Akisimulia tukio hilo, mara baada ya kuvalishwa nishani hiyo na Rais, Kassim alisema anakumbuka ilikuwaJulai 7, mwaka jana saa 3 usiku eneo la Buguruni Malapa, ambapo akiwa kwenye eneo lake la kazi ya kuuza chipsi kama mwajiriwa, alikuja jambazi huyo na kujidai ni mteja.
Baada ya muda jambazi huyo alitoa silaha na kuanza kutishia wateja na baadhi ya wateja walikimbia huku na huko, huku bosi wake akitishiwa kwa silaha kichwani, ndipo akapata wazo la kuchukua chepe na kumpiga nalo mara mbili kichwani na ndipo jambazi huyo akaanguka na kupoteza fahamu.
Tukio hilo lilisababisha iwe rahisi kuchukua silaha aliyokuwa nayo na kisha polisi walifika na kuondoka na mtuhumiwa na kijana huyo kwenda kutoa maelezo Polisi ya jinsi alivyofanikisha tukio hilo, lisilete madhara makubwa.
"Niliwaza sasa kama huyo jambazi atachukua na hizo hela, ina maana mimi leo sitapata kitu, ujira wenyewe ni mdogo halafu niukose, nikaona njia pekee ni kumdhibiti huyo jambazi ili asilete madhara zaidi, na kweli nilifanikiwa", alisema Kassim.
Katika hatua nyingine, watunukiwa 27 walipokea nishani zao, ambapo baadhi yao ni marehemu ambao waliwakilishwa na ndugu na jamaa zao.
Katika nishani hizo, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alikuwa miongoni mwa watunukiwa wa Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50, ya Muungano Daraja la Pili.