NYALANDU NAE AJITOSA KINYANG'ANYIRO CHA URAIS

MBIO za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimechukua sura mpya baada ya jana Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kutangaza rasmi nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Nyalandu anaungana na makada wengine wa CCM wakiwemo mawaziri waandamizi katika serikali ya Rais Kikwete, mawaziri wakuu wastaafu na hata wabunge waliotangaza nia au kutajwatajwa kwa nafasi hiyo, hivyo kuongeza joto la urais ndani ya CCM.

Akizungumza katika mkutano wa kuwashukuru wapiga kura wake kwenye uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Ilongero Wilaya ya Singida Vijijini jana, Nyalandu mmoja wa waziri vijana, alisema muda wa Tanzania kupata maono mapya umefika.

"Muda wa Tanzania kupata maono mapya umefika, nitachukua hatua ya kuelekea Dodoma kuchukua fomu muda ukifika, maelfu ya watu watanisindikiza,wanawake, vijana, wanawake kutoka mikoa mbalimbali. "Naitazama mpya siku ambayo ndoto yangu itakamilika, Mungu atanyanua vyombo na kushangaza wakubwa. Najua tulikuwa wadogo kama Nazareti, lakini Ilongero imekuwa na mchango mkubwa ambao utakuwa si faida kwa wana Singida bali taifa zima la Tanzania," alisema Waziri Nyalandu.

Alisema kila mtu ambaye ametangaza nia ya kuwania urais ndani ya CCM, lazima kazi zake zipimwe kwa moto.

"Wale wote waliotangaza nia ndani ya chama chetu, kazi zao lazima zipimwe kwa moto na zianikwe hadharani ili mwisho wa siku CCM yenyewe itazipima,"alisema Nyalandu.

Aliongeza kuwa, pindi Rais Jakaya Kikwete atapohitimisha utawala wake, lazima atakabidhi kijiti kwa kizazi kipya, hivyo ndani ya CCM anaamini utakuwa mwaka wa mabadiliko na fikra mpya.

"Tuna wajibu wa kubadili fikra zetu,watu wasimamie Tanzania kuchukua hatua, licha ya ukweli kwamba CCM tuna utaratibu na itikadi zetu,tumeondoa zuio kwa vijana wasiwe waoga…tumejipanga kuwashangaza wengi,"alisema Nyalandu. Wapinzani Alisema muda wa kuwashangaza wengi unaanzia kwa vyama vya upinzani, zikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)."

Katika safari yangu ya miaka ya ubunge, Mungu ametusaidia kusonga mbele, safari moja huanzisha nyingine, nawaomba tusonge tena kwa hatua nyingine, mlianzisha safari yangu ya kisiasa nilikuwa kama mzabibu uliotoa matunda, mkaniita 'Mwanyengu' maana yake mtoto wa tai la kuishangaza dunia.

Safari hii imekuwa ya milima na mabonde kwa pamoja tumeweza, Mungu ameona,Kikwete ameona sawasawa.

"Nikitazama naona nchi hii inahitaji kubadilika kama nyingine zilizopiga hatua, Rais Kikwete amesimama kama jemedari, shujaa, mpambanaji hapa alipofika lazima tuwapongezee," alisema Nyalandu.

Alisema anatambua atapitia kwenye ushindani mkubwa ndani ya chama, ambao utatoa mtu mmoja wa kupeperusha bendera ya chama hicho kugombea urais waTanzania.

"Nawambia wale wote wanaoogopa kushindanishwa ni waoga, siku, saa,mwezi na hata mwaka utakapofika chini ya Kikwete,wachukue fomu na kupeleka kazi zao ili zipimwe," alisema Nyalandu.

Katika mchuano ndani ya CCM, Nyalandu anatarajiwa kuchuana na wanaotajwatajwa, wakiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri waandamizi, Stephen Wasira (Ofisi ya Rais, Uratibu na Mahusiano), Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Wengine ni wabunge, Dk Hamisi Kigwangalla, William Ngeleja na wengine ambao wanahusishwa, lakini hawajajianika hadharani.