MAKASISI WAPEWA KICHAPO

Makasisi watatu wa kanisa la Baptist nchini Guinea wamechapwa na kisha kutekwa nyara baada ya wenyeji kuwashuku kuwa maafisa wanaohamasisha jamii dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Makasisi hao, walikuwa wametembelea kijiji cha Kabac eneo la Forecariah wakilenga kufukiza dawa ya wadudu kwenye kuta za vyoo za umma na katika sehemu za kuteka maji.

Mwandishi wa BBC anasema kwamba wanakijiji hao punde tu walipowaona, waliwashuku kutaka kueneza ugonjwa wa Ebola katika eneo hilo.

Zaidi ya watu 8,600 wamefariki katika kanda ya Afrika Magharibi kutokana na ugonjwa wa Ebola.

Mapema mwezi huu, wakazi katika eneo la Forecariah walishambulia na kuwaua polisi wawili walioshukiwa kuwa na njama ya kueneza Ebola katika eneo hilo.

Makasisi hao walipewa kichapo cha Mbwa huku magari yao yakiteketezwa.

Baada ya kuwavamia makasisi hao, wakazi walikwenda katika makao ya baraza la mji na kuanza kuyashambulia.

Pia waliteketeza jumba hilo na kuwalazimisha wafanyakazi kukimbilia usalama wao.

Duru zinasema kwamba mfanyakazi mmoja wa baraza la jiji aliuawa ingawa taarifa hii haingeweza kuthibitishwa.

Watu hao walizua vurugu zaidi pale polisi walipowakamata washukiwa wa vurugu hizo.