WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA KWA KUMUUA POLISI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa hukumu ya kunyongwa hadi kufa kwa washitakiwa sita kati ya 14 waliohusika katika mauaji ya askariwa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa mkoani Morogoro na mfanyakazi wa Benki ya NMB, wakati wa uporaji wa fedha katika eneo la Ubungo Mataa.

Hata hivyo, mahakama hiyo imewaachia huru washitakiwa nane, ambao walionekana hawana hatia kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kutoridhisha.

Washitakiwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Mashaka Paulo, John Mdasha, Martine Mdashaa, Haji Kiwelu, Wickliff Limbora na Rashid Abdukadir.

Walioachiwa huru ni Rashid Lembres, Philipo Mushi, Yassin Kanyari, Hamis Daudi, Zinareth Akurike, Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd ambao ushahidi uliotolewa dhidi yao haukutosha kuwatia hatiani.

Akisoma hukumu hiyo jana, kuanzia 10: 00 asubuhi hadi saa 12:20 mchana, Jaji Projest Rugazia alisema aliwatia hatiani washitakiwa hao baada ya kusikiliza ushahidi ulitolewa na mashahidi 29wa upande wa mashtaka pamoja navielelezo 78 vilivyowasilishwa mahakamani hapo.

"Maungamo ya washitakiwa, ushahidi wa kitaalamu na utambuziwa washitakiwa katika eneo la tukio, vinaonesha wazi walikuwa nania ya kujaribu kupora Sh milioni 150 mali ya benki ya NMB, zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro tawi la Wami," alisema Jaji Rugazia.

Alisema katika siku hiyo ya huzuni ya Aprili 20, 2006, washitakiwa hao walilivamia gari kwa lengo la kupora lakini bila ya kuwa na huruma yoyote, walimimina risasi na kuwaua D 6866 Konstebo Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi Alizidi kufafanua kwamba tukio hilo la kusikitisha lilifanyika nyakati za saa 6:30 mchana, eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.

Awali, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, mahakama hiyo ilitupiliambali vielelezo muhimu vya ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji,ikiwemo ripoti saba, kati ya nane za uchunguzi wa silaha zilizotumika katika mauaji hayo.

Ripoti hizo zilitupwa baada ya Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Godfrey Luhamba, ambaye ni mtaalamu wa milipuko, kuiomba mahakama hiyo ipokee ripoti hizo kama vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo.

Mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Richard Rweyongeza, walipinga ripoti hizo kupokewa, wakidai kuwa ziliwasilishwa kinyume cha sheria kwa kuwa hazikusomwa kwa washitakiwa, wakati wa kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu.

Katika uamuzi wake, Jaji Rugazia alikubaliana na utetezi kuwa ripoti hizo hazikuwahi kusomwa kwa washitakiwa, basi mahakama hiyo haiwezi kuzipokea kwa kuwa uwasilishwaji wake ulikuwa ni kinyume sheria.


Chanzo: Habari leo