MGANGA WA KIENYEJI ATUPWA JELA MIAKA SABA

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu mganga wa kienyeji, Yahaya Michael (34) kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikanana hatia ya wizi wa gari kwa njia ya udanganyifu.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma alisema kwamba kutokana na mshitakiwa kutoroka chini ya dhamana, atatumikia kifungo hicho mara baada ya kukamatwa.

Alisema kwa kuwa mshitakiwa alitoroka chini ya dhamana, mahakama hiyo ilisikiliza shauri hilo kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai.

Alisema upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watatu ambao waliithibitishia mahakama bila ya kuacha shaka.

Ilidaiwa kwamba gari hilo lilipatikana maeneo ya Urambo Tabora huku mshitakiwa huyo akiwa analiendesha.