WAKURUGENZI 6 WATIMULIWA KWA KUVURUNDA UCHAGUZI

SERIKALI imechukua hatua kali kwa wakurugenzi 17 wa halmashauri mbalimbali nchini, ambapo sita uteuzi wao umetenguliwa, watano wamesimamishwa kazi, watatu wamepewa onyo kali na watatu wamepewa onyo.

Wote hao wamepewa adhabu hiyo kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wao katika kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika Jumapili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri MkuuTawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Hawa Ghasia alisema hayo Dar es Salaam jana.

Alikuwa akitangaza uamuzi wa serikali dhidi ya wakurugenzi hao, waliosababisha kutokea kwa kasoro na kuvurugika kwa uchaguzi huo na kusababishwa kuahirishwa katika baadhi ya maeneo.

Alisema ofisi yake ilitimiza wajibu wake wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ukamilifu kwa kutoa miongozo na mafunzo kwa watendaji wa halmashauri na kuwezesha kwa fedha mikoa na halmashauri ili kugharamia maandalizi muhimu, ikiwa ni pamoja na kuandaa vifaa na karatasi za kupiga kura.

"Kimsingi kama maelekezo, miongozo na mafunzo yaliyotolewa yangezingatiwa na kila mmoja, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ungefanyika vizuri nchini kote. Wakurugenzi walikuwa wanawajibika kutambua nafasi zao kama wasimamizi wakuu katika kufanikisha uchaguzi huo," alisema.

Alisema kutokana na ripoti walizopokea kuhusu masuala yaliyojitokeza katika uchaguzi huo nidhahiri kwamba wakurugenzi wa Halmashauri zenye dosari, wameonesha udhaifu mkubwa katika kutekeleza jukumu la usimamizi wa uchaguzi, ambalo ni moja ya majukumu ya ukurugenzi

Alisema wakurugenzi hao wametenda makosa ambayo yanawaondolea sifa za kuwa wakurugenzi, ikiwemo kuchelewa kuandaa vifaa vya kupigia kura na kukosa umakini katika kuandaa vifaahasa karatasi za kupigia kura na hivyo kuwa na makosa.

Alitaja makosa mengine kuwa ni kuchelewa kupeleka vifaa kwenye vituo vya kupigia kura, uzembe katika kutekeleza majukumu yao nakutoa taarifa za kupotosha kuhusu maandalizi ya uchaguzi kuwa yamekamilika huku wakijua siyo kweli.

Aidha, alisema wapo waliodiriki kumsingizia Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuwa alipelekewa nyaraka kwa ajili ya kuzichapa, lakini akazikosea, wakati siyo kweli kwa sababu zilipelekwa kwa watoa huduma binafsi.

"Tumeridhishwa na hatua ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kumchukulia hatua mtumishi wake aliyemsingizia Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, ni jambo baya kutenda kosa na kusingizia watu au ofisi zisizohusika. Naelekeza uongozi wa Ilala umwombe radhi Mpiga Chapa Mkuu kwa upotoshaji uliotolewa dhidi yake," alisema.

Alisema, "kutokana na udhaifu waliouonesha wakurugenzi hao, kwamamlaka aliyo nayo chini ya Ibara ya 36(1)(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Rais ameridhia wachukuliwe hatua hizo," alisema.

Aliwataja wakurugenzi sita ambao uteuzi wao umetenguliwa na watapangiwa kazi za taaluma zao wakati uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini dhamira ya vitendo vyao kuwa ni Benjamin Majoya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuranga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kaliua, Abdalla Ngodu na Mkurugenzi Mtendaji wa Kasulu, Masalu Mayaya.

Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti, Goody Pamba, Mkurugenzi Mtendaji wa Sengerema, Julius Madigana na Mkurugenzi Mtendaji wa Bunda, Simon Mayeye.

Aidha, aliwataja wakurugenzi watano wanaosimamishwa kazi ya Ukurugenzi ili kupisha uchunguzi zaidi wa kiwango cha ushiriki wao katika kasoro zilizojitokeza kwenye halmashauri zao kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hanang', Felix Mabula, Mkurugenzi Mtendaji wa Mbulu, Fortunatus Fwema, Mkurugenzi Mtendaji wa Ulanga, Isabella Chilumba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kwimba, Pendo Malabeja na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela.

Ghasia aliwataja wakurugenzi watatu wanaopewa onyo kali na ambao watakuwa chini ya uangalizi ili kubaini kama wana udhaifu mwingine ili wachukuliwe hatua zaidi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Rombo, Mohamed Maje, Mkurugenzi Mtendaji wa Busega, Hamis Yuna na Mkurugenzi Mtendaji wa Muheza, Jovin Jungu.

Alitaja wakurugenzi wanaopewa onyo na kutakiwa kuongeza umakini wanapotekeleza majukumu yao kuwa ni Mkurugenzi wa Manispaa yaIlala, Isaya Mngulumi, Mkurugenzi wa Hai, Melchizedeck Humbe na Mkurugenzi wa Mvomero, Wallace Karia.

"Nasisitiza kwamba kila kiongozi na mtumishi wa TAMISEMI anao wajibuwa kutekeleza majukumu yake yotekwa weledi na uadilifu ili kuepuka kasoro zinazoweza kuepukwa," alisema.

Aidha, alisema TAMISEMI haina nia ya kuadhibu watendaji wake, lakini haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wote watakao kiuka maadili ya kazi au watakao pungukiwa uwezo wa kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa.

Wakati huo huo, matokeo ya jumla ya awali ambayo yametangazwa jana na Tamisemi, yanaonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kwa asilimia 80.58 katika matokeo ya awali ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata asilimia 13.79 na kinachofuatia ni Chama cha Wananchi (CUF) asilimia 3.6.

Chama cha NCCR-Mageuzi kimepata asilimia 0.19, TLP asilimia 0.03, NLD asilimia 0.00 na ACT asilimia 0.04.

Matokeo hayo yalitangazwa jana na Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka Tamisemi, Calist Luanda katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Alikuwa akitoa tathimini ya baadhi ya mikoa iliyofanya uchaguzi, halmashauri za miji na majiji. Kwa upande wa Vitongoji, CCM imeshinda kwa asilimia 83.05 ikifuatiwa na Chadema asilimia 13.9, CUF asilimia 36, NCCR asilimia0.09, TLP asilimia 0.03, NLD asilimia 0.00, ACT asilimia 0.02 Alisema katika vijiji 9,047, CCM imepata vijiji 7,290 , Chadema vijiji 1,248, TLP vijiji viwili, NLD vijiji viwili na UDP vijiji vinne.

Kwa upande wa mitaa 3,078 iliyofanya uchaguzi, CCM imeshinda katika mitaa 2,116, Chadema mitaa 735, CUF mitaa 235, NCCR mitaa nane ,TLP mtaa moja, ACT mitaa tisa, UDP mtaa moja na NRA mtaa moja.

Kwa upande wa vitongoji 42,824, CCM imepata vitongoji 35,564, Chadema 5,670, CUF 1,555, NCCR 80, TLP 11, NLD kitongoji kimoja, ACT vitongoji 10.

Alisema uchaguzi katika maeneo mengine, unaendelea na matokeo yatatangazwa baada ya zoezi hilo kukamilika.

Chanzo: Habari leo