11 WADAKWA MSITUNI WAKIJIFUA KIJESHI

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka Watanzania kujiandaa na uvamizi wa kigaidi, vijana 11 wenye umri kati ya miaka 18 na 39, wametiwa mbaroni mkoani Mtwara, wakidaiwa kuwa katika mafunzo ya kijeshi msituni, yaliyotajwa kuwa ya kutisha na hatari.

Vijana hao wanadaiwa kukutwa katika mlima wa Makolionga wilayani Nanyumbu, wakiwa katika maficho wakitumia CD zipatazo 25 zenye mafunzo mbali mbali. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen alielezeatukio hilo kuwa si la kawaida na kutaja aina ya CD zilizokuwa zikitumika.

Kwa mujibu wa Zelothe, CD hizo zilihusu Al -Shabaab, mauaji ya Osama bin Laden, Zindukeni Zanzibar, kuandaa majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu sniper.

"Pamoja na CD hizo, watuhumiwa walikuwa na zana nyingine na vyakula," alisema.

Alitaja zana hizo ni DVD player moja, Solar panel moja yenye wati 30, mapanga mawili, visu viwili, tochi moja na betri ya pikipiki namba 12. Pia, wanatuhumiwa walikutwa na simu tano za viganjani, vyombo mbalimbali vya chakula, jiko la mkaa, jiko la mafuta ya taa, taa ya chemli, baiskeli tatu, ndoo nne za maji na vitabu vya dini ya Kiislamu.

Vitu vingine walivyokutwa navyo niunga wa mahindi kilogramu 50, mbaazi kiroba kimoja chenye kilogramu 50, mahindi viroba vitatu sawa na kilogramu 150, virago vya kulalia na mfuko wa kijani, unaosadikiwa ni wa kijeshi wenye nembo ya nanga ya meli yenye mistari kulia na kushoto na nyoka katikati.

Kamanda Zelothe alitaja waliokamatwa kuwa ni Mohamed Matete (39), mkazi wa kijiji cha Sengenye ambaye anadaiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo na Hassan Omary, maarufu kama Ajili (39), mkazi wa Nalunyu.

Wengine ambao wote ni wakazi wa Likokona ni Rashidi Ismail (27), Abdallah Hamis (32), Salum Bakari maarufu Wadi (38), Ramadhan Rajabu (26), Fadhil Rajabu (20), Abbas Muhdini (32), Ismaili Chande (18), Said Mawazo (21) na Issa Abed mwenye umri wa miaka 21.

"Watuhumiwa hao wote tayari wamefikishwa mahakamani na wakati huo Polisi mkoani hapa inaendelea na upelelezi wa kina kuhusu tukio hili ambalo si la kawaida.

"Tunasaidiwa na Makao Makuu ya Polisi pamoja na kushirikisha mikoa mingine kuwanasa watu wote ambao wanatajwa kuhusishwana tukio hilo la mafunzo ya kutishana hatari," alisema Zelothe katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Jeshi la Polisi limetoa rai kwa wananchi wote wenye taarifa, inayohusu tukio la aina hiyo, watoetaarifa mapema iwezekanavyo ili watu hao wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.


Chanzo: Habari Leo