Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alieleza kuwa mkasa huo ulitokea juzi saa 7:00 mchana baada ya mvua kubwa iliyoambatana na ngurumo na radi hiyo kuwapiga na kuwasababishia mauti papo hapo.
Kamanda alibainisha kuwa mchana huo wa tukio, watu hao walikuwa shambani mwao wakilima na mvua ikaanza kunyesha hivyo wakalazimika kusitisha shughuli ya kilimo na kurejea nyumbani, lakini kabla hawajafika walikumbwa na dhahama hiyo.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa linamshikilia mkazi wakijiji cha Mpembano wilayani Sumbawanga akituhumiwa kumtupamtoto wake wa kiume muda mfupi baada ya kujifungua na kumsababishia mauti.Inadaiwa alifanya uamuzi huo kutokana na fedheha ya kupewa ujauzito na shemeji yake.
Kamanda Mwaruanda alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana wakati mtuhumiwa huyo ambaye ni bubu kumtelekeza mtoto wake huyo mchanga kwenye mtaro barabarani kijijini humo kisha akarejea nyumbani kwao.
"Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mtuhumiwa huyu alikuwa ameolewa na kuzaa naye watoto wanne lakini waliachana na mumewe kutokana na ugomvi wa kifamilia, ndipo mama huyo alianza mahusiano ya kimapenzi na shemeji yake yaani mdogo wa mumewe wa awali ambaye alimpatia ujauzito na alipobaini alikimbilia kusikojulikana," alibainisha.
Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi wa awali utakapokamilika.