WAWILI MBARONI KWA KUKAMATWA NA MENO YA TEMBO

WATU wawili wametiwa mbaroni na Polisi mjini Mpanda kwa kukutwa nameno ya tembo waliokamatwa yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 157 ndani ya basi la Adventure.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema vipande vilivyokamatwa ni 22 vyenye uzito wa kilo 46.3 sawa na tembo saba waliouawa.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Justine Baruti (39) mkazi wa kijiji cha Ivungwe – Katumba katika Kambi ya Wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi iliyoko wilayani Mlele mkoani Katavi.

Mtuhumiwa mwingine ni Boniface Hoza (40) mkazi wa kijiji cha Kalela wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Akisimulia mkasa huo Kidavashari alisema Desemba 24 mwaka huu saa 12:00 alfajiri, askari polisi wakiwa doria katika Kituo Kikuu cha mabasi kilichopo eneo la Mji wa Zamani mjini Mpanda walimtilia shaka mmoja wa watuhumiwa Jusitine Baruti ambaye akiwa na kifurushi tayari kupanda basi la abiria la Kampuni la Adventure.

Inadaiwa kuwa basi hilo la Adventure lenye nambari za usajili T992 DDT lilikuwa limepaki katika Kituo Kikuu cha mabasi mjini Mpanda tayari kwa safari ya kuelekea mjini Kigoma.

"Mtuhumiwa huyu alijaribu kuwatoroka askari hao wa doria lakini walifanikiwa kumkamata na kumweka chini ya ulinzi. Walipopekua mabegi mawili aliyokuwa nayo walikuta vipande 15vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 33.
Vipande hivi kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh 90,000,000 ni sawa na tembo wanne waliouawa," alieleza. Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, basi hilo la abiria liliamriwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kilichopo mjini Mpanda ambapo baada ya upekuzi wa kina, mtuhumiwa mwingine Boniface Hoza alikamatwa akiwa ameficha begi kwenye uvungu wa kiti alichokalia chenye namba K3.

Chanzo: Habari Leo