WAZIRI ATIMULIWA, IGP AACHIA NGAZI

MBUNGE wa Kajiado ya Kati nchini Kenya, Joseph Nkaissery ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo wa Ndani wa nchi hiyo.

Nkaissery anachukua nafasi hiyo kutoka kwa, Joseph ole Lenku ambaye wakati wa uongozi wake Kenya imekumbwa na ukosefu mkubwa wa usalama.

Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo alitangaza uteuzi huo wakati akilituhubia taifa kuhusiana na hali ya usalama ya Kenya.

Nkaissery anatarajiwa kujiuzulu ubunge mara atakapokubali uteuzi huo.

Wakati huo huo Mkuu wa Polisi nchini Kenya Inspekta Jenerali, David Kimaiyo amejiuzulu wadhifa huo.

Kimaiyo ameachia ngazi saa chache baada ya wapiganaji wa kikundi cha al shabaab cha Somalia kuwaua watu 36 katika Kaunti Mandera nchini humo.