CIA YATUHUMIWA KWA MBINU ZAKE ZA MATESO

Ripoti ya Seneti Marekani imekosoa vikali mbinu zinazotumiwa na CIA, kuwahoji washukiwa wa uhalifu, kwamba ni za kikatili na zisizofaa.

Ripoti ya kamati ya bunge la Seneti nchini Marekani imekosoa vikali mbinu zinazotumiwa na Shirika la Ujasusi la nchi hiyo za kuwahoji washukiwa wa uhalifu na kuelezea kwamba ni za kikatili na zisizofaa.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama ya bunge la seneti Dianne Feinstein amesema katika baadhi ya matukio wanavyotendewa washukiwa hao ni sawa na mateso.

''Watu waliowekwa kizuizini walipaswa kutii mbinu zilizokuwa zikitumiwa, kuvuliwa nguo na kuachwa watupu, walikuwa wakiwekwa katika hali ya mateso ya muda mrefu.

Walikuwa wakizuiwa kulala kwa siku kadhaa, hadi saa 180- ikiwa ni sawa na siku saba na nusu, zaidi ya wiki bila ya kulala, kawaida wakiwa wamesimama au katika hali ya kuwachosha na wakati huohuo mikono yao ikiwa imefungwa pamoja juu ya vichwa.

Mbonu hizo za utesaji zilianzishwa baada ya shambulio la kigaidi la Septemba 11, mwaka 2001 nchini Marekani...''

Mbinu hizo zinazotumiwa na shirika hilo la ujasusi zimeelezwa na wabunge hao wa seneti kuwa zinamapungufu na kwamba CIA imekuwa ikitoa taarifa zisizo sahihi kwa umma.