VIJANA MILIONI 2.6 WANAISHI NA VVU NCHI

Vijana milioni 2.6 wenye umri wa miaka kati 15 na 24 nchini, wanaishi na virusi vya Ukimwi.


Takwimu hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Abdoul Coulibaly, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya elimu ya jinsia na afya ya uzazi kwa vijana katika nchi 21 za Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema karibu vijana 50 katika nchi hizo huambukizwa virusi vya Ukimwi kila saa moja, huku idadi ya wasichana wakiongoza kwa maambukizi hayo.

Coulibaly alisema idadi hiyo ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana kwa Tanzania, inachangiwa na kutokuwapo kwa elimu ya kutosha ya jinsia pamoja na VVU na Ukimwi, afya ya uzazi na ukuaji wa binadamu.


Alisema asilimia kubwa ya vijana hawana uelewa wa masuala ya afya ya uzazi na jinsia, jambo ambalo husababisha kujiingiza kwenye mapenzi katika umri mdogo na kusababisha kuongezeka kwa mimba za utotoni.

Pia aliiomba serikali kuweka mikakati madhubuti ya kutoa elimu ya afya na jinsia kwa vijana kwa ajili ya kusaidia kupunguza idadi ya maambukizi kwao pamoja na mimba za utotoni zinazosababishwa na ukosefu wa elimu hiyo.

Kaimu Mkurugenzi, kitengo cha masuala mtambuka kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Laetitia Sayi, alisema changamoto ya maambukizi ya VVU kwa vijana ni kubwa na kwamba serikali kwa upande wake inafanya jitihada mbalimbali za kutatua tatizo hilo.