MKURUGENZI MTENDAJI IRAMBA ALIPUKIWA NA BOMU

MKURUGENZI Mtendaji wa Wilaya (DED) ya Iramba, Halima Mpita (47) amenusurika kifo baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu la kutengenezwa kienyeji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema mjini hapa jana kuwa tukio hilo lilitokea Januari 2, mwaka huu saa 1.15 asubuhi wakati mkurugenzi huyo akiwa nyumbani kwake, akijiandaa kwenda kazini huku bahasha yenye mlipuko ikiwa juu ya kitanda.

Akisimulia mkasa huo, Kamanda Sedoyeka alisema Desemba 30 mwaka jana saa 4.00 asubuhi, mkurugenzi huyo alipokea bahashakutoka kwa katibu muhtasi wake naalipoifungua alikuta ujumbe usemao: "Poleni sana, hatuwezi kufanya 'dili' la milioni 90 halafu mkala peke yenu, sisi katudhulumu tukawaacha".

Alisema kuwa baada ya kusoma ujumbe huo, Mpita aliamua kwenda na bahasha hiyo nyumbani kwake, bila kujua iwapo kulikuwa na kitu kingine ndani yake.

"Ilipofika siku ya tukio (jana), akiwaanajiandaa kwenda kazini huku ile bahasha ikiwa juu ya kitanda chake tayari kuichukua, alishitukia ikilipuka kwa kishindo," alisema Kamanda Sedoyeka.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mlipuko huo ulitoboa godoro kiasi cha nusu inchi kwenda ndani na upana wa inchi mbili.

Alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na mlipuko huo, lakini jeshi la polisi likishirikiana na wataalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanashughulikia suala hilo.