WINGU ZITO KURA YA MAONI YA KATIBA

Mchakato wa Katiba Mpya, hatua ya Kura ya Maoni umegubikwa na wingu zito kutokana na kuibuka utata na ukiukwaji wa sheria.

Wakati hali ikiwa hivyo, jana Ofisi ya Rais, Ikulu iliibuka na kutoa ufafanuzi kuwa Rais Jakaya Kikwete hajakiuka Sheriaya Kura ya Maoni kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni.

Juzi, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema kuna mwingiliano unaoleta mkanganyiko katika mchakato wa kuboresha Daftari la Wapiga kura na Sheria ya Kura ya Maoni.

Jaji Warioba alisema sheria inaweka utaratibu maalumu wa mchakato wa kura ya maoni ambao hautaendana na ratiba ya uandikishwaji katika daftari hilo.

Alisema Sheria Kura ya Maoni Na. 3 ya mwaka 2014 inasema wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kura ya maoni kwa miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni lakini hadi sasa, hakuna ratiba inayoeleweka, jambo ambalo alisema linaleta mwingiliano.

"Hii ni Januari, kama watafuata sheria na kuanza kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni Juni ina maana kura itapigwa Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa zimepamba moto," alisema.

Mkanganyiko huo umeibua maswali kutoka kwa wanasiasa, wanasheria na wanaharakati wakisema hali hiyo inaweza kuathiri kura ya maoni ambayo imepangwa kufanyika Aprili 30.

Kwa upande mwingine, Mbungewa Ubungo (Chadema), John Mnyika amewasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili ijadiliwe na kutoa maazimio kutokana na kutokuwapo uwezekano wa kufanyika kura ya maoni Aprili 30.


Kauli ya Ikulu

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu alisema katika mchakato huo, Rais Kikwete alifuata taratibu zote zilizopo katika sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na kutangaza katika Gazeti la Serikali tarehe ya kuanza kwa upigaji wa kura hiyo.

"Sheria inasema Rais atatangaza tarehe hiyo wiki mbili baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa na alitekeleza hilo na baadaye alieleza jinsi ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itakavyosimamia suala hilo," alisema.

Katika hotuba yake kwa wazee wa Dodoma Novemba mwaka jana, Rais Kikwete alisema, "Ninaomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka ya Sheria ya Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itapigwa, lini kampeni zitafanyika na lini wadau watatoa elimu, naomba tuwe na subira. Tukizingatia sheria hii hakuna ugomvi," alisema Rais Kikwete.

Alisema licha ya sheria kuruhusu kampeni kufanyika ndani ya siku 60 kabla ya kura za maoni, kwa mamlaka yake yakiuongozi, kura na kampeni vitafanyika ndani ya siku 30 tu.

"Kampeni zitaanza Machi 30 na kumalizika Aprili 29 ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura ya maoni. Muda huo ndiyo utakuwa wa kufanya hivyo," alisema Rais Kikwete.


Hoja ya Mnyika

Mbunge huyo wa Ubungo alisema mpaka sasa Nec ilitakiwa iwe imetangaza ratiba ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura lakini haijafanya hivyo, pia Sheria ya Kura ya Maoni inasema kabla yakufanyika kwa kura hiyo kutakuwa na miezi miwili ya kutoa elimu ambayo haitatosha.

"Hakuna haja ya kuuharakisha mchakato huu kwani unaweza kufanyika baada ya Uchaguzi Mkuu, unajua baada ya mjadala,Bunge litakuja na maazimio ambayo yatakuwa suluhisho la mchakato huu unaoharakishwa na chama tawala."

Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara) alisema; "Hata Rais Kikwete anatakiwa kutengua kauli yake kuwa kura ya maoni itafanyika Aprili 30 kwani hali ilivyo hakuna uwezekano wa kufanyika."

Akifafanua baadaye, Mnyika alisema anazo taarifa za ndani ya Nec kuwa vifaa vinavyotakiwa havijakamilika na Serikali haijatoa fedha za kutosha na ndiyo sababu haijatangaza ratiba ya uboreshaji daftari.

Alisema kwa muda uliotangazwa kati ya Februari 15 na Machi 15 kufanya uboreshaji huo, hauwezekani kwa kuwa hakutakuwa na muda wa kuhakiki daftari hilo kabla ya kura ya maoni.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Julius Malaba alipoulizwa alisema atazungumzia suala hilo leo.


Msimamo wa Makamba

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba akizungumzia suala hilo alisema; "Kama tukijipanga vizuri kwa Tume na Serikali tunaweza kufanikiwa na hakuna sababu ya kuharakisha kitu.Katiba itapata uhalali kama mchakato wa kuipitisha utakuwahalali."


Wanasheria waponda

Wanasheria mbalimbali wamesema Sheria ya Kura ya Maoni 2013, ina upungufu mkubwa na inaweza kuathiri Wazanzibari wengi kutoshiriki katika upigaji kura ya maoni.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema miongoni mwa udhaifu wa sheria ni pamoja na mwingiliano wa Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 na Sheria ya Kura ya Maoni ya 2010 ya Zanzibar.

Alisema katika utaratibu wa kupatikana wapiga kura, kila upande wa Muungano utatumia daftari lake kuwasajili.

"Kwa upande wa Bara kuna daftari linaloandaliwa lakini kwa upande wa sheria ya kura ya Zanzibar ya 2010, ili Mzanzibari atambuliwe na kusajiliwa kwenye daftari la wapigakura ni lazima awe ni mkazi aliyeishi Zanzibar kwa miaka isiyopungua mitatu," alisema na kuongeza:
"Kutokana na sheria hiyo, kuna Wazanzibari wengi ambao wanaishi Bara kwa muda mrefu ambao hawatakuwa na sifa za kuandikishwa kwenye daftari hilo. Nilitoa hoja hiyo bungeni lakini wabunge wa CCM walikataa kwa kuhofia Wazanzibari wakipata nafasi ya kuandikishwa, wataikataa Katiba hiyo.

"Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema mbali ya udhaifu huo alioutaja Lissu, mpaka sasa hakuna dalili zozote za kufanyika kura ya maoni kutokana na muda uliobakia.

Alisema katika tathmini yake, hatua zote za maandalizi ya tukio hilo zitakamilika Mei, kinyume na tarehe iliyopangwa na Serikali.

"Mpaka sasa haijulikani daftari kama litakamilika kutokana na muda uliopangwa na ukosefu wa fedha kwa Tume, Pili hatua ya kampeni na maandalizi mengine yanaweza kukamilika Mei," alisema Kibamba.

Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema Nec haitaweza kukamilisha uandikishaji kabla ya Aprili 30.

"Tulikutana kwenye kikao cha TDC ambacho kilihusisha viongozi wote wa vyama na Jaji Lubuva alikuwapo, aliahidi kutimiza ahadi hiyo lakini mpaka sasa hajapata fedha za kununulia vifaa vingine vilivyobakia," alisema Nyambabe.

Mashine za BVR zinazohitajika ni 7,750 na zilizopatikana ni 250 tu, vituo vya kuandikishia viko 40,500 nchi nzima na Watanzania wanaotarajiwa ni milioni 23, kwa hivyo hakuna uwezekano wa kufanikiwa shughuli hiyo kwa mwaka huu."

Chanzo: Mwananchi