BLATTER APATA MPINZANI MBIO ZA URAIS

Makamu wa Rais wa shirikisho la soka duniani, Mwanamfalme Ali Bin Al Hussein wa Jordan, amesema kuwa atamenyana na Sepp Blatter kuwania urais wa shirikisho hilo.

Ali Bin Al Hussein amesema atagombea urais wa shirikisho hilo katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Mei.

Sepp Blatter anawania urais wa shirikisho hilo kwa muhula wa tano.

Kwa upande wake, Ali Bin Hussein, huenda akapokea uungwaji mkono wa mashirikisho ya soka Ulaya ingawa haijabainika ikiwa ataungwa mkono na shirikisho lenye nguvu sana la soka ya Bara Asia.

Mwanamfalme huyo, amesema ni wakati sasa wa kubadilisha mambo katika shirikisho hilo hasa kutokana na kashfa nyingi ambazo zimekumba soka duniani.

Alikuwa akigusia madai ya rushwa ambayo amehusishwa nayo, bwana Blatter na kutikisa uongozi wake wa shirikisho hilo kwa miaka 17 iliyopita.

Mwanadiplomasia wa Ufaransa Jerome Champagne, pia anajiandaa kuwania uongozi huo dhidi ya wawili hao.