VIONGOZI WA SIASA WAMTAKA RAIS KIKWETE KUTEKELEZA AHADI YA KUMNG'OA MUHONGO

Viongozi wa vyama vya siasa nchini wamemtaka rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi yake aliyoahidi wakati wa mkutano na wazee wa Dar es Salaam ya kufanya maamuzi ya kumwajibisha waziri wa nishati na madini ambaye alimweka kiporo na kudai kuwa atatoa maamuzi ndani ya siku mbili lakini hadi leo amekaa kimya.
Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Prof Iibrahim Lipumba amesema suala la viongozi wakiwemo mawaziri kuwajibika halikuanza leo hasa anaposhindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuisababishia serikali hasara au kushusha heshima ya taifa hivyo ni vyema uwajibikaji ukawa ni kwa kila mtumishi wa umma bila kubagua ili kuleta tija kwa taifa.

Kwa upande wake mjumbe wa halmashauri kuu taifa ya chama cha mapinduzi CCM Bw Najim Msenga amesema niimani ya chama chake kuwa rais atafanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya taifa kama alivyoahidi na kwamba suala hilo haliwezi kuathiri uhai wa CCM kwani bado iko imara baada ya baadhi ya watuhumiwa kuchukuliwa hatua.

Akizungumzia suala hilo katibu mkuu wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Dk Willbroad Silaa amesema hata hao waliojiuzulu na kuenguliwa uteuzi wao maadam uchunguzi ulifanywa na vyombo sahihi hadi kufikia hatua ya kupelekwa bungeni na kujadiliwa na wao kutoa maazimio watuhumiwa wote hadi sasa walipaswa wawe wamefikishwa mahakamani.

Katika mkutano wake na wazee wa Dar es Salaam uliofanyika ukumbi wa Diamond Jublee desemba 22 mwaka jana rais Kikwete alitengua uteuzi wa aliyekuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mh Anna Tibaijuka na kutangaza kumweka kiporo waziri wa nishati na madini Prof Muhongo.