Kwenye mahojiano na BBC Bwana Zeidani alisema kuwa Libya inatumika kama sehemu ya kusambazia silaha katika kanda nzima.
"Hizi silaha zinapelekwa kwa wingi katika nchi jirani kwa hivyo lazima pawepo ushirikiano wa kimataifa kukomesha jambo hilo,'' alisema bwana Zeidan.
Mnamo siku ya Jumatatu serikali ya Libya ilimhoji balozi wa Marekani nchini humo kuhusu kukamatwa kwa mshukiwa wa ugaidi na mmoja wa viongozi wa kundi la al-Qaeda mjini Tripoli.
Anas al-Liby, alikuwa anasakwa kwa kuongoza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998 na baada ya zaidi ya miaka kumi aliweza kukamatwa mjini Tripoli na makomando wa Marekani.
Marekani imetetea hatua ya kukamatwa kwa gaidi huyo ikisema kuwa kilikuwa kitendo halali kuambatana na sharia za kimataifa.
Lakini bunge la Libya Jumanne lilitaka al Liby kurejeshwa nchini humo likitaja kukamatwa kwake kama kitendo cha utekaji nyara na kupuuza utawala wa Libya.
Rais Barack Obama aliambia waandishi wa habari Jumanne kuwa Marekani ina ushahidi wa kutosha kuonyesha kua Al Liby alipanga na kusaidia katika kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani na kuwaua watu wengi sana.
Obama aliongeza kuwa Al Liby atafikishwa mbele ya vyombo vya sharia.