MWANASHERIA MKUU ANG'OKA

WAKATI Watanzania wakisubiri kusikia uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete juu ya maazimio manane yaliyotolewa na Bunge kuhusu sakata la uchotaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amejiuzulu wadhifa huo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, iliyotolewa jana na Mkurugenzi wake, Salva Rweyemamu kwa vyombo vya habari imethibitisha kujiuzulu kwa Werema kuanzia jana.

Amekuwa kwenye wadhifa huo tangu mwaka 2009, alipochukua nafasi ya Johnson Mwanyika aliyestaafu. Taarifa hiyo iliongeza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekubali ombi la kujiuzulu kwa mwanasheria huyo.

Kabla ya kugeukia taaluma ya sheria, Werema alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1979 na 1980.

Kabla ya kuwa Mwanasheria Mkuu, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tangu 2007 mpaka 2009. Mwaka 2004 hadi 2006 alikuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Werema alihitimu Shahada ya kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1984 na shahada ya pili ya sheria mwaka 1993 katika Chuo Kikuu cha American, Washington DC nchini Marekani.

Kisa ni Escrow "Katika barua yake kwa Mheshimiwa Rais Kikwete, Jaji Werema amesema kuwa ameomba kujiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusu suala la Akaunti ya Tegeta Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa iliongeza kuwa Rais Kikwete amemshukuru Jaji Werema kwa utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu. Katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliohitimishwa Novemba 28, mwaka huu, moja ya mambo makubwa yaliyoibuka na kuzua mjadala mzito ni sakata la uchotwajiwa fedha katika akaunti ya Escrow, kiasi cha kutaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, baadhi ya mawaziri na watendaji Serikali wajiuzulu.

Bunge liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh bilioni 306 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwekwa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya kukata kodi.

Hata hivyo, Jaji Werema hakusalimu amri wakati Bunge likijadili tuhuma dhidi yake, akisema anaamini alichofanya na kutaka abebeshwe msalaba na wakati fulani alishiriki kupendekeza jinsi ya kufikia maazimio ya Bunge dhidi ya watuhumiwa.

Aidha, alilalamikia uamuzi wa Bunge uliokuwa umependekeza yeye na baadhi ya vigogo wachukuliwe hatua, akidai kuwa haukuwa wa haki kwa wote waliotuhumiwa na ulifanywa kwa hasira na kufuata mkumbo.

Akizungumzia maazimio ya Bunge katika sakata la uchotaji wa fedha hizo, Jaji Werema alisema: "Kilichofanywa na Bunge ni mob justice (uamuzi wa kufuata mkumbo) kwa sababu hata waliowatuhumu, hawakupewa nafasiya kujieleza.

(Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna) Tibaijuka na (mmiliki wa hisa za IPTL, James) Rugemalira hawakusikilizwa lakini wamehukumiwa… ilionekana dhahiri jinsi Bunge linavyoingilia uhuru wa Mahakama kwa kutoizingatia hukumu ya Jaji (John) Utamwa.

"There was no justice at all (hakukuwa na haki kabisa).

Bado haijathibitika ukweli kuhusu fedha zile kama ni za umma au la. Ninyi waandishi bado mna nafasi ya kufanya uchunguzi ili muwaeleze wananchi ukweli kuhusu wasichokijua," Akijizungumzia yeye mwenyewe, alisema: "Nitasimama mwenyewe kujitetea, lakini nawaomba, tafadhalini msichafuane.
Acheni kutoa makaratasi na vitabu. Kesi hii inaendeshwa kiuchunguzi. Tuache kuchafuana."

Aidha, katika hilo, alisisitiza kuifuata Katiba ya nchi akisema ndio mwongozo unaokubalika. Werema alitaka pia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iueleze umma ili kuondoa sintofahamu iliyopo juu yammiliki halali wa fedha zilizokuwamo katika akaunti hiyo.

Bunge lilihitimisha mjadala wa kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, kwa kupitisha maazimio manane, ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Bunge hilo pia lilipendekeza kuwajibishwa kwa wajumbe wa Bodiya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco) na lilipendekeza kuwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge ambao ni mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge.

Akisoma maazimio hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema kuwa baadhi ya watu waliochukua fedha hizo ni viongozi wa umma na maofisa wa Serikali kama mawaziri, majaji, wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.

Maazimio yaliyopendekezwa ni pamoja na kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki kwamujibu wa sheria za nchi ili kukabiliana na kile kinachoonekana kuwa ni rushwa katika utoaji wa mabilioni yaliyokuwemo katika akaunti hiyo.

Azimio la tatu lilikuwa ni kuzitaka Kamati za kudumu za kuwavua nyazifa zao za wenyeviti wa kamati husika za Bunge kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge hilo na la nne likiwa ni kumwomba Rais aunde tume ya kijaji kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.