TRENI YA MWENDO KASI YAJA

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRL) limetangaza usafiri mpya wa reli kwa kutumia treni maarufu za Delux, zitakazofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Kigoma hadi Mwanza, utakaoanza mwezi huu.

Usafiri huo wa treni utatumia saa 30 tu kufika katika mikoa hiyo na kusimama kwenye vituo vikubwa 14, kati ya vituo 54 vya treni vilivyopo; na kufanya safari zake mara moja kwa wiki kwa kupokezana kwa mikoa ya Kigoma na Mwanza.

Akitoa mada katika mkutano wa wadau, kujadili nauli za treni hiyo, Meneja Biashara wa kampuni hiyo, Charles Ndenge alisema hayo jana wakati wa mkutano wa wadau wa usafiri wa reli, kujadili nauli pendekezwa ya usafiri huo, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na majini (SUMATRA).Alisema itatumia mabehewa yenye ubora zaidi na kupunguza msongamano kwenye mabehewa huku ikitembea kwa wakati na abiria, hawataruhusiwa kusimama kwenye usafiri huo na safari za treni kwenda mikoa hiyo, zitakuwa mara tatu kwa wiki badala ya mbili.

"Pia kwenye treni hiyo kutakuwa na behewa moja zuri la huduma chakula na vinywaji pamoja na huduma ya mawasiliano za kisasa huku tukiangalia huduma yake na kuongeza," alisema.

Akizungumzia muundo wa treni hiyo ya Delux, alisema itakuwa na mabehewa 10 ya daraja la tatu, ambapo kila moja litabeba abiria 80, mabehewa manne ya daraja la pili ambayo kila moja litabeba abiria 60 wa kukaa na mabehewa sita ya kulala ya daraja la kwanza kila moja litabeba abiria 36.Alisema vichwa vimejengwa upya na kuwekewa teknolojia mpya na kutengenezwa makochi mapya.

Ndenge alisema gharama za uendeshaji ni Sh114,257,580 huku wakitegemea mapato kuwa Sh 116,259,200 huku wakitoa nauli wanayopendekeza kuelekea Kigomani Sh 77,600 kwa daraja la kwanza, Sh 44,900 daraja la pili na Sh 38,800 kwa daraja la tatu.

Aidha, alieleza kuelekea Mwanza kwa treni hiyo ni Sh 76,400 kwa daraja la kwanza, Sh 44,400 daraja la pili na Sh 38,100 kwa daraja kwanza huku mkoani Dodoma Sh 37,00 daraja la kwanza, Sh 21,400 daraja la pili na Sh 18,900 daraja la tatu.Kwa mkoa wa Tabora daraja la kwanza Sh 56,700, daraja la pili 32,900 na daraja la tatu Sh 28,600 huku wa mkoani Mwanza Sh 67,200,kwa daraja la kwanza na daraja la pili Sh.38900 na daraja la tatu Sh 33,600.

Awali, Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema nauli hizo nipendekezwa, ambazo hazijapitishwa na kwamba watatangaza viwango vya nauli siku 14 baada ya kupata maoni ya wadau mbalimbali.

Alisema usafiri huo, unatarajia kuanza katikati ya mwezi huu na kwa kuwa usafiri huo haujaanza, hakuna anayejua ubora na huduma zake, bali kutumia mapendekezo kwa wadau kuchangia.

"Usafiri huu utasaidia katika kupunguza kero ya usafiri kwa umma na kuongeza tija kwa wasafiri kusafiri kwa wakati ikiwa ni pamoja na kupunguza ajali kwa kutumia usafiri huo wa uhakika," alisema.

Wakichangia mapendekezo hayo ya nauli, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wanchi kavu na Majini (SUMATRA CCC)walitaka kuboreshwa kwa miundombinu ili kuwa na uhakika kwa usafiri huo kwani kuwa na mabehewa mapya bila miundombinu mipya ni bure.