ESCROW YABURUZA WAWILI MAHAKAMANI

WATUMISHI wawili waandamizi wa Serikali wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kupokea zaidi ya Shmilioni 485 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Washitakiwa hao ni Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma na Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Theophil Bwakea.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashitaka mbele ya mahakimu wawili tofauti.

Awali, Bwakea alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi akidaiwa kupokea rushwa ya Sh milioni 161,700,000 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya VIP Engineering and Marketing ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai alidai, Februari 12, 2014 katikajengo la Benki ya Mkombozi Ilala, alijipatia fedha hizo kupitia akaunti namba 00410102643901 akiwa kama mjumbe aliyeandaa sera kuruhusu sekta binafsi kuzalisha na kuliuzia umeme Shirika la Umeme (Tanesco).

Mujunangoma alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru na kusomewa mashitaka ya kupokea Shmilioni 323,400,000 baada ya kushughulikia masuala ya kampuni ya IPTL kama mfilisi jambo ambalo linahusiana na kazi yake.

Wakili Swai alidai Februari 5, 2014 katika jengo la Benki ya Mkombozi alipokea rushwa ya fedha hizo kupitia akaunti namba 00120102602001 kutoka kwa Rugemalira. Inadaiwa fedha hizo ni sehemu ya zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hizo umekamilika na kuomba terehe nyingine kwa ajili yawashitakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washitakiwa wote wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa, ambapo Bwakea alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi serikalini waliotoa Sh milioni 25 kilammoja. Aidha, Mahakama imeamuru fedha zilizo katika akaunti ya Bwakea zisitumike hadi kesi hiyo itakapokwisha.

Mujunangoma aliwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya nusu ya fedha anazodaiwa kupokea, alikuwa na wadhamini wawili watumishi wa umma waliosaini hati ya Sh milioni 10 kila mmoja, aidha upande wa Jamhuri umetakiwa kuwasilisha ombi la kuzuia matumizi ya akaunti yenye fedha anazodaiwa kupokea.

Kesi zitatajwa Januari 29 mwaka huukwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali. Mujunangoma atafika mahakamani kesho kwa ajili ya kuwasilisha tathmini ya hati alizotoa mahakamani kama dhamana pamoja na baadhi ya nyaraka za wadhamini wake.

WanaCCM kikaangoni

Katika hatua nyingine, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow limechukua sura mpya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kuagiza hatua za kimaadili zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili katika sakata hilo.

Wanaobanwa zaidi ni wale ambao nisehemu ya vikao vya maamuzi katika chama hicho tawala. Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari mjini humo kuzungumzia yaliyojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana juzi.

Alisema Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika Januari 19, kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo.

Aliongeza kuwa, CCM imesikitishwa sana na sakata hilo linalohusishwa na uchotaji fedha zaidi ya Sh milioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyofunguliwa baada ya kuibuka kwa mgogoro wa kibiashara baina ya kampuni ya kufua umeme ya IPTL na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).

"Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na serikali, Kamati Kuu imeitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya bunge juu ya swala hilo."

Aidha, Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha. "Na Tatu, Kamati Kuu imeiagiza Kamati Ndogoya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya maamuzi vya Chama."

Sakata la Escrow, baada ya kuibua mjadala mzito bungeni, wabunge walitoka na maazimio kadhaa yaliyowasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, ikiwa ni pamoja na kutaka kuwajibishwa kwa wahusika wa sakata hilo, wakiwemo mawaziri na watendaji wengine serikalini.

Tayari Rais Kikwete ameshachukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliakim Maswi amesimamishwa kwamuda usiojulikana ili kupisha uchunguzi wakati Jaji Frederick Werema amejiuzulu wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akisema anawajibika, ingawa amekuwa akisisitiza haoni kama alifanya kosa lolote katika kushauri juu ya suala la akaunti ya Escrow.

Chanzo: Habari leo