Moto uliowaka katika eneo la Jalala la kiwanda cha OK Plast Ltd kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam umesababisha hali ya taharuki ikiwemo watu kukimbia ovyo na kuacha ofisi na mali zao kwa kuhofia maisha yao baada ya Moshi mzito uliotokana na moto huo kutanda angani.
Tukio la moto huo umetokea katika eneo la wazi la kiwanda cha OK Plast Ltd inayohusika na utengenezaji wa vitu mbalimbali ikiwemo viatu aina ya kandambili pamoja na mikeka, ambapo kwa mujibu wa wenyweji wa eneo hilo wamedai kiwanda hicho cha OK Plast Ltd walikuwa wakitumia eneo hilo kutunzia mabaki ya mali gafi yao ambapo ghafla kijana mmoja amedaiwa kwenda katika eneo hilo na kuwasha moto ikisemekana alikuwa akitafuta asali kutokana na kuwepo kwa nyuki waliokuwa wakiishi kwa muda mrefu katika eneo hilo.
Moto huo ulisababisha moshi mzito kutanda angani huku vikosi vya zimamoto na baadhi ya wafanyakazi wa makampuni ya jirani na eneo la tukio wakijitahidi moto kuenea katika viwanda na makampuni mengine ambayo kwa wakati huo tayari yalikuwa yapo tupu baada ya watu kutimua mbio kuokoa maisha yao ambapo mkurugenzi wa Pb Investment bwana Mushtack Fazar aliyethibitisha kununua eneo hilo kutoka kwa kiwanda cha Ok Plast Ltd anaeeleza tukio ilivyokuwa.
Licha ya tukio hilo la moto kutokea katika eneo hilo lakini wakazi wa maeneo wamesema kiwanda hicho kinaongoza kwa kuchafua mazingira na kwamba tukio kama hilo si la kwanza ambapo afisa utawala wa kiwanda cha OK Plast Ltd bwana Martin Msamba alipofuatwa kujibu malalamiko hayo amesema ni tukio la kwanza na kwamba kijana aliyehusika kuwasha moto ameshikiliwa na polisi tayari.