WATUHUMIWA WATATU WA MAUAJI WAUAWA NA WANANCHI

WAKAZI wa kijiji cha Burunde kata ya Karitu wilayani Nzega mkoani Tabora, wamewapiga, kuwaua na kuwachoma moto watu watatu kwa tuhuma za kushiriki kumuua Helena Abel na kumjeruhi mume wake, Said Msoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Juma Bwile alisematukio hilo limetokea Januari 15 mwaka huu.

Alisema kuwa Januari 12 mwaka huu Helena Abel na mume wake Said Msoma walivamiwa katika tukio hilo Helena aliuawa na Said Msoma alifanikiwa kumjeruhi mmoja wa wahalifu hao ambaye alikimbia.

Kamanda Juma alisema kuwa wananchi hao walifanya doria na kumkamata mhalifu huyo aliyejeruhiwa ambaye anaitwa Mainda Mahila na kuanza kumhoji kuhusika na mauaji hayo na kukiri kufanya hivyo.

Bwile alisema kuwa mtuhumiwa huyo aliwaeleza wananchi hao kuwa mauaji hayo alifanya kwa kuagizwa na Mama Zainabu Hamis pamoja namtoto wake aliyefahamika kwa jina la Zena Yasoda.

Wananchi hao waliwapata watuhumiwa hao wawili kisha kuanza kuwapiga hadi kufa na baadaye kuwachoma moto.

Wakati huo huo mkazi mmoja wa kijiji cha Muhugi kata ya Muhugi wilayani hapa Chenge Kasinki (75) aliuawa na watu wasiofahamika baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.