa na mvutano mkubwa na kulazimika kuweka viporo ibara 72 na 73 zinazojadili mamlaka.