WAANDISHI WA HABARI WAZUIWA KUINGIA MAHAKAMANI KESI YA IPTL

KATIKA hali ya kushangaza, Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara imewazuia waandishi wa habari kuingia mahakamani kusikiliza maombi ya kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) na Kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL) kwa Bodi ya Rufaa yaKodi nchini, kutaka Kamishna Mkuu wa TRA akamatwe na kupelekwa gerezani.

Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, waliofika mahakamani hapo jana kusikiliza maombi hayo, walishindwa kusikiliza kinachoendelea baada ya kuambiwa kuwa waandishi wamezuiwa kusikiliza.

Mmoja wa makarani wa mahakama hiyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawaruhusiwi kusikiliza maombi hayo, lakini hakuwaeleza sababu.

Maombi yenyewe Juzi PAP na IPTL ziliwasilisha maombi kwa Bodi ya Rufaa ya Kodi (TRAB) zikitaka iamuru Kamishna Mkuu wa TRA, akamatwe kwa kukiuka amri wa Bodi hiyo iliyozuia kufuta hati za kuthibitisha ulipaji wa kodi wa kampuni hiyo, katika mauzo ya hisa za IPTL.

Hatua ya TRA kufuta hati hizo ilitokana na madai kwamba PAP ilifanya udanganyifu kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi za ununuzi wa hisa, zinazodaiwa kuiwezesha kukwepa kodi ya Sh bilioni 8.68.

Maombi ya kampuni hiyo inayomilikiwa na Harbinder Singh Seith, yaliwasilishwa chini ya hati yadharura, yakiambatana na kiapo cha Mkurugenzi Mwendeshaji wa IPTL, Parthiban Chandrasakaran.

Kamishna Mkuu wa TRA anadaiwa kukaidi amri halali iliyotolewa na bodi hiyo Novemba 26 mwaka huu, iliyozuia kwa muda kuziondoa hati hizo.

"Tunaomba bodi imwamuru Kamishna Mkuu wa TRA kutekeleza amri iliyotolewa, pia bodi itoe amri ya kuondoa barua ya Kamishna ya Novemba 27 mwaka huu ambayo ilifuta hati za kodi, mpaka maombi ya msingi yatakaposikilizwa," ilidai hati hiyo ya maombi.

Hati za PAP zilizofutwa zilitolewa kwa ajili ya uuzaji wa hisa saba za IPTL kutoka Kampuni ya Mechmar kwenda Piper Links Investment, na ununuzi mwingine wa hisa hizo hizokutoka kampuni ya Piper Links kwenda PAP.

Historia ya hati Katika hati hiyo ya kiapo, Chandrasakaran alidai Desemba 23 mwaka jana walipata hati hizo za kuthibitisha walilipa kodi kwa ajili ya uuzwaji wa hisa hizo.

Anadai kwamba Novemba 19, walalamikiwa (TRA) walitoa taarifa ya siku sita kwa BRELA wakionesha nia ya kuziondoa hati hizo, kwa mazingira kwamba walalamikaji walipata mkataba feki wa mauzo ya hisa hizo.

"Kamishna si tu anabanwa na mamlaka, pia anatakiwa kufuata sheria za nchi zikiwamo za bodi, kwa kukiuka amri anapoteza sifa za kuendelea kushikilia nyadhifa hiyo aliyonayo," alidai Chandrasakaran katika hati ya kiapo.

Hata hivyo, kutokana na maombi hayo kuwasilishwa chini ya hati ya dharura, bodi hiyo mbele ya Katibu wake, Respicius Mwijage iliamuru yasikilizwe jana, lakini waandishi wakatimuliwa.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ameelezea kushangazwa na madai ya Seith, aliyokaririwa hivi karibuni katika vyombo vya habari, kuwa suala la Akaunti ya Tegeta Escrow na umilikiwa Kampuni ya IPTL lilivyoendeshwa na Bunge, limesababisha atafakari kama ataendelea kuwekeza Tanzania au la.

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya NCCR Mageuzi jana, Kafulila alidai kuwa Seith hapaswi kutafakari kwa kuwa yeye sio mwekezaji na anapaswa kukamatwa na vyombo vya dola, kujieleza namna alivyonunua IPTL.

" Ripoti ya CAG imebainisha wazi kuwa Seith alinunua IPTL kwa nyaraka za kughushi ambalo ni kosa la jinai," alisema. Hata hivyo, Seith amekuwa akisisitiza kuwa ununuzi ulifanywa kwa kihalali bila kukiuka sheria.

Aidha, Kafulila pia alisema NCCR-Mageuzi, imeanza tena ziara mkoani Kigoma kuendeleza kampeni zake za kuhamasisha wananchi kupigia kura viongozi wa chama hicho, katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Jumapili ya wiki ijao.

Kafulila anasema kampeni hizo zinaanza kesho hadi wakati wa uchaguzi na NCCR itatumia fursa hiyo kuwahabarisha wananchi kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL.

Chanzo: Habari Leo