MZUNGUKO WA KWANZA WA AFCON WATAWALIWA NA SARE, MZUNGUKO WA PILI KUANZA LEO

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon zinazoendelea nchini Equatorial Guinea zilikamilisha mzunguko wa kwanza kwa timu zote 16 ambapoza kundi D zilicheza Jumanne usiku.

Ambroise Oyongo aliifungia goli lake la kwanza timu yake ya Cameroon katika dakika ya 84 ilipopambana na Mali katika mchezo wao wa kundi D uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Oyongo mlinzi wa kulia aliingia katika eneo la penalti na kupokea pasi kutoka kwa Raoul Loe kabla ya kutumbukiza mpira kimiani kwa umakini mkubwa akiwa karibu na lango la Mali.

Naye Sambou Yatabare aliiwezesha Mali kuongoza mpambano huo alipopachika goli katika dakika ya 71 ya mchezo baada ya kufunga kwa kiki ya karibu akiwa ndani ya eneo la hatari.

Yatabare alifikiria kuwa ameshinda katika dakika za mwisho wakati alipotumbukiza mpira kwa kichwa langoni mwa Cameroon, lakini kibendera kilikuwa juu kuashiria kuwa tayari alikuwa ameotea.

Mali ilicheza vizuri kipindi cha kwanza kwa kupata nafasi kadha za kufunga magoli kwa kiungo wake Bakary Sako kujaribu mara mbili kutumbukiza mpira kimiani, huku akikataliwa na mlinda mlango wa Cameroon Fabrice Ondoa.

Katika mchezo wa awali wa kundi D, Ivory Coast iliambulia sare ya goli 1-1 dhidi ya Guinea. Ivory Coast ilipigana ili kupata sare hiyo, licha ya mshambuliaji wake hatari Gervinho kutolewa nje kwakadi nyekundu, mapema kipindi cha pili.

Iliwachukua Guinea dakika 36 kuongoza mtanange huo wakati Mohamed Yattara alipofunga kutokana na makosa ya mawasiliano ya walinzi wa Ivory Coast.

Gervinho, mshambuliaji wa zamani wa timu ya Arsenal, ambaye aling'ara katika mchezo huo huku moja ya mikwaju yake ikigonga mwamba wa goli la wapinzani wao, alitolewa nje ya dimba kwa kadi nyekundu katika dakika ya 58 baada ya kumpiga usoni Naby Keita. Gervinho kwa hakika alikuwa ndiye mchezaji bora kuliko wote katika mchezo huo, huku wachezaji wenzake wa timu ya Ivory Coast wakishindwa kuonyesha uwezo wao uliowapa majina makubwa katika timu zao za Ulaya kama vile Yaya Toure, ambaye alibadilishwa dakika ya 86 akitoa nafasi kwa Doukoure.

Ivory Coast ndio waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo kutokana nakusheheni wachezaji wenye vipaji kama vile Wilfried Bony, ambaye amejiunga na Manchester City kwa kitita cha pauni milioni 28(£28).
Bony alitarajiwa kushirikiana na Yaya Toure na Gervinho katika kuipatia ushindi timu yao, lakini haikuwa hivyo.

Kwa upande wake Guinea ilionyesha uwezo ulioiwezesha kufika fainali hizi za kombe la mataifa ya Afrika, licha ya kucheza mechi zao za kufuzu nje ya uwanja wao wa nyumbani kutokana na ugonjwa wa Ebola kuikumba nchi yao.

Michezo ya mzunguko wa pili inaanza leo kwa timu za kundi A. Wenyeji Equatorial Guinea yenyepointi moja itavaana na Burkina Faso isiyo na pointi katika mchezo wa kwanza kabla ya Gabon inayoongoza kundi hilo kwa kujikusanyia pointi tatu kupepetana na Congo katika mchezo wa pili wa kundi A.