WAANDISHI WAMFUNGIA MKUU WA MKOA

WAANDISHI wa habari mkoani Rukwa wamepitisha azimio la kutoandika habari zitakazomhusu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Rukwa, Stella Manyanya, kwa madai ya kutoa kauli za uzalilishaji dhidi ya wanahabari hao mkoani hapa.

Mbali na RC huyo, rungu hilo limemwangukia pia Katibu Tawala wa Mkoa Salum Chima ambaye amekuwa na uhusiana mbaya na waandishi kwa muda mrefu.

Uamuzi huo ulitangazwa jana na uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari, mkoani Rukwa (RKPC), baada ya kikao chao cha dharura kujadili kauli za mkuu huyo wa mkoa.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Peti Siyame, alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ambacho pamoja na mambo mengine, kilipokea taarifa ya kilichojili kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Rukwa (RCC)ambapo kiongozi huyo wa serikali ilidaiwa kutoa lugha zisizopendeza kwa waandishi hao.

"Maamuzi hayo yalifikiwa Septemba 28 mwaka huu katika kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Rukwa Press Klabu baada ya kujadili kwa kina kauli ya maudhi, kejeli, dharau, udhalilishajina unyanyasaji dhidi ya waandishi mbele ya wajumbe wa RCC zaidi ya 70 kwenye kikao kilichofanyika mjini Laela wilayani Sumbawanga," alisema Siyame.

Siyame pasipo kufafanua alisema mahusiano hayo yatarejea tu baada ya mkuu huyo wa mkoa na msaidizi wake watakapowaomba radhi waandishi kwenye kikao kijacho cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kwani ndiko alikozungumza lugha zisizo sahihi dhidi ya wanahabari hao.


"Sisi tuliamini kwamba mkuu wa mkoa hakutumia busara kabisa.....alipaswa atuite pembeni kama kuna tatizo na kutueleza; sio kuzungumza kwenye hadhara ya watu."Wengine ni wadau wetu wakubwa tunaheshimiana; wanajua mchango wetu kwenye maendeleo ya mkoa huu, ndio maana alivyoongea wengine waliguna na kucheka," alisema.

Manyanya ameanza kuonja chungu ya waandishi kutofanya naye kazi baada ya juzi waandishi kuondoka wakati akipanda jukwaani katika hafla fupi ya kukabidhi nyumba 20 zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa kwa watumishi wa afya iliyofanyika katika kijiji cha Chipu.

Pia wanahabari hao juzi walikataa mwaliko wake wakati Makamu wa Kwanza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Shariif Hamad, alipokuwa mkoani Rukwa kwa ajili ya kufunga Sherehe za Kiislamu za Hija Ndogo (Jitimai).

Mgogoro wa waandishi hao na viongozi wa serikali ni wa pili baadaya mwaka 2007 walipotangaza kuvunja uhusiano wa kikazi na aliyekuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa Germanus Mpongoliana baada ya kuwazuia kufanya kazi wakati wa ujio wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Saidi Mwema.

Busara za Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC), Baraza la Habari na Mwema mwenyewe ndizo zilizorudisha uhusiano kati ya waandishi na kamanda huyo.


Chanzo: Tanzania Daima