RWANDA YAPUUZA VIKWAZO VYA MAREKANI

Jeshi la Rwanda limepuuzilia mbali hatua ya Marekani kuiwekea vikwazo kuhusiana na madai ya watoto kutumiwa kupigana kama wanajeshi katika vita ambavyo Rwanda inadaiwa kuunga mkono waasi wa M23 ndani ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.Shirika la habari la AFP lilimemnukuu msemaji wa jeshi la Rwanda akisema kuwa sio haki kwa Rwanda kuadhibiwa kwa mambo ambayo hayafanyiki ndani ya mipaka yake wala kutekelezwa na jeshi la Rwanda.

Joseph Nzabamwita alisema kuwa hatua ya kujumlisha Rwanda kuwa miongoni mwa nchi zinazotumia watoto kama wanajeshi haina misingi hata kidogo.

Umoja wa mataifa unatuhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasiwa M23 katika harakati zao dhidi ya serikali ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo madai ambayo Rwanda imekana.

Mnamo siku ya Alhamisi naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani kuhusu maswala ya Afrika Linda Thomas-Greenfield alisema kuwa Marekani inatumia sheria ya kuwalinda watoto ya mwaka 2008 katika kuiwekea Rwanda vikwazo ili ikome kujihusisha na vita ndani ya DRC hususan katika kuwasajili watoto kama wanajeshi.

Kwa mujibu wa afisaa mkuu katika idara ya mambo ya nje alisema kuwa hatua hiyo itaifanya Rwanda kunyimwa msaada wa kijeshi katika mwaka 2014.

Nzabamwita alinukuliwa na AFP akisema kuwa Marekani inafahamu fika kuwa Rwanda haijawahi kuunga mkono utumiaji wa watoto kama wapiganaji na kuwa licha ya vikwazo hivyo Rwanda itaendelea kushirikiana na Marekani.

Kundi la waasi la M23 lilianzishwa na waliokuwa waasi wa Tutsi waliojiunga na jeshi la DRC chini ya mkataba wa amani wa mwaka 2009 Mwaka 2012 mwezi Aprili waasi wa M23 waliwageuka waliokuwa wanajeshi wenza na kuanza uasi Mashariki mwa nchi ambako kuna utajiri mkubwa wa madini.