AMKATA MKE WAKE MASIKIO YOTE KUTOKANA NA WIVU WA MAPENZI

POLISI mkoani Katavi inamsaka mkazi wa kijiji cha Majimoto wilayani Mlele, Ndomo Mwandu (32) akituhumiwa kumsababishia ulemavu wa kudumu mkewe wa ndoa Agnes Sikazwe (28) kwa kumkata masikio yote mawili kwa kisu akiwa amelala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari akithibitisha mkasa huo ambao umetokea hivi karibuni kijijini humo usiku wa manane kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

"Tunaendelea kumsaka kwa udi na uvumba mshtakiwa huyu ambaye baada ya kumkata mkewe huyo masikio yake akitumia kisu na kumsababishia ulemavu wa kudumu maishani.....baada ya kumkata alikimbia na masikio hayona kutokomea kusikojulikana," alieleza Kamanda Kidavashari.

Akisimulia unyama huo, Kidavashari alieleza kuwa mara kwa mara mtuhumiwa alikuwa akisikika akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine, lakini mkewe huyo siku zote alikuwa akikanusha kwa nguvu zake zote.